Habari za Punde

SMZ yajidhatiti kukabili tatizo la ajira. • WB kuendelea kuisaidia Zanzibar

Na Said Ameir,Ikulu
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada kuimarisha sekta za utalii, kilimo, uvuvi na viwanda vidogo vidogo ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alisema hayo alipozungumza na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia (WB) kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi,Phillipe Dongier.

Hata hivyo, alisema jitihada hizo zinakabiliwa na changamoto ya kukosa uwezo wa kuziwezsha sekta hizo kujiimarisha hadi kufikia hatua ya kutoa ajira zinazotarajiwa.

“Sekta za kilimo, uvuvi, utalii na viwanda vidogo vidogo zikiimarishwa ipasavyo zitapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la ajira linalowakabili vijana wengi wakiwemo waliohitimu elimu ya juu Zanzibar,” alieleza.

Kwa hiyo alisema serikali imekuwa na inaendelea kukaribisha washirika mbalimbali ikiwemo sekta binafsi kushiriki katika kuendeleza na kuimarisha sekta hizo.

Alifafanua kuwa hivi sasa serikali imejipanga kuifanya sekta ya kilimo iweze kuvutia vijana wengi kwa kuhimiza kilimo cha umwagiliaji pamoja na matumzi ya zana za kisasa pamoja na mbegu bora.

“Ni sekta ambayo inaweza kutoa ajira nyingi lakini tunahitaji kuiimarisha kwa kuipatia na kuhimiza matumizi ya zana za kisasa na mbegu bora na ndio kitu ambacho serikali yangu inachokifanya ili vijana wengi wavutiwe na sekta hii,”alifafanua Dk.Shein.

Kwa upande wa sekta ya utalii, alisema kwa kuvishirikisha na kuviwezesha vikundi vya kijasiriamali vya kinamama na vijana kutoa huduma mbalimbali katika sekta hiyo, kutasaidia kuongeza nafasi za ajira na sekta hiyo kuwa na manufaa zaidi kwa wananchi wa Zanzibar.

Kuhusu sekta ya uvuvi, alisema Zanzibar haijatumika ipasavyo kama ilivyo katika nchi nyingine za Mauritius, Sycheles na Msumbiji ambako mbali ya kuingiza mapato makubwa kwa nchi hizo lakini imetoa ajira nyingi.

Alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia kwa misaada yake kwa Tanzania hususan Zanzibar ambayo alisema mbali ya kuchangia maendeleo lakini pia imeongeza ari kwa serikali na wananchi wa Zanzibar kuongeza juhudi katika kutekeleza majukumu yao.

“Tumefarijika sana na misaada yenu ambayo imetuwezesha kutekeleza miradi mingi ambayo kwa hakika kama ingekuwa ni nguvu zetu pekee hapana shaka tusingefikia hatua ilivyo sasa,” alisema.

Naye Phillippe Dongier alimhakikishia Rais wa Zanzibar kuwa Benki ya Dunia iko tayari kuendelea kushirikiana na serikali na wananchi wa Zanzibar katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na jitihada zao za kujiletea maendeleo.

“Sisi Benki ya Dunia tuko tayari kuendelea kushirikiana na serikali ya Zanzibar na kuziunga mkono jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo na nimefurahishwa kwa matokeo mazuri ya hatua ambazo serikali imechukua kuimarisha uchumi wake,”alibainisha.

Akizungumzia suala la ajira,alieleza kuwa suala hilo ni changamoto katika nchi nyingi hivi sasa ambapo imeonekana kuwa si kila uwekezaji hutoa nafasi nyingi za ajira hivyo inatakiwa mikakati ya kuwekeza katika miradi ambayo inatoa ajira nyingi.

Benki ya Dunia hivi sasa inafadhili miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa uimarishaji elimu ya msingi, mradi wa mazingira wa fukwe za bahari na mradi wa kuimarisha huduma katika miji ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.