Habari za Punde

Papa:Nimejiuzulu kwa mapenzi ya Mungu



VATICAN, Italia
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict wa XVI alionekana tena hadharani kwa mara ya mwisho jana wakati alipowahutubia wafuasi wake katika ibada ya Jumapili.
Katika hotuba yake, Papa Benedict alisema amejiuzulu kwa mapenzi ya Mungu na uamuzi wake huo kamwe hauna maana kuwa amelitelekeza kanisa.

Akizungumza kwa hisia na sauti nzito, Papa aliwambia maelfu kwa maelfu ya Wakiristu waliokusanyika katika kanisa la St. Peter kuwa ataendelea kuliombea kanisa katika kipindi chote kilichosalia cha maisha yake.
"Mwenyezi Mungu ndie alieniambia nipumzike kutokana na afya yangu na kwa maslahi na utukufu wa kanisa,” alisema huku akishangiriwa na umati mkubwa wa wafuasi wake ambao walimtakia maisha marefu.

"Lakini hii haina maana kwamba nimelitelekeza kanisa. Kawaida, kama Mwenyezi Mungu amenitaka nipumzike ni lazima niheshimu kwa sababu naweza kuendelea kumtumikia kwa mapenzi yale yale,” alisema.
Hotuba ya jana itakuwa ya mwisho kwa Papa kabla ya Jumatano kufanya mkutano wake wa mwisho kama Papa na baadae kukutana na Makadinali siku ya Alkhamis.
Nafasi ya upapa itakuwa wazi kuanzia saa 2:00 asubuhi kwa saa za Italia siku ya Alkhamis.

Makadinali wataanza kukutana siku ya Ijumaa kuandaa mkutano wa makadinali (conclave) ambao ni makhasusi kwa kumchagua Papa mpya.
Kiongozi huyo (85) ambae anaongoza Wakatoliki wapatao bilioni 1.2 duniani kote alisema anajiuzulu kwa sababu afya yake imezorota na hana uwezo wa kutosha wa kulitumikia kanisa.
Aliwashuru waumini wa dini ya kikiristu na kuwambia:”Siku zote tutaendelea kuwa pamoja”.
Polisi wa Vatican wanasema zaidi ya watu 100,000 walimiminika katika makao makuu ya Papa kwenda kumsikiliza kiongozi wao.
Benedict anakuwa Papa wa kwanza kujiuzulu katika kipindi cha miaka 600 iliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.