Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Afya,katika utelezaji wa Kazi za Wizara hiyo kwa kipindi cha miezi
mitatu,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
mitatu,[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Na Rajab Mkasaba
WIZARA ya Afya imeeleza kuwa inaendelea na mchakato wa kutafuta vifaa ili kuweza kuanzisha redio maalum (Afya FM Redio) itakayosadia katika utoaji elimu ya afya kwa jamii.
Hayo yameelezwa leo na uongozi wa Wizara ya Afya katika mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai, 2012- Machi, 2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee pia, walishiriki ambapo Wizara hiyo ilieleza ilivyoweka azma hiyo kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata taarifa mbali mbali za afya.
Uongozi huo chini ya Waziri wake Mhe. Juma Duni, alieleza kuwa kuwepo kwa redio hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutengeza na kuonesha vipindi kadhaa vya redio ambayo vitaelimisha jamii juu ya masuala mbali mbali ya afya.
Wizara hiyo ilieleza kuwa bado inaendelea kutoa elimu ya afya kwa wananchi ili kuweza kujikinga na maradhi mbali mbali yakiwemo ya kuambukiza na yasio ya kuambukiza ambapo jumla ya vipindi 69 vya elimu ya afya vimesharushwa hewani kupitia redio na televisheni hapa nchini.
Waziri Juma Duni alieleza kuwa sekta ya afya ni miongoni mwa sekta muhimu katika maendeleo ya taifa lolote ulimwenguni hivyo ipo haja ya kuhakikisha Wazanzibari wote wanapata huduma bora za afya.
Alisisitiza kuwa Wizara ya Afya ndiyo iliyopewa jukumu la kuhakikisha huduma za afya za kinga na tiba zinaimarika na kuendeleza ustawi wa watu wa Zanzibar kwa kutilia mkazo zaidi wanawake, watoto na makundi wengine yanayoishi katika mazingira magumu.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa tayari hatua za awali za ujenzi wa wodi ya mama wajawazito katika hospitali ya Wete zimeshaanza ikiwa ni pamoja na kuitisha tenda ya kutafuta wakandarasi watakaosimamia ujenzi wa wodi hiyo.
Wizara hiyo ilieleza kuwa ujenzi huo unasimamiwa na Mradi wa kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB na unatarajiwa kumaliza ifikapo Juni, 2014.
Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza azma yake ya kujenga jengo la ghorofa moja la Ofisi ya Mradi Shirikishi wa Afya ya Uzazi na Mtoto, jengo ambalo linajengwa katika eneo la hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu Mjini Zanzibar.
Ilielezwa kuwa ujenzi uko katika hatua nzuri na tayari ghorofa ya juu imeshajengwa na kilichobaki ni kuendelea na hatua za mwisho za ujenzi ikiwemo kuezekwa na kumalizwa matengenezo ya mwisho.
Uongozi huo pia, ulieleza juhudi unazozichukua katika kuhakikisha tatizo la upungufu wa wafanyakazi kwenye hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba linapatiwa ufumbuzi ama kuondoka kabisa kutokana na ajira mpya kwenye Wizara hiyo.
Pia, uongozi huo ulieleza azma yake ya kutoa elimu kwa wananchi wanaokwenda kuwaangalia wagonjwa katika hospitali Kuu ya MnaziMmoja kufuata taratibu zilizowekwa na hospitali hiyo ili kuepusha usumbufu uliopo hivi sasa.
Kwa upande wake Dk. Shein alisisitiza haja ya kutoa elimu ya afya kwa wananchi hasa juu ya maradhi ya Malaria kwani Zanzibar inatambulika duniani kote kutokana na mafanikio iliyoyapata hivyo kuna haja ya kusonga mbele badala ya kurudi nyuma.
Alieleza kuwa ipo haja ya kuongeza nguvu na kasi ya kuelimishana juu ya maradhi hayo huku akieleza juhudi za serikali katika kuondosha maradhi hayo ambazo zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa juhudi zake inazoendelea kuzichukua katika kutoa huduma ya afya kwa wananchi huku akiwasisitiza watendaji wa wizara hiyo kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kufuata maadili ya kazi zao.
Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi wa Wizara hiyo mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuendeleza Chuo cha Udaktari cha Zanzibar kiliopo chini ya ukufunzi wa Madaktari bingwa kutoka Cuba hivi sasa ambapo hivi karibuni Chuo hicho kinatarajiwa kuwa chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
No comments:
Post a Comment