HOTUBA YA MWENYEKITI WA
KAMATI YA MAWASILIANO NA
UJENZI YA BARAZA LA
WAWAKILISHI, ZANZIBAR KUHUSU
MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA
YA ARDHI MAKAAZI MAJI NA
NISHATI
KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa
kunijaalia afya njema na uzima wa kuweza kusimama mbele ya Baraza lako tukufu
katika kutekeleza majukumu ya kulijenga
taifa letu. Aidha napenda kwa moyo wa dhati nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa
nafasi hii muhimu ya kutoa maoni ya Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi kuhusu
makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati kwa
mwaka wa fedha 2012/2013.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Waziri wa Wizara ya Ardhi,
Makaazi, Maji na Nishati Mheshimiwa Ramadhani Abdalla Shaaban pamoja na
watendaji wa Wizara hii wote kwa mashirkiano yao ya dhati wanayoipatia Kamati
yetu katika kutekeleza kazi zake za msingi kama ilivyoelekezwa katika
kanuni za Baraza la Wawakilishi. Aidha,
napenda kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa
Wizara hii, tunaamini kwamba uzowefu na jitihada zake zitasaidia ufanisi wa
Wizara hii ngumu, aliyokabidhiwa. Mheshimiwa
Spika, kwa moyo thabiti kabisa napenda pia kuchukua fursa hii kuwashukuru
wajumbe wote wa Kamati hii kwa mashirikiano yao wanayonipatia katika
kuhakikisha kwamba Kamati yetu inaweza kukamilisha kutekeleza kazi zake za
kuliwakilisha Baraza katika kusimamia na kufuatilia shughuli mbali mbali za
Wizara inazozisimamia.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza msisitizo wa Shukurani zangu naomba
uniruhusu niwatambue wajumbe wa waliounda Kamati hii kwa majina.
- Mhe. Makame Mshimba Mbarouk M/kiti
- Mhe. Rashid Seif Suleiman M/Mwenyekiti
- Mhe. Hassan
Hamad Omar Mjumbe
- Mhe. Subet Khamis Faki Mjumbe
- Mhe. Salma
Mussa Bilali Mjumbe
- Mhe. Shawana Bukhet Hassan Mjumbe
- Ndg. Aziza
Wazir Kheir Katibu
- Ndg. Abdalla Ali Shauri Katibu
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ardhi ni miongoni mwa Wizara muhimu sana kwa
maendeleo na mustakabali wa nchi na wananchi wa nchi yetu, hii ni kutokana na
ukweli kwamba Wizara hii imebeba sekta muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu
pamoja na maisha ya wananchi kwa ujumla, miongoni mwa sekta hizo ni pamoja
na Sekta ya Ardhi, Maji na Umeme.
Umuhimu wa sekta hizi umepelekea kuwepo kwa changamoto nyingi katika Wizara ya
Ardhi Makaazi Maji na Nishati. Kutokana na hali hiyo yamekuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
kuhusiana na uendeshaji wa taasisi zinazohusika na sekta hizo katika
kuwahudumia wananchi. Hivyo ni wajibu wa watendaji wa Wizara hii kufanya kazi
kwa uadilifu na umakini mkubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia
wananchi pamoja na taifa kwa ujumla. Aidha, kwa upande wa Serikali ni vyema ikahakikisha
kwamba inazijengea mazingira mazuri taasisi zilizomo katika wizara hii, ikiwemo
suala zima la kuwajengea uwezo watendaji wake, pamoja na kufanya tathmini ya
mara kwa mara ili waweze kuona kasoro na kuchukua hatua zinazofaa katika
kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wa shughuli za kawaida za
Wizara hii.
Mheshimwa Spika, baada ya maelezo hayo machache sasa naomba kutoa maoni
ya Kamati ya mawasiliano na Ujenzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Ardhi, Makaazi Maji na Nishati kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Hotuba
hii ya maoni ya Kamati, itagusa baadhi ya maeneo ambayo Kamati yetu imehisi
kuwa hatuna budi kuyatolea maelezo. Maeneo hayo ni kama yafuatayo;
UWAJIBIKAJI WA WAFANYAKAZI
Mheshimiwa Spika, kufanya kazi kwa kujituma na kwa ubunifu ni suala
muhimu sana katika kufikia malengo ya tasisi yoyote ile, kwa muda mrefu
tumekuwa tukishuhudia wafanya kazi wengi wa taasisi za umma wakifanya kazi kwa
mazoea bila ya kujali ni kwa kiasi gani wanaweza kufikia malengo ya kazi
zao kwa mujibu wa muongozo na mwelekeo wa
taasisi hizo. Mheshimiwa Spika, hali hii inajitokeza kutokana na ukweli kwamba
wafanyakazi wengi wa taasisi za umma hufanya kazi katika hali ya utaratibu wa
kawaida tu yaani ‘daily rootine’ bila ya kuwa wabunifu na kuzingatia mipango na
miongozo maalum ya kazi kama vile mipango kazi (action plans), sera (policies),
na dira (vision) za taasisi za Wizara wanazozifanyia kazi, hali hii hupelekea
kutokuwepo kwa ufanisi wa kazi hizo. Aidha, wafanyakazi hushindwa kujitathmini
wao wenyewe namna wanavyozisaidia taasisi
zao ili ziweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ya taasisi hizo. Aidha Kamati yetu inazidi kusisitiza kuwa ni
wajibu wa kila mtumishi wa umma kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa
na Serikali na inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi za kukemea tabia hizo na kuwataka watumishi
wa umma wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazowea ili kuleta mabadiliko
katika sekta zote na wananchi waweze kunufaika na huduma za taasisi hizo.
MAFUNZO KWA WAFANYA KAZI
Mheshimiwa Spika, Suala la
kuwajengea uwezo wafanyakazi ni muhimu sana katika kukuza ufanisi na uwezo wa
watendaji. Kamati yetu inapenda kuiomba Wizara izidishe juhudi zaidi za
kuwapatia mafunzo wafanyakazi wake, mafunzo ambayo ni muhimu sana katika kukuza
uelewa na kuwajengea uwezo wa kufanyakazi zao kwa ufanisi mkubwa. Aidha Kamati
yetu inaipongeza Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kuweza kuwapatia
mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi wapatao 84 kwa mwaka 2011/2012 katika vyuo mbali mbali, ndani na nje ya nchi
pamoja na kuwapatia mafunzo ya muda mfupi wafanya kazi wapatao 91 .
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inasomesha wafanyakazi wake kwa lengo
la kupata wataalamu katika sekta husika,
ni vyema kukawekwa mikakati maalum
kuhakikisha kuwa wafanya kazi hao wanapomaliza masomo yao wanarejea
kuitumikia Serikali hasa katika taasisi zao walizotoka. Ili kuwabana watendaji hao wanaosomeshwa na
Serikali kurudi kufanya kazi katika taasisi zao za awali ni vyema Serikali
ikazingatia kuwapatia wafanyakazi maslahi yanayoendana na utaalamu wao baada ya
kumaliza masomo yao.
IDARA YA MIPANGO, SERA, NA
UTAFITI
Mheshimiwa Spika, pamoja na malengo iliyojiwekea Wizara, Kamati inasisitia
haja ya kuwepo kwa chombo cha kusimamia ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini na
kitakachoratibu uhalali wa bei za umeme na maji. Pia Kamati inaitaka Wizara
kuharakisha nia yake ya kuweka sheria ya tathmini ya ardhi na majengo na kupatikana kwa taasisi hiyo.
Mheshimiwa Spika, sheria inayohusu uhaulishaji ardhi au mali
isiyohamishika bado ina mapungufu na ni moja kati ya chanzo cha migogoro.
Wizara inapaswa iliangalie upya na kuona haja ya kufanya marekebisho ili
kuepusha migogoro na kupatikana kwa uadilifu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuandikwa lengo la kufikisha umeme katika
vijiji vilivyokosa huduma hiyo, Idara inapaswa isimamie ufikishaji umeme huo
vijijini badala ya suala hilo kubakia kwenye maandishi tuu.
IDARA YA UTUMISHI NA
UENDESHAJI
Mheshimiwa Spika, kwa vile Idara hii ndiyo inayoshughulika na maslahi ya wafanyakazi,
Kamati inaitaka Wizara kupitia Idara hii kuendeleza mawasiliano na Wizara ya
Utumishi na Utawala Bora kutatua tatizo lililojitokeza hivi sasa la baadhi ya
watumishi wa ngazi ya chini wa Wizara hii kutofaidika na nyongeza ya mishahara
iliyoanza kulipwa mwezi wa Oktoba, 2011.
IDARA YA ARDHI NA USAJILI,
MIPANGO MIJI NA VIJIJI NA IDARA YA UPIMAJI NA RAMANI.
CHANGAMOTO ZA IDARA
MIGOGORO YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, moja kati ya
matatizo sugu katika nchi yetu ni
suala la migogoro ya ardhi ambapo mara kwa mara imekuwa ikiibuka katika sehemu
mbali mbali. Miongoni mwa migogoro hiyo
ni pamoja na kuchukuliwa kwa baadhi ya maeneo ya wananchi kwa mabavu, kufutiwa
hati kwa baadhi ya wawekezaji bila ya kufuata taratibu za sheria ya umiliki wa
ardhi. Vilele vile kuna baadhi ya wawekezaji hufutiwa hati za ardhi na kupewa
wawekezaji wengine bila kuzingatia taratibu za kisheria. Mheshimiwa Spika,
iwapo hali hii itaendelea inaweza
kupelekea wawekezaji kutokuja nchini kuwekeza na hivyo kutuletea athari kubwa ya
kiuchumi. Aidha kwa upande mwengine kumekuwa na shutuma kwa baadhi ya Masheha,
Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhusika kwa namna moja ama nyengine katika
migogoro hii, pia inawezekana kuna baadhi ya watendaji wa Serikali wachache
wasio waaminifu kuhusika katika kadhia hii. Hali hii inajitokeza kutokana na
ukweli kwamba ardhi imekuwa ni rasilmali muhimu na ambayo thamani yake
inaongezeka siku hadi siku, hivyo baadhi yao wamekuwa wakijenga tamaa ya fedha
na kukuika maadili ya kazi zao.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inasisitiza kuwa pamoja na ahadi nyingi
zinazotolewa na Serikali kuhusiana na utatuzi wa suala la migogoro ya
ardhi, ipo haja kwa Serikali yetu
kuwawajibisha wahusika wote wanaotumia nafasi zao kinyume na ilivyokusudiwa
wakiwemo baadhi ya viongozi wa Serikali na watendaji wote wanaohusika na kadhia
hiyo. Hatua hiyo italeta matumaini kwa wananchi walio wengi ambao wamekumbwa na
suala la migogoro ya ardhi na wamekata tamaa kwa sasa.
UJENZI HOLELA
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia kuendelea kwa ujenzi holela ambao hauzingatii mipango
maalum na mahitaji ya baadae “Master Plan” Kumekuwa na wimbi kubwa la uvamizi
wa maeneo ya kilimo na maeneo mengine ya wazi, ambayo yanavamiwa na kujengwa
majengo ya biashara na makaazi. Kamati yetu inatoa wito kwa Serikali
kuhakikisha kwamba maeneo ya wazi hayatolewi kwa ajili ya shuguli za biashara
na makaazi.
Mheshimiwa Spika, Kwakuwa nchi yetu ni kisiwa na haina eneo kubwa sana la
ardhi, ni vyema kwa Serikali ikalizingati hilo kwa kuweka mipango mizuri ya
matumizi ya ardhi. Ardhi ni raslimali
muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi iwapo itatumika vizuri, hivyo ipo haja
kwa Serikali kujiwekea mipango mizuri katika kuhakikisha inatenga maeneno
maalum kwa ajili ya kilimo, maeneno ya uwekezaji na maeneno ya makaazi ya
wananchi, kinyume na hali ilivyo hivi
sasa ambapo hakuna utaratibu maalum wa kudhibiti hali hiyo. Iwapo ardhi haitotumika vizuri inaweza ikawa
ni sababu ya kuliingiza taifa letu katika umasikini kwa kukosa kuweka maeneno
maalum kwa ajili ya shughuli za kilimo na uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupima maeneo na kugawanywa kwa wananchi
na taasisi bila kupeleka miundombinu siyo tu inazorotesha maendeleo ya ujenzi
bali pia inachangia katika uvamizi wa maeneo ya njia na sehemu za wazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukaribu wa kazi zinazofanywa na Idara tatu
hizi ambazo ni Idara ya Ardhi na Usajili, Idara ya Mipango Miji na Vijiji na
Idara ya Upimaji na Ramani, Kamati inatoa msisitizo kuwa ile fikra ya kuziweka
chini ya mwamvuli mmoja Idara hizi zikawa kama “Kamisheni” iharakishwe ili
ziweze kufanya kazi kwa mashirikiano na kurahisisha kazi za Idara hizo kwa
kuwahudumia wananchi kwa wakati na hatimaye kupunguza migogoro ambayo imekua
ikiibuka na kuongezeka kila siku.
Mheshimiwa Spika, Kamati pale inapoamua kukutana na Idara zote tatu kwa
pamoja umuhimu wa kufanya hivyo huonekana ambapo maafisa kutoka katika Idara
hizo walishirikiana kujibu hoja za Wajumbe
na kutoa rai zao ambazo ni za msingi katika kuziimarisha taasisi hizo,
na kupelekea Kikao hicho kwenda kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Spika, Kwa vile Wizara hii kupitia Idara tatu hizi ndiyo
inayogawa maeneo ya ujenzi wa nyumba, viwanda, mahoteli na mengineyo, na kuwa
ni dhamana wa kufuatilia ripoti ya tathmini ya mazingira (Environmental Impact
Assessment- E I A) ni dhahiri kuwa Idara ya Mazingira mahali pake ni hapa. Kwa
vile Idara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Kilimo wanafuatilia Mazingira ya
baharini na maeneo ya kilimo, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais ingepewa jukumu
la uratibu wa mazingira yote kwa ujumla.
MAHAKAMA YA ARDHI
Mheshimiwa Spika, Bado tunakabiliwa na tatizo la mrundikano wa kesi za
ardhi hususan katika kisiwa cha Unguja, Wakati Kamati yetu ikipitia bajeti ya
Wizara ilielezwa kuwa kati ya kesi 95 zilizofunguliwa Unguja kati ya Julai hadi
Machi 2012 ni kesi 15 tu ndizo zilizotolewa hukumu, hali hii inatokana na
uchache wa Mahakimu katika mahakama hizo, ili kuondokana na tatizo hilo Kamati
yetu inashauri Wizara ichukue hatua za dharura kwa kuiombea Mahakama ya Ardhi
iongezewe Mahakimu pamoja na kufungua Mahakama za Ardhi za Mikoa.
Aidha, Kamati yetu inaiomba Wizara katika Bajeti ya
2012/2013 iangalie uwezekano wa kuwajengea mazingira bora ya kimaslahi
watendaji wa Mahakama ya Ardhi kutokana na unyeti wa majukumu yao, ni vyema
watendaji hawa wakajengewa mazingira bora ya kimaslahi ili kuepusha uwezekano
wa kuchukua rushwa wakati wa kutekeleza kazi zao.
IDARA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika, Ili kukuza uchumi wa nchi yetu suala la kuwepo kwa
nishati ya uhakika ya umeme ni suala la lazima, na hatuwezi
kuendelea bila ya kuwa na nishati ya uhakika, moja kati ya vitu vya msingi ambavyo wawekezaji huangalia kabla ya kuekeza ni kuwepo kwa nishati ya uhakika.
Kwa muda mrefu sasa nchi yetu imekosa
umeme wa uhakika na ambao hautoshelezi mahitaji yetu ya kawaida. Katika hali
kama hii athari yake ni kupoteza fursa nyingi za wawekezaji kuja kuekeza katika
nchi yetu, hususan katika sekta za viwanda sekta ambayo kimsingi huhitaji
kuwepo kwa nishati ya umeme ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imefarajika kusikia kwamba, ripoti ya
wataalamu wa Jumuiya ya Ulaya ‘European Union’ (EU) kuhusu uwezekano wa
Zanzibar kuzalisha nishati mbadala,
inayoonesha kwamba, Zanzibar inaweza kuzalisha umeme mbadala kwa kutumia
upepo, takataka na jua. Kamati yetu inaishauri Serikali kuifanyia kazi ripoti
hiyo ya wataalamu kuhusu njia muafaka
kwa uzalishaji wa umeme ili kuharakisha mchakato wake wa kupatikana kwa
nishati mbadala ya uhakika na ambayo itakuwa ina gharama nafuu ili kuwapunguzia ugumu wa
maisha wananchi kwa kuwa hali ya hivi sasa
sio nzuri ambapo bei ya nishati hiyo iko juu na inazidi kupanda siku
hadi siku.
NISHATI YA MAFUTA
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imefarajika na taarifa ya Idara ya Nishati
kwamba kwa hivi sasa masuala yanayohusu
nishati yatasimamiwa moja kwa moja na Idara hiyo badala ya kusimamiwa na
Wizara ya Fedha. Aidha, tumefarijika
kupata taarifa kwamba Wizara inaandaa
Rasimu ya Sheria ya usamabazaji wa Mafuta (Zanizbar Petroleum Supply Act), pamoja
na Sheria ya udhibiti wa mafuta, ili
bidhaa ya mafuta iweze kusimamiwa na sekta husika kwa ufanisi zaidi na kuwa na
mdhibiti mahususi wa bidhaa ya mafuta. Kamati yetu inaisisitiza Serikali
kuzingatia kuwaandaa watendaji wa Idara ya Nishati kwa kuwapatia mafunzo
yanayohusiana na masuala ya Nishati ili kuwaweka tayari na mabadiliko ambayo
tunayatarajia likiwemo suala la kuanzisha nishati mbadala pamoja na suala la uchimbaji wa mafuta.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utegemezi mkubwa wa nishati ya umeme hapa Zanzibar
kutoka Tanzania bara, Idara hii ina jukumu kubwa la kutafuta mbinu za nishati
mbadala. Kutokana na jukumu hilo ambalo lingehitaji utafiti, taaluma na
mikakati ya hali ya juu ambayo itaweza kuipeleka nchi katika nishati inayotumia
nyenzo tulizonazo na ambayo haiharibu mazingira ( Environmental friendly).
Mheshimiwa Spika, kutokana na bajeti ndogo ya Idara hii, Kamati inaona
kuwa dalili za kufikiwa mapema malengo hayo hayapo, hivyo Kamati inaishauri
Serikali inapopanga bajeti iangalie na unyeti wa malengo yake kwa kuziwekea
bajeti ya kutosha Idara zake ili ziweze kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaendelea kusisitiza kuwa Idara hii ikabidhiwe
mambo yote yanayohusu nishati ikiwemo udhamini juu ya uingizaji wa mafuta
nchini, pamoja na upangaji wa bei na uhalali wa kuyashughulikia makampuni
yanayoingiza na kuuza mafuta ya petroli na mengineyo.
SHIRIKA LA UMEME
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme lingehitaji kufanya marekebisho makubwa
katika uendeshaji wake. Ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 40 kwa mkupuo si
utaratibu mzuri bali kama gharama zimeongezeka za uendeshaji ni vyema kwa
Shirika na Serikali kwa ujumla kupandisha bei ya umeme kidogo kidogo kulingana
na hali za wananchi zilivyo.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme (ZECO) halina budi kujifanyia tathmini
ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuwapunguzia wananchi gharama za
kuunganisha na kulipia umeme. Aidha udhibiti wa mapato ya Serikali siyo tu
ungeliletea faida Shirika bali pia ungepunguza mzigo kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Shirika halina budi kuweka transfoma za akiba za ukubwa
tofauti Unguja na Pemba, ili kuwapunguzia usumbufu wananchi wakati transfoma
inapoharibika.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Umeme lina azma nzuri ya
kuleta vifaa vya kutosha kwa
ajili ya kuwaungia umeme wananchi, hata hivyo Kamati inasisitiza kuwa jambo
hilo lifanywe kwa vitendo na Kamati inafuatilia kwa kina ahadi hiyo ili kuona
utekelezaji wake unafanikiwa.
MAMLAKA YA MAJI
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya maji (ZAWA) ni taasisi muhimu sana iliyobeba
jukumu la uhai kwa maelfu ya wananchiwa Zanzibar, kwani “MAJI NI UHAI”.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaikumbusha Mamlaka kuchukua
tahadhari zote za kiutawala na kiufundi kuhakikisha kuwa maji yanapatikana
katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa pump za akiba, mabomba na mafundi stadi
ni sehemu muhimu za kutoa huduma hii. Ujenzi wa matangi yanayohimili hali ya
hewa yetu kunasaidia sana usambazaji maji badala ya kutumia njia ya moja kwa
moja. Hata tathmini ya uwezo wa pump zetu unaweza kufanyika.
Mheshimiwa Spika, ili kufuatilia kwa karibu upatikanaji na ukosefu wa
huduma ya maji, Kamati inasisitiza ufungaji wa mabomba ya maji kwa zone maalum
katika sehemu za miji na kuunganishwa katika maeneo ya dharura. Utaratibu huu
utatoa taarifa mapema “Early warning system” katika maeneo ambayo maji
yanakosekana na kujua mapungufu yaliyopo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuipa uwezo Mamlaka ya Maji, Kamati inawaomba
wananchi wote wanaopata huduma hii ya maji kulipia huduma hiyo bila ya
kuchelewa.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Ili Wizara iweze kutekeleza malengo yake na kutoa huduma
safi kwa wananchi nawaomba wajumbe wenzangu tuipokee, kuichangia na baadae
kuipitisha bajeti ya Wizara ya T.sh. 80,082,728,000 zikiwemo Tsh. 6,708,000,000
kwa kazi za kawaida na T.sh 73,374,728,000 kwa kazi za Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, sasa napenda
kutamka kuwa kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Ziwani, naiunga mkono hotuba hii
ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa mwaka wa fedha 2012/
2013.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
………………………
RASHID SEIF
SULEIMAN,
M/MWENYEKITI,
KAMATI YA
MAWASILIANO NA UJENZI
BARAZA LA WAWAKILISHI
No comments:
Post a Comment