Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), wamesema Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, amewadanganya Wazanzibari kwa kuwaruhusu kutoa maoni ya kupinga Muungano kinyume na sheria ya mabadiliko ya Katiba.
Walitoa kauli hiyo wakati wakichagia makadirio na matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba katika kikao cha Baraza la Wawakilishi visiwani hapa jana.
Mwakilishi wa Magomeni (CCM), Salmin Awadh Salmin, alisema haikuwa mwafaka kwa Jaji Warioba kuruhusu watu wanaopinga Muungano kutoa maoni mbele ya tume yake kulingana na kifungu cha cha 9 (1)((a) kwa vile kinakataza kutoa maoni kama hayo.
Alisema kifungu hicho kimesema: “Tume itaongozwa na misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha mambo yafuatayo, kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, mfumo wa kiutawala wa Kijamhuri, uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama.
Awadh, ambaye pia mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kifungu cha 17 cha sheria ya mabadiliko ya Katiba, pia kimesema tume hiyo itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na hadidu rejea ya mpango kazi wa tume hiyo.
Alisema kitendo cha Jaji Warioba, kuwataka wananchi wa Zanzibar wanaopinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutoa maoni mbele ya tume hiyo, ni sawa ni kuwadanganya na kuwapotezea muda wao.
“Mheshimiwa Spika, Jaji Warioba, katujaza kitu katika vichwa matokeo yake tunajadili kitu ambacho hakitakiwi kujadiliwa kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania,” alisema huku akipigiwa makofi.
Awadh, alisema bahati mbaya na kikundi cha Jumuiya ya Uamsho na mihadhara ya dini ya Kislamu (Jumiki) badala ya kuelimisha watu juu ya elimu ya uraia badala yake kinafanya kazi ya kuwapotosha wananchi wa Zanzibar.
Alisema uamsho wanafanya kampeni kwa wananchi watoe maoni ya kuukataa Muungano wakati watu watake wasitake, Muungano utaendelea kuwepo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.
Alisema Zanzibar itakuja kujuta kutokana na nafasi nzuri iliyopatikana ya kutatua kero za Muungano na kutaka serikali kutoa elimu ya uraia juu mambo ya Katiba ili kuwajengea uelewa wananchi juu ya mambo ya Muungano.
Awadh, alisema yapo mambo ya msingi ya kujadili kama namna ya kumpata Rais wa Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, nafasi za kazi katika Muungano, mgawo wa fedha kuwa wa kikatiba na nafasi ya Zanzibar katika ushirikiano wa kimataifa.
Mwakilishi wa Kwamtipura (CCM), Hamza Hassan Juma, alisema yanayotokea katika ukusanyaji wa maoni ya Katiba Zanzibar ni sawa na kuanika karafuu wakati wa masika.
Alisema wananchi wengi wa Zanzibar hawafahamu Katiba na ndiyo maana wanakwenda kutoa maoni yasiyokuwa na manufaa kwa Zanzibar na wananchi wake kutokana na serikali kushindwa kutoa elimu ya uraia kabla ya kazi ya kukusanya maoni kuanza kufanyika mwaka huu.
Aidha alisema wananchi wa Zanzibar wanatumia muda mwingi katika mikusanyiko ya kijamii na masikani kubishana suala la Muungano wakati suala hilo halitakiwi kuzungumzwa kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya Katiba.
Naye Mwakilishi wa Mji Mkongwe na Naibu Katibu Mkuu wa (CUF) Ismail Jussa Ladhu, alisema wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na Jamhuri yake itakayokuwa na mamlaka yake kamili ya kujiamulia katika mambo ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa.
Alisema mfumo wa Muungano wa sasa umepitwa na wakati na badala yake kuwepo na Muungano wa mkataba kwa kuhakikisha kuna kuwepo na Serikali ya Tanganyika, Zanzibar pamoja na Serikali ya Muungano inayotokana na mkataba maalum.
Mwakilishi wa Kiwani (CUF), Hija Hassan Hija, alisema Tume ya mabadiliko ya Katiba imeanza kazi ya kukusanya maoni vibaya kutokana na baadhi ya majimbo kupangiwa kituo kimoja wakati majimbo mengine vituo karibu vitatu.
Alisema hatakuwa mgumu kupitisha bajeti ya wizara hiyo hadi serikali itakapotoa maelezo kwa nini jimbo lake limepangiwa kituo kimoja na kuwanyima nafasi wananchi hasa wanaoishi katika visiwa vidogo Zanzibar.
Naye Mwakilishi wa Wawi (CUF), Saleh Nassor Juma, alisema Tume ya Warioba imeanza kuleta wasiwasi katika jamii kutokana na kitendo cha kuwatenganisha askari na raia katika utoaji wa maoni ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Alisema kambi za jeshi kisiwani Pemba wanaishi askari wengi kutoka Tanzania bara, jambo ambalo linaweza kutoa sura tofauti juu ya mtazamo wa Muungano kutokana na ratiba kuwapa muda mwingi askari na kuwapa muda mdogo raia.
Mwakilishi wa Chake Chake, Ali Omar Shehe (CUF) alisema ameshtushwa sana kuibuka mtindo wa watu kuandikiwa maoni ya kutoa kwa kutumia bahasha na kupewa posho ya Sh. 1,000 bila ya kuzingatia kuwa kitendo hicho ni kinyume na huru wa kikatiba wa wananchi kutoa maoni yao.
Alisema matatizo hayo yanatokana na serikali kushindwa kutoa elimu ya uraia kwa wananchi wake kuhusu mambo ya katiba kabla ya kufanyika kazi ya kukusanya maoni mwaka huu.
Mapema akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakary Khamis Bakary, alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu cha 18(1), kila mwanachi ana uhuru wa kutoa maoni yake isipokuwa maoni hayo yasikiuke mipaka kwa kukera mwananchi mwingine au kuvuruga maslahi ya umma.
Chanzo : Nipashe
No comments:
Post a Comment