Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Bi. Joyce Mapunjo, akifungua warsha ya kujadili mpango wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini (PVoC) uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Bureau Veritas, Bw. Jean-Michel Marnoto (katikati), akifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Warsha ya kujadili mpango wa ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini (PVoC) uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Mratibu wa Bureau Veritas, Bw. Michael Maryogo na wa tatu ni Meneja wa Bureau Veritas Tanzania, Bw. Cedric Serre.
Wadau mbalimbali wakifuatilia kwa umakini hotuba ya ufunguzi wa Warsha ya kujadili Mpango wa Ukaguzi wa Bidhaa kabla ya kuingizwa nchini (PVoC) uliofanyika kwenye Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam
Mhina Shabani, Dar es Salaam
Wakala wa Kimataifa wa ukaguzi wa ubora na viwango vya bidhaa, Bureau Veritas (BV), kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wametoa tahadhali kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa nchini kuzingatia uzalishaji na biashara zenye tija na viwango vya ubora kulingana na muktadha wa soko la leo kimataifa, vinginevyo watashindwa kushindana.
Akizungumza kwenye warsha iliyojumuisha wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Bureau Veritas, Jean-Michel Marnoto, alisema taifa lolote linalozalisha bidhaa kwa kuzingatia ubora ni dhahiri hujisafishia njia ya kufikia maendeleo kwa nyanja zote, hususan kiuchumi na kijamii.“Ndio sababu tumekutana hapa ili kuelimishana na kubadilishana mawazo ya namna ya kukidhi viwango na ubora kulingana na mahitaji ya soko. Na kikubwa kinachotupa matumaini ni jinsi serikali ya Tanzania ilivyojitoa na kuonesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha siku hadi siku inaweka mazingira bora katika sekta ya viwanda na uzalishaji kwa maendeleo endelevu ya taifa na watu wake,” alisema Marnoto
Marnoto aliongeza kuwa BV kama wakala anayetambulika Kimataifa katika ukaguzi wa bidhaa sanjari na kuthibitisha na kisha kutoa cheti cha ubora kwa bidhaa husika, kwa kipindi kirefu imejijengea mwonekano mzuri na kukubalika kimataifa, huku ikiamini hiyo ni fahari, heshima na jambo la kujivunia na la thamani katika taswira ya dunia.
“Tunachukua fursa hii kuungana na wateja wetu na watanzania kwa ujumla katika kubadilishana mazuri tuliyonayo kwa ustawi na maendeleo, jambo la kuungana ndio hasa azma yetu kufikia dira ya kule tunakokwenda,” alisema Marnoto
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, alisema kwa miaka mingi sasa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, zimekuwa zikifanya jitihada kuhakikisha zinakidhi vigezo vya uzalishaji wa bidhaa zake kulingana na mahitaji ya soko, jitihada ambazo hata hivyo zimekuwa zikikwamishwa na changamoto kadhaa zikiwemo rushwa na mifumo thabiti ya usimamizi.
Aliongeza kwa kuwahakikishia wadau wa sekta hiyo kuwa serikali kwa kushirikiana na jumuiya za kimataifa na taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) imeazimia kuboresha mazingira ya kiufanisi katika kufikia malengo, viwango na vigezo vya ubora kulingana na uhalisia sambamba na mahitaji ya soko kwa bidhaa husika.
Bureau Veritas ilianzishwa mwaka 1828, lengo likiwa ni kushirikiana na taasisi za serikali ya nchi husika zinazotoa huduma ya ukaguzi wa viwango na ubora wa bidhaa na kuthibitisha ubora wake, na kisha kutoa cheti cha ubora kwa kampuni au taasisi husika iliyokidhi viwango na ubora, kinachojulikana kama ‘Certificate of Conformity CoS’
No comments:
Post a Comment