Habari za Punde

Utunzaji wa mashamba ya Serikali unasikitisha

Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali Asili zisizorejesheka Nd. Said Juma Ali akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuhusu juhudi za uimarishaji wa miche ya Mikarafuu katika shamba la Kilimo Makuwe Kaskazini Pemba.Naibu Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji Nishati na Madini Mh. Makame Mwadini na kushoto yao ni Naibu Waziri Biashara, Viwanda na Masoko Mh. Thawaiba Kisasi

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitembelea baadhi ya mashamba ya Serikali alipokuwa katika ziara ya siku mbili Kisiwani Pemba
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitoa agizo kwa watendaji wa Wizara ya Ardhi kuandaa utaratibu maalum wa usafishwaji wa mashamba ya Serikali Kisiwani Pemba.

Shamba la Serikali liliopo Shungi Mkoa wa Kusini Pemba likionekana kukosa huduma za usafishaji kwa kipindi kirefu.
Picha na Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame,OMPR
Wakati Serikali kuu ikitegemea kupata mapato yake kutokana na vianzio vyake mbali mbali lakini hali ya utunzaji na uendelezaji wa mashamba ya Serikali katika maeneo mengi hapa Nchini ambayo nayo ni miongoni mwa vyanzo vya mapato hayo bado ni ya kusikitisha.
Hali hiyo imejidhihirisha wakati wa ziara ya siku mbili ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kukagua mashamba ya Serikali katika Mikoa miwili Kisiwani Pemba.
Akiambatana na Viongozi wa Wizara za Biashara, Kilimo na Ardhi katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea kusikitishwa kwake kutokana na kutokushughulikiwa kwa mashamba hayo hasa yale ya mikarafuu ambayo baadhi yake hushughulikiwa wakati wa mzao.
Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Idara ya Ardhi na Usajili Kisiwani Pemba kuandaa utaratibu maalum wa kuwakabidhi wananchi walio tayari kuyahuisha na baadaye kupewa upendeleo maalum wa kukodishwa wakati wa mzao wake.
Alisema mfumo unaotumiwa hivi sasa wa uhifadhi wa mashamba ya Serikali umekosa huduma za msingi na kupelekea uzalishaji hafifu wakati jamii inaelewa kwamba Zao la Karafuu bado linaendelea kuwa ni muhimili wa uchumi wa Taifa.
“ Jamani hili ndio zao linalolipatia pato Taifa letu. Kwa kweli Serikali haina tegemezi kipindi hichi isipokuwa Karafuu. Sasa nitalazimika kuja tena kukagua mashamba haya mara tuu baada ya kumalizika kwa Kikao cha Baraza la Wawakilishi cha Mwezi wa April mwaka huu kufuatilia hatua mlizochukuliwa”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikubaliana na ushauri wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi wa kutafutwa vijana watakaokuwa makini kutekeleza kazi hiyo ya usafishaji wa mashamba hayo chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya na uratibu wa Watendaji wa Taasisi za Ardhi.
Alifahamisha kwamba Jamii na Serikali ilifanya makosa ya kutoliendeleza zao la karafuu kipindi ambacho bidhaa hii iliteremka bei katika masoko ya Kimataifa.
Alisema Taasisi zinazosimamia zao hili pamoja na wananchi walipunguza kasi ya kuhuisha miti ya mikarafuu pamoja na kuiimarisha ile iliyopo kufutia kuanguka kwa soko lake katika kipindi kilichopita.
“ Tulifanya makosa wakati zao la Karafuu lilipoporomoka bei katika soko la kimataifa, Jamii na Serikali tuliliachia hili ambalo lilikuwa kosa jengine”. Alisisitiza Balozi Seif ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya kufuatilia na kusimamia Mashamba ya Serikali.
Naye Afisa mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji ,Nishati na Madini Ndugu Hemed Salum alisema ipo haja kwa Serikali kwa wakati huu kuandaa utaratibu wa kutenga fungu maalum litakalowezesha huduma za usafishaji wa Mashamba ya Serikali.
Ndugu Hemed alisema wakati maafisa wake wakiendelea na mipango ya kuyatambua mashamba hao Kisiwani Pemba nguvu kazi ya usafishaji huo ipo kutokana na Vijana wengi kujitokeza kufanya kazi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionyesha kufarajika kwake wakati akilikagua shamba la Majaribio la Kilimo liliopo Makuwe Wilaya ya Micheweni kutokana na hatua za utunzaji mzuri zilizofikiwa na Watendaji wa Wizara ya Kilimo.
Afisa Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali asili zisizorejesheka Ndugu Said Juma Ali alimueleza Balozi Seif kwamba zaidi ya shilingi Milioni 28,000,000/- zilipatikana katika msimu uliopita wa mzao wa karafuu baada ya kukodishwa shamba hilo la ekari 200.
Ndugu Said alifahamisha kwamba mbali ya vilimo mchanganyiko vinavyoendeshwa kwenye shamba hilo lakini pia watendaji hao wanashughulikia uoteshaji wa miche ya mikarafuu kwa ajili ya kuigawa kwa wakulima lengo likiwa kufikia miche milioni moja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mashamba ya mikarafuu ya vijiji vya Shungi, Kigope, jaani na uweni Mkoa wa Kusini Pemba na Mtambwe , Ukunjwi, Bungala pamoja na Makuwe yaliyomo Mkoa wa Kaskazini Pemba. 
 

 
 

 





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.