Mkurugenzi wa Habari Maelezo Zanzibar Omar Yussuf Chunda amesema njia pekee ya kuwawezesha Wanahabari kufanya majukumu yao kwa ufanisi mkubwa ni kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo katika fani yao.
Amesema mafunzo ndio njia muhimu ya kuwafahamisha Wanahabari mabadiliko na mbinu muhimu zinazotumika katika uandishi wa kisasa wenye lengo la kuhudumia jamii kikamilifu.
Mkurugenzi Chunda ameyasema hayo alipokuwa akifunga Semina ya siku tano ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Idara yake katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Kikwajuni mjini Zanzibar
Amesema fani ya habari hubadilika katika mifumo tofauti ya kiuandishi na kwamba ujuzi huo unahitajika ili kuwawezesha Waandishi kufanya kazi kwa ari na kasi kubwa.
Mkurugenzi Chunda ameongeza kuwa Idara yake pia inatarajia kuwapatia mafunzo Wanahabari mwezi April mwaka huu kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uingereza Nchini.
Aidha Chunda amewataka Washiriki wa Semina hiyo kuyatumia vizuri mafunzo waliyoyapata ili yaweze kuwasaidia katika kufanya majukumu yao ya kila siku.
Mapema Mkufunzi wa Mafunzo hayo Salim Said Salim aliwataka waandishi hao kufichua maovu yanayotokea katika jamii sambamba na kuzingatia maadili ya kazi zao.
Amesema Zanzibar kuna maovu mbalimbali ambayo hutendeka na kwamba Waandishi ndio watu muhimu wa kuyafichua ili kuilinda jamii na matatizo hayo.
Ameongeza kuwa Ufisadi unaofanywa na baadhi ya watu haupaswi kufumbiwa mamcho kwani kufanya hivyo ni kusaliti maslahi ya taifa.
“Nakuombeni fanyeni uchunguzi wa kubaini ufisadi na maovu yanayofanyika ili kuinusuru Zanzibar na maovu hayo kinyume na hivyo nanyie mtakuwa mnahusika kuchochea maovu hayo” Alisisitiza Salim
Salim amewasisitiza Waandishi hao kujitolea kufanya habari za kiuchunguzi bila kuegemea upande wowote na kuwataka wazingatie maslahi ya Taifa badala ya maslahi binafsi.
Semina hiyo ya Siku tano iliyofadhiliwa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ilikuwa na lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa Idara ya Habari Maelezo.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
22-2-2013
No comments:
Post a Comment