Habari za Punde

DK Shein Ahimiza Kuzingatia Uhalisia katika Kupanga Bajeti.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                    17 Novemba, 2013
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara na Idara za Serikali zimekumbushwa kuandaa bajeti kwa kuzingatia uhalisia wa gharama katika soko ili kusaidia Serikali kufanya maamuzi sahihi ya kibajeti.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema hayo wakati akihitimisha Kikao cha Kujadili Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2012/2013 na robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2013/2014 kilichofanyika jana Ikulu.
Mheshimiwa Rais alieleza kuwa mtindo wa kuweka makisio makubwa yasiyolingana na hali halisi ya bei ya vitu na huduma katika soko kunapelekea Serikali kuwa na bajeti isiyo halisi na kuathiri utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa hiyo alisema kutokana na Serikali kuamua kuingia katika mfumo wa bajeti unaozingatia matokeo wizara na Idara za Serikali hazina budi kuhakikisha michakato ya kupanga bajeti inakuwa yakinifu na kuzingatia uhalisia.
Aliongeza kuwa chini ya mfumo huo mpya suala la thamani ya fedha (value for money)katika manunuzi ya bidhaa na huduma ni ajenda muhimu lengo likiwa ni kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alieleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Wizara ya Katiba na Sheria na kupongeza hatua ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kupeleka huduma za Ofisi yake katika ngazi ya wilaya.
Alieleza matumaini yake kuwa kutokana na Wizara hiyo kupokea karibu fedha zote ilizotengewa katika bajeti ya mwaka uliopita pamoja na kuweza kuajiri watumishi zaidi wananchi wataendelea kupata huduma zinazotolewa na Wizara pamoja na taasisi zake kwa wakati na zenye ubora zaidi.

Awali akitoa maelezo ya Wizara yake, Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis alieleza kuwa katika mwaka wa fedha uliopita Wizara yake iliweza kukamilisha rasimu ya awali ya Mkakati wa Mageuzi ya Sheria, ilikamilisha pia Utafiti wa Matumizi ya Sheria Zanzibar pamoja na kazi ya kuandaa Mfumo wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Wizara.
Aliongeza kuwa Wizara inaendelea na kazi ya kutayarisha Sera ya Msaada wa Kisheria pamoja na kazi ya kutathmini mahitaji ya mafunzo ya Wizara.
Kuhusu marekebisho ya sheria, Waziri alibainisha kuwa kazi ya utafiti wa sheria za Zanzibar inaendelela na kwamba hadi sasa ripoti za awali za marekebisho ya sheria 4 zimeandaliwa kwa kuziwasilisha kwa Makamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
Alizitaja sheria hizo kuwa ni Sheria ya Mwenendo wa Jinai No. 7/2004, Notaric Public Decree sura ya 29/1949, The Limitation Decree sura 12/1917 na The Legal Practitioners Decree sura 28/1941.  
Aliishukuru Serikali kwa kuipa fursa ya kuajiri watumishi 77 katika taasisi zake kitendo ambacho alisema kitaongeza ufanisi katika utendaji katika taasisi hizo.
Kwa upande wa kuimarisha utawala wa sheria na kukuza upatikanaji wa haki kwa jamii alisema jumla ya kesi 6,633 zikiwemo za jinai, madai, ndoa, talaka, mirathi, za watoto, pamoja na kesi za Mahkama za Rufaa zilifunguliwa ambapo kesi 3,298 zilitolewa maamuzi ikiwa ni asilimia 50.
Akizungumzia bajeti, Waziri Abubakar alisema kuwa katika mwaka wa fedha uliopita Wizara yake ilipokea kutoka serikalini jumla ya Tshs. bilioni 7.4 sawa na asilimia 98.6 ya Tshs. 7.5 zilizotengwa kwa wizara hiyo kwa ajili ya matumizi ya kawaida.   


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.