Na Husna Mohammed
WIZARA ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, imekiri kutofanikiwa katika mradi mkubwa wa usambazaji maji kwa baadhi ya maeneo ya mjini kutokana na sababu mbalimbali.
Waziri wa Wizara hiyo, Ramadhan Abdalla Shaaban, alisema hayo jana katika taarifa yake ya mafanikio ya utekelezaji wa wizara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ya serikali ya swamu ya saba 2010-2012
Alizitaja sababu zilizopelekea kutofanikiwa kwa mradi huo kuwa ni pamoja na uchakavu wa mabomba, ambapo maji mengi yamekuwa yakipotea ardhini kabla ya kuwafikia watumiaji.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo wizara hivi sasa inategemea kutekeleza mradi mwengine katika mkoa wa Mjini Magharibi ambao unategemewa kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Sambamba na kukamilika mradi wa maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi, wizara pia imeweza kuendeleza utekelezaji wa miradi midogo midogo kwa ulazaji wa mabomba mapya, uchimbaji wa visima, ununuzi na utiaji wa pampu mpya, ujenzi wa vituo na upelekaji wa umeme katika maeneo ya miradi.
Akizungumzia kuhusu usambazaji wa maji vijijini alisema unalenga zaidi katika vijiji ambavyo huduma ya maji bado haipatikani vizuri.
Aidha alisema utekelezaji wake umegawiwa katika miradi midogo midogo kwa mujibu wa maeneo yaliyokaribiana ambapo kazi zilizotekelezwa zinatofatuana kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
Waziri Shaaban alisema miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na uchimbaji wa visima, ujenzi wa matangi, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo na uwekeji wa Pampu na Mota.
“Katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, wizara yangu kupitia Mamlaka ya Maji imetekeleza miradi mbali mbali katika maeneo ya vijijini Unguja na Pemba,” alisema.
Akizungumzia sekta ya umeme waziri Shaaban, alisema wizara kupitia shirika lake la umeme imeendeleza kazi za usambazaji umeme vijijini kwa mfuko wa Serikali, Shirika la Umeme pamoja na mchango wa wanavijiji.
Katika kufanikisha kazi hiyo, shirika limefanikiwa kusambaza umeme wa laini kubwa vijijini katika vijiji vya Kijichi, Fuoni meli tano, Fuoni kidarajani, Bumbwisudi, Dole, Kianga, Matemwe mkunguni, Kianga kidarajani kwa Unguja na Pujini kijili, Mgogoni, Msengele na Kilindi kwa Pemba.
Aidha alisema shirika linalenga kuimarisha mradi wa njia za kusambaza umeme kwenye maeneo ya kusini, kaskazini na Fumba Unguja, hasa baada ya mradi wa jjia ya pili ya umeme kukamilika.
Ujenzi wa njia za umeme unaendelea sambamba na ujenzi wa vituo vipya vya umeme vya Mtoni, Mwanyanya na Welezo na kwa sasa upo katika hatua ya kukamilisha ujenzi wake.
“Mradi huu unafadhiliwa na serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA pamoja na mchango wa serikali uliotumika kwa kufidia mali na mazao ya wananchi walioathiriwa kwa njia moja au nyengine. Mradi huu unatarajiwa kumalizika mapema mwaka 2013,” alisema.
Pia waziri Shaaban alisema katika Sekta ya Ujenzi Wizara imefanikiwa kuendeleza ujenzi wa nyumba za maendeleo Mpapa, mradi wa nyumba hizi unafadhaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo hadi hivi sasa Idara ya Ujenzi imekamilisha.
“Kazi za upigaji wa Plasta kwa jengo zima umekamilika ikiwa ni pamoja na uwekaji wa fitting ya maji safi na maji machafu, uwekaji wa shata za milango tayari umeanza na matayarisho ya uwekaji wa zege ya juu kwa ajili ya kuzuia maji ya mvua yamekamilka,” alisema.
No comments:
Post a Comment