Habari za Punde

Dk Shein ahesabiwa katika sensa ya watu na makaazi leo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Moahmed Shein,akijiandikisha na  familia yake kwa Karani Asia Hassan Mussa,(kushoto) katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi, lililoanza leo nchini kote,Rais  akiwa katika  Shehia ya Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,(kulia ) Mke wa Rais Mama Mwanamwema Shein,  [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Moahmed Shein,na Mkewe Mama Mwanamwema Shein,pamoja na familia yao walipojiandikisha  kwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi, lililoanza leo nchini kote, wakiwa katika Shehia ya Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,   [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
 
Na Rajab Mkasaba
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na familia yake leo asubuhi wamekamilisha zoezi la sensa ya watu na makaazi linaloendelea nchi nzima hapo nyumbani kwake Migombani Mjini Unguja, na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
 
Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kukamilisha zoezi la sensa lililoanza katika Kaya yake hiyo, majira ya saa tatu na nusu asubuhi na kuweza kujibu masuala yote yaliokuwemo kwenye dodoso maalum lililotayarishwa kwa ajili ya zoezi hilo.
 
Dk. Shein  akiwa pamoja na mama Mwanamwema Shein, alitoa pongezi na shukurani kwa uongozi, Maafisa na washiriki wote wa zoezi hilo muhimu linaloendelea nchini kote na kueleza jinsi lilivyoanza vizuri.
 
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa wananchi watatoa majibu  na mashirikiano mazuri kwa maafisa wa sensa ili kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo  ya nchi na wananchi wake kwa jumla.
 
Aidha, Dk. Shein aliwataka Maafisa wa sensa na wote watakaoshiriki katika zoezi hilo kuwa na subira kutokana na kazi ya zoezi hilo kuwa ngumu.
 
Akitoa neno la shukurani Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bwana Mohammed Hafidh, alimshukuru Dk. Shein kwa kushiriki kwake kikamilifu katika zoezi hilo hali ambayo itakuwa ni darasa kwa wananchi wote kutokana na umuhimu wa zoezi hilo.
 
Mtwakimu huyo, alieleza kuwa zoezi hilo lilianza rasmi saa sita ya usiku wa kuamkia leo, zoezi ambalo lina madodoso ya aina tano kutokana na umuhimu wake mkubwa ambapo miongoni mwa madodoso hayo ni pamoja na lile lililoanza siku tatu kabla ya sensa.
 
Alieleza kuwa miongoni mwa madodoso hayo ni pamoja na dodoso la jamii, dodoso linalowahusu watu wasio makaazi maalum, dodoso linalohusu Kaya za Jumuiya pamoja na lile la  Wasafiri.
 
Kwa mujibu wa maelezo yake Mtwakwimu Mkuu huyo alieleza kuwa matokeo ya awali ya  zoezi hilo yanatarajiwa kutolewa Disemba 31 mwaka huu na taarifa zote za zoezi hilo linatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu.
 
Pamoja na hayo, alizieleza aina mbili za dodoso zinazotumika ambazo ni dodoso fupi ambazo zitatumika kwa asilimia 30 na dodoso refu ambazo zitatumika kwa asilimia 70.
 
Katika taarifa yake aliyoitoa hapo juzi kwa wananchi, Dk. Shein alisema kuwa lengo la kukusanya taarifa za zoezi hilo ni kuiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutekeleza na kutathmini mipango iliyopangwa ili kubaini hatua iliyofikiwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana.
 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimuomba Mwnyezi Mungu kujaalia amani, utulivu katika kulifanikisha zoezi hilo bila ya dosari ili sifa ya Wazanzibari ipande na kuwataka wananchi kudhihirisha uzalendo na ustaarabu wao kwa kushiriki kikamilifu katika sensa.
 
Pia, Dk. Shein aliitumia fursa hiyo kwa mara nyengine tena kuwasihi wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu hapa nchini ambapo litaiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutekeleza na kutathmini mipango iliyopangwa ili kubaini hatua iliyofikiwa pamoja na mafanikio yaliopatikana.
 
Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano baada ya Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hapo mwaka 1964 ambapo sensa nyengine zilizotangulia zilifanyika mwaka 1967, 1978,1988 na mwaka 2002.
 
Miongoni mwa taarifa zinazokusanywa katika zoezi hilo ni pamoja na umri, jinsia, hali ya uzazi na vifo, ulemavu, hali ya makaazi na taarifa zinazohusu maisha ya kila siku ya wananchi pamoja na hali ya makaazi wanamoishi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.