Habari za Punde

Simba, Jamhuri vitani

Bandari mikononi mwa Tusker FC
Ni ufunguzi michuano ya Mapinduzi
Na Salum Vuai, Maelezo
 
 
PAZIA la michuano ya Kombe la Mapinduzi, linatarajiwa kufunguliwa leo, kwa mechi mbili za kundi A, zitakazochezwa uwanja wa Amaan wakati wa alasiri na usiku.
 
  Katika pambano litakalochezwa wakati wa saa kumi kamili alasiri, Bandari ya Zanzibar itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Tusker ya Kenya, timu inayoundwa na wachezaji warefu na wenye uzoefu mkubwa kimataifa.
 
Kutokana na ushindi ambao Tusker ilipata katika mechi zake mbili za kirafiki dhidi ya Yanga (1-0) na Simba (3-0) wiki iliyopita mjni Dar es Salaam, mashabiki watarajie burudani mwanana,ambapo Bandari inatarajiwa kutotishika na majina ili kusaka pointi tatu muhimu.


  Katika mchezo huo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk.
 
Baada ya patashika hiyo, uwanja wa Amaan utakuwa mashakani tena mnamo saa 2:00 usiku, pale mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba, watakapoikabili Jamhuri kutoka Pemba. Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mtanange huo unaotazamiwa kuwa wa kukata na shoka kutokana na kuwa timu zote mbili zinajuana vyema na zinacheza soka la kuvutia.
 
Timu zote hizo zitashuka dimbani zikiwa na makocha wapya baada ya kuondoka kwa walimu wao wa awali, Milovan Cirkovic kwa Simba na Ahmed Shubeir wa Jamhuri.
 
Kwa sasa, Simba imeanza kunolewa na Mfaransa Patrick Liewig aliyewasili nchini juzi kurithi mikoba ya Milovan aliyetimuliwa, huku Jamhuri ikifundishwa na Sebastian Mkomo aliyeajiwa baada ya Shubeir kuipa kisogo timu hiyo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.