Wachezaji wafungiwa kuchezea klabu, Taifa Stars
Cannavaro, Morris watoswa kwa kuongoza uasi
Na Salum Vuai, Maelezo
KAMATI Tendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imeamua kuivunja timu ya Taifa Zanzibar Heroes, pamoja na kuwafungia kucheza mpira ndani na nje ya nchi wachezaji wote wa timu hiyo ambao hawajarejesha fedha za zawadi ya ushindi wa tatu wa mashindano ya Tusker Challenge.
Adhabu hiyo haiwahusu baadhi ya wachezaji waliorejesha fedha hizo, baada ya kikosi hicho kukaidi maagizo ya viongozi wao walipokuwa nchini Uganda, na kuamua kugawana fedha hizo dola elfu kumi.
Wachezaji walionusurika na adhabu hiyo ambao walirejesha dola hizo mia tano walizopata kila mmoja, ni Issa Othman ‘Amasha’, Adeyum Saleh, Abdallah Othman, Abdallah Rashid, Suleiman Hamad na Jaku Joma.
Kamati hiyo ilifanya kikao cha dharura jana mchana katika ofisi za ZFA Kiembesamaki, chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa chama hicho Unguja, Haji Ameir, akiwemo pia Rais wa ZFA Amani Ibrahim Makungu, na viongozi wote waliofuatana na timu hiyo nchini Uganda.
Wajumbe hao kwa kauli moja, walikubaliana kuwa kitendo kilichofanywa na wachezaji hao ni utovu wa nidhamu, na kimekitia doa chama hicho, serikali na Wazanzibari wote kwa jumla.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Katibu Mkuu wa ZFA Kassim Haji Salum, alisema kuwa, kutokana na aibu waliyoitia nchi, kuanzia jana, wachezaji hao wamefungiwa kucheza mpira na klabu yoyote, na pia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Aidha, alisema kuwa, ZFA inawataka nahodha wa timu Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake Aggrey Morris, ambao wametajwa kuongoza uasi huo, kufika ofisi za ZFA keshokutwa Ijumaa wakati wa saa saba mchana, kutoa maelezo juu ya utovu wa nidhamu wanaodaiwa kuufanya, kabla hatua kubwa zaidi hazijachukuliwa.
“Baada ya kukidhalilisha chama, serikali na wananchi wote, tumeona tuwape adhabu hiyo, huku nao wakipewa haki ya kujieleza juu ya sababu zilizowashawishi kufanya hayo. Adhabu hii pia inawahusu wale waliomo Taifa Stars na klabu za ligi kuu Tanzania Bara”, alifafanua Katibu huyo.
Mapema, Rais wa ZFA Amani Ibrahim Makungu, alieleza kufadhaishwa na kitendo cha wachezaji hao, hasa baada ya kuzungumza na Nadir Haroub kwa simu na kumtaka awatulize wenzake ili wazirejeshe fedha kwa uongozi, na kuwaahidi mambo mazuri watakaporejea nchini.
“Majibu aliyonipa yalinifadhaisha sana kwani alisema kuwa fedha hawazirudishi huku akidai ZFA imeshawaibia miaka miwili nyuma. Kwa hatua ya kwanza tunawafungia, lakini tutamwita aje athibitishe kauli zake, na kama hazina ukweli aombe radhi kwetu na Wazanzibari kwa jumla”, alisema Makungu.
Timu ya Zanzibar Heroes ilimaliza ya tatu katika mashindano ya Chalenji yaliyomalizika Jumamosi iliyopita mjini Kampala Uganda, na kuzawadiwa dola elfu kumi, ambazo wachezaji waligawana zote bila kuuhusisha uongozi kwa hofu ya kupunjwa.
No comments:
Post a Comment