Habari za Punde

Wafanyakazi kampuni ya H/Young wadaiwa kuwadhalilisha wafanyakazi wa kike


Na Masanja Mabula,Pemba
BAADHI ya wafanyakazi wa kampuni ya H/Young inayojenga barabara kisiwani Pemba wanadaiwa kuwadhalilisha kimapenzi wafanyakazi wao wa kike na kisha kuwapiga picha ambazo zinadaiwa kusambaa kwenye simu za mkononi.

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia moja ya picha zinazodaiwa kusambazwa.

Hata hivyo, habari hizo zimekanushwa vikali na Mkuu wa Wilaya ya Wete ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Omar Khamis Othman.

Mkuu wa wilaya hiyo amewataka wananchi kuacha kuipaka matope kampuni hiyo.

Alisema taarifa hizo hazina ukweli, kwani baada ya kufuatilia wameshindwa kubaini wahusika wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Wete, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi walio na ushahidi juu ya picha hizo wapeleke ushahidi wao ofisini kwake ili hatua zinazofaa zichukuliwe.

Alisema ofisi ya Wilaya imefanya ziara ya kuwatafuta wahusika wa vitendo hivyo kutokana na picha hizo, lakini wameshindwa kupatikana kwani kila sehemu walizokwenda walipelekwa sehemu nyingine.

"Mwanzo tuliambiwa anayedaiwa kudhalilishwa ni mkaazi wa Pandani, kufika Pandani tukaambiwa kuwa ni mkaazi wa Piki, wakati wakaazi wa Piki wao wakatuambia kuwa ni mkaazi wa Bopwe, na tulipofika Bopwe tukaambiwa anaishi Kinyasini," alisema.

Aidha amewataka wananchi kuacha kuzua mambo ambayo hayana ushahidi wake, kwani kitendo hicho kinawakosesha uwaminifu watendaji wa kampuni hiyo katika jamii wanayofanya kazi.

Mwandishi wa habari hizi katika kutaka kujua undani juu ya suala hilo , alifuatilia katika Shehia ya Kinyasini ambapo sheha wa shehia hiyo, Raiya Othman naye alisema kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote.

Alisema yeye binafsi ameziona picha hizo kwenye mtandao kupitia simu ya mkononi na kusema msichana anaedaiwa kufanyiwa vitendo hivyo sio mkaazi wa Kinyasini.

"Baada ya kuiona sura ya msichana huyo nilibaini kwamba sio mkaazi wa Kinyasini, pia nina wasiwasi kwamba huenda akawa sio mkaazi wa kisiwa cha Pemba ," alieleza Sheha huyo.

Kwa upande wake Sheha wa Pandani, Said Hamad Shehe ambaye kampuni ya H/Young ndiko yaliko makao makuu yake amelezea kusikitishwa na taarifa hizo na kusema zimelenga kuiondoshea uwamini kampuni hiyo ambayo ipo nchini kwa ajili wa ujenzi wa barabara za mkoa wa kaskazini Pemba.

Aliwashauri wananchi kufanya utafiti na uchunguzi kabla ya kueneza uvumi ambao unaizidi kuwaweka katika wakati mgumu watendaji wa kampuni hiyo katika jamii inayowazunguka.

"Ni jambo la kusikitisha, kwani taarifa hizi zimewafanya wafanyakazi wa kampuni hii kuwa na wasiwasi kwani jamii inayowazunguka inaweza kukosa imani nao, wakati wao kila wakati wako barabarani," alisema Sheha.

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye hakuta jina lake kuandikwa gazetini alisema kama kuna mtu ana ushahidi juu ya suala hilo walipeleke kwenye vyombo vya sheria.

Alisema kuedelea kuzungumza mitaani hakuwezi kusaidia kupatikana na ufumbuzi na kwamba hali hiyo inawafanya wazazi kuingia wasiwasi juu wa watoto wao wanaofanya kazi na kampuni hiyo.

Wananchi wanawashutumu wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kufanya mapenzi na wafanyakazi wao na baadae kuwapiga picha ambazo zinadaiwa kusambazwa kwenye simu za mkononi.

1 comment:

  1. Huyu Mkuu wa Wilaya anaonesha ameshahongwa. Atashindwaje kuthibitisha wahusika wa hatia hii? Kama kweli anataka kutenda wajibu wake angewauliza wale mabinti nani anawadhalilisha na kuwapiga picha chafu. Lakini kwa vile mpaka sasa jamaa zake hawajaaibishwa yuko tayari kupokea bahasha za hao wageni na kufumbia macho madhambi yao. Ole wako Bw Mkuu wa Wilaya siku atakopigwa mkeo au binti yako picha ya uchi. Utashindwa kusema ng'e!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.