Na Haji Nassor, Pemba
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Major Mstaafu Juma Kassim Tindwa amewataka waandishi wa habari chini, kutumia kalamu zao vizuri, kwa kuwaelimisha wananchi juu ya utaratibu unaotakiwa wa utoaji wa maoni ili kukamilisha uundwaji wa katiba mpya.
Alisema kuwa wakati huu wa tume ikiwa hapa Zanzibar, kwa kukusanya maoni kwa ajili ya uundwaji wa katiba mpya, baadhi ya wananchi wamekuwa hawaelewi jinsi ya utoaji wa maoni na kusababisha kueleza masuala yasioendana na hadudi rejea za tume.
Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza hayo jana huko ofisini kwake mjini Chake Chake alipokua akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar (ZJMMC) ambao wapo Kisiwani Pemba kwa mafunzo ya vitendo (field).
Alisema kuwa waandishi wa habari wanafasi kubwa ya kutoa taaluma juu ya mambo kadhaa yalipo nchini, ikiwa ni pamoja na suala la utoaji wa maoni, na endapo watazitumia vyema kalamu zao watawasaidia wananchi ili kuelewa namna ya utoaji wa maoni hayo.
Alieleza kuwa kazi ya kuelimisha wananchi juu ya utoaji bora wa maoni , sio ya taasisi husika pekee, bali kila sekta inayo nafasi hiyo ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari kutumia vitengo vyao mbali mbali kama vile utengenezaji wa vipindi, uandishi wa makala.
‘’Nyinyi waandishi wa habari mnayo nafasi kubwa iwe ni kuandaa vipindi vya radio na tv, habari za kawaida, makala, na vipindi maalum ili kuwalekeza wananchi kipi wakifanye na kipi wakiepuke wakati tume ikifika hapa Pemba’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba Juma Kassim Tindwa amewataka wananchi kuhakikisha wanatoa maoni kwa mijibu wa utaratibu unaotakiwa na tume, ili maoni yao yaweze kuingizwa kwenye katiba mpya.
Alifafanua katika Mkoa Kusini Unguja, amekuwa akishuhudia baadhi ya wananchi wakielezea masuala ambayo hayaendani na lengo hilo, ambapo hilo linaiwezesha tume kuyachukua au kuyaacha kwa vile hayamo kwenye hadudi rejea.
‘’Wapo wananchi kwa mfano anasema rais wa Zanzibar asichaguliwe Dodoma, jamani hili halihusiani na hadudi rejea za uundwaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, toeni maoni mambo ya msingi’’,alifafanua Tindwa.
Tume ya kukusanya maoni inatarajiwa kuwasili Kisiwani Pemba Juni 15 na kuanza kukusanya maoni Juni 17 kwa Mkoa wa Kusini Pemba, mara tu watakapo maliza zoezi hilo kwa Mkoa wa Kusini Unguja.
No comments:
Post a Comment