Habari za Punde

Serikali yazialika timu za Vietnam na China kushiriki Mapinduzi Cup


Na Mwajuma Juma

SERIKALI  ya Mapinduzi ya Zanzibar imezialika Timu za Klabu Bingwa za Mataifa ya Vietnam na Jamuhuri ya Watu wa China kushiriki katika mashindano ya Kimataifa ya Mapinduzi Cup yatakayopamba  vuguvugu la maadhimisho ya sherehe za kutimia Nusu Karne { Miaka 50 } ya Mapinduzi ya Zanzibar  yanayofikia kilele chake Tarehe 12 Mwezi Januari mwaka 2014.

Mualiko huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Sherehe za Kitaifa Balozi Seif Ali Iddi alipokuwa akizungumza na Mabalozi wa Nchi za  vietnam na Jamuhuri ya Watu wa China kwa nyakati tofauti Nyumbani kwake Mtaa wa Haile Selassie Mjini Dar es salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imesema kuwa Serikali imefikia uamuzi wa kutoa upendeleo wa kuzialika Timu Bingwa za Nchi hizo kutokana na msimamo wa Nchi hizo kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara tuu baada ya Wananchi wake kufanya Mapinduzi ya kumuondoa Mkoloni mwaka 1964.

Balozi Seif kupitia taarifa hiyo alisema Mashindano hayo ya Kimataifa yatafanyika katika makundi matatu ambao mawili yatakuwa katika Kisiwa cha Unguja na Kundi moja litakuwepo Kisiwani Pemba wakati fainali yake itafanyika katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Mabalozi hao wa China na Vietnam kwamba Serikali imejiandaa kuzihudumia Timu hizo kwa kutoa huduma za malazi, chakula na usafiri wa ndani wakati zitakapokuwepo hapa Nchini.

“ Tunachokiomba kwa Nchi Zenu kuwapatia Tiketi za usafiri wa kuja na kurudi wachezaji wa Timu zenu na masuala mengine yote yatakuwa juu ya dhamana ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar muda wote watakaokuwepo Nchini “. Alifafanua Balozi Seif.
Alisisitiza kwamba mashindano hayo mbali ya kutoa Burdani na upinzani mkali wa kimichezo lakini pia yanatarajiwa kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya Zanzibar na Nchi hizo mbili kimichezo.

“ Tumeshaziandikia barua za mualiko Serikali za Nchi Zenu za China na Vietnam kuzitaka Klabu Bingwa za Timu za Nchi hizo kushiriki katika mashindano yetu.

Kwa upande wao Mabalozi hao  Nguyen Thanh Nam wa Vietnam na  Lu youqing wa China wameahidi kulishughulikia ipasavyo suala hilo la mualiko ili kuona kwamba lengo lililokusudiwa la kutoa mualiko huo linafanikiwa vyema.

“ Ukweli tunafurahia uwepo wa timu za Nchi zetu katika mashindano hayo ya Kimataifa ya Kombe la Mapinduzi ambayo yataongeza kasi ya uhusiano wa wananchi wetu hasa katika nyaja za michezo “. Walisema Mabalozi hao Nguyen Thanh wa Vietnam na Lu Youqing wa China.

Michuano ya Kombe la Mapinduzi yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Disemba ambayo yanatarajiwa kushirikisha timu 12.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.