Habari za Punde

Chamber:Bei ya umeme yakwamisha biashara, uwekezaji

Na Hafsa Golo
RAIS wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima (ZNCCIA), Mbarouk Mohammed amesema bei kubwa ya umeme na kutokuwepo kwa uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo, ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha mazingira ya kibiashara.

Rais huyo alieleza hayo jana katika ukumbi wa ofisi za Jumuiya hiyo zilizopo jengo la Livingstone liliopo Kinazini mjini hapa na kueleza kuwa umeme Zanzibar umepandishwa kwa asilimia 50 ikilinganishwa na watumiaji wa Tanzania bara.

Alisema nishati ya umeme Zanzibar imekuwa ikilipwa kwa bei kubwa Zanzibar ikilinganishwa na Tanzania bara, jambo ambalo linafanya suala la uwekezaji kuwa gumu.

Rais huyo alisema utafiti uliofanywa na mtaalamu mzalendo uchumi Dk.Mohammed Hafidh Khalfan umebaini kuwa upandishwaji ovyo wa nishati ya umeme ni miongoni mwa kikwazo kitakachosababisha kutofikiwa dira ya maendeleo ya mwaka 2020 ambayo inabashiri kuinua vipato vya wananchi hadi kufikia tabaka la kati.

“Bei ya umeme ni miongoni mwa kikwazo kikubwa katika sekta ya kukua kwa maendeleo ya biashara Zanzibar na bila ya kuwepo kwa suluhisho la kudumu juu ya tatizo hilo, ndoto ya kuwa natabaka la kati kwa wananchi katika mwaka 2020 halitafikiwa”, Rais huyo alimnukuu mtaalamu huyo.

Alisema ili mazingira ya uwekezaji wa viwanda yaweze kutekelezwa vyema ni lazima uwepo umeme wa uhakika ambayo utaviwezesha viwanda kuzalisha bidhaa pamoja na utoaji wa huduma.

Aidha Rais huyo wa Chamber, alisema bei ya umeme inapopandishwa katika nchi husababisha kuongezeka kwa matumizi hali ambayo inachangia kuzorotesha mfumo mzima wa biashara hasa kwenye manunuzi kwa wateja wa kawaida ambao ni wananchi.

Rais huyo alisema kwa kawaida pindipo bei ya umeme inapopandishwa, viwanda vya uzalishaji navyo hulazimika kupandisha bei ya bidhaa inazozizalisha hali inayosababisha usumbufu kwa watumiaji.

Aidha Rais huyo alisema upandishaji wa umeme kwa kiasi kikubwa huchangia kuzorota kwa uzalishaji kwa wamiliki wa viwanda na wawekezaji.

Aidha alibainisha tatizo jengine ambalo ZECO imekuwa ikikumbana nalo ni lile la kuwepo kwa wadaiwa sugu zikiwemo taasisi pamoja na wizi wa umeme.

Alisema ni vyema kabla ya shirika la Umeme kupandisha bei ya umeme, ni vyema sekta binafsi ikashirikishwa katika kutoa maoni.

Rais huyo alibainisha kuwa Zanzibar lazima iwe na mipango ya kuwa na umeme wake utakaokuwa wa uhakika na kuacha kutegemea umeme kutoka TANESCO ambao unauzwa kwa bei mbaya.

“Serikali kwa kushirikiana na shirika la umeme na wadau wengine mbalimbali ni vyema wakakaa pamoja kutafuta njia za kuanzisha umeme ikiwa wa jenereta, solar, na njia nyengine lakini Zanzibar na umeme wake, kwani shughuli nyingi zinakwama kuendelea kutokana na kutokuwa na umeme wa uhakika”, alisema.

Shirika la umeme Zanzibar (ZECO) kuanzia Jun1 1 mwaka huu liliongeza bei za umeme mabapo imekuwa 161/kutoka shilingi 120/kwa watumiaji umeme majumbani na viwanda vidogo imekuwa shilingi 172 kutoka shilingi 140, viwanda vikubwa imekuwa shilingi 169/kutoka shilingi 142/ na kwa upande wataa za barabarani imekuwa shilingi 141kutoka shilingi 105 na gharama za huduma kwa wateja zimeongezeka kutuka shilingi 1,500 hadi shilingi 2,000.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.