Habari za Punde

CCM kutoa kipaumbele kwa vijana wasomi wa vyuo vikuu

 Wajumbe wa Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar walioshiriki kongamano la Kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar  ya mwaka 1964 liliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.
Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar  Nd. Machano Haji Machano akijiandaa kumkaribisha Mjumbe wa Kamati Kuu ya ccm Balozi Seif kufungua Kongamano la wana vyuo hao kutimia miaka 50 ya Mapinduzi.Kulia yake ni Mgeni rasmi wa ufunguzi wa Kongamano hilo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Baalozi Seif, Katibu wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mh. Hamad Masauni Yussuf na kushoto ya Balozi  Seif ni Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mstahiki Khatib Abdullrahman.

 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Vijana wa Mkoa wa Vyuo vikuu CCM Zanzibar kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964

Mjumbe  wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha  Mh. Steven wasira ambaye ndie mgeni rasmi katika ufungaji wa Kongamano la Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar akisalimiana na wanakongamano hao kwenye ukumbi wa Hoteli ya Garand Palace Malindi Mjini Zanzibar. Wajumbe wa Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar walioshiriki kongamano la Kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar  ya mwaka 1964 liliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kongamano la kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar la Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar.

Kulia yake ni Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar Nd. Machano Haji Machano na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Abdulla Mwinyi, Kushoto ya Balozi ni Mjumbe mwenzake wa Kamati Kuu ya CCM Mh. Steven Wasira na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar Khatib Abdullrahman.

Picha na Hassan Issa wa  - OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Chama cha Mapinduzi kinakusudia kutoa kipaumbele zaidi kwa vijana wasomi wa vyuo vikuu walio wanachama wa chama hicho katika kuwapatia fursa zaidi za kimasomo katika elimu ya juu kwa lengo wa kuwajengea uwezo wa kukitumia vyema chama chao katika misingi ya Kitaalamu.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akilifungua Kongamano la Siku moja na Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Grand Palace Malindi Mjini Zanzibar.

 Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Vijana ndio rasilmali kuu ya Taifa lolote pale ulimwenguni. Hivyo chama cha Mapinduzi kina kila sababu ya kuwajengea mazingira mazuri vijana katika kulitumikia vyema Taifa lao.

Aliwataka Vijana hao wa Mkoa wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar kuhakikisha kwamba wanalazimika kuzungumzia hatma yao hasa katika kutafuta elimu  yenye fani inayokubalika wakati wote katika kujijengea ajira na Serikaliitakuwa tayari kupokea mapendekezo au maazimio yao.


Balozi Seif alifahamisha kwamba historia ya Zanzibar inaelewa wazi kwamb a Chama kilichopigania uhuru wa Visiwa hivi cha ASP Kilikuwa na utaratibu wa kuendesha harambee ili kusomesha vijana wake kutokana na madhila ya watawala kuwakosesha taaluma watoto wa wakulima wa Visiwa hivi.

Hata hivyo alisema inasikitisha kuona baadhi ya Viongozi ndani ya Taifa hivi hawataki kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kufikia kutumia madaraka yao kuvuruga vielelezeo vya Mapinduzi kwa kuvichoma moto.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif aliwapongeza Vijana hao wa Mkoa wa Vyuo Viku CCM Zanzibar kwa juhudi zao za kusherehekea Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 50 licha ya kwamba asilimia kubwa kati yao hawayatambui kwa vile walikuwa bado 
hawajazaliwa.

“ Nimefarajika sana na Mada zenu mlizozichagua kwenye Kongamano lenu hili ambazo ni dhana ya Mapinduzi na Vijana wa leo, harakati za Vijana na maendeleo ya sayansi na Teknolojia, Wajibu wa vijana wasomi kwa Taifa pamoja na Vijana na Maendeleo “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Vijana hao wa vyuo vikuu bado wana fursa kubwa ya kutumia elimu katika kuyalinda Mapinduzi  pamoja na kutumia nguvu kazi ya kilijenga Taifa.

Katika kuunga mkono juhudi za vijana hao  wasomi wa vyuo vikuu vya Zanzibar Balozi Seif alisema Chama kitaandaa utaratibu wa kukutana na uongozi wa Mkoa huo wa vyuo Vikuu CCM Zanzibar katika jitihada za kutafuta njia za kukabiliana na changa moto zinazowakabili.

Katika risala yao wanachama hao wa Mkoa wa vyuo Vikuu CCM Zanzibar   iliyowasilisha na Ndugu Zeyana alisema vugu vugu la kuanzishwa mkoa huo wa vyuo limekuja ili kuwaunganisha wanafunzi hao wa vyuo pamoja na kuwajengea uwezo wasomi  kukitumikia chama na Serikali katika misingi ya uzalendo.

Ndugu Zeyana alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa Mkoa huo mwaka 200 ni pamoja na kuongeza idadi ya wasomi katika vyuo mbali mbali nchini licha ya kuwepo kwa baadhi ya change moto.

“Tumekuwa tukipata changamoto mbali mbali tokea tulipoanzisha Mkoa wetu hasa suala la ukosefu wa mfuko wa kuendeshea Mkoa, uhaba wa vitendea kazi pamoja na ukosefu wa mikopo kwa wanachama wa Mkoa wetu “. Alifafanua Ndugu Zeyana.

Alisisitiza kwamba Vijana hao hivi sasa wameamua kupambana kwa hoja na sio matusi na kuuomba Uongozi wa Chama Afisi Kuu kuwapatia msaada wa Laptop ili wawe na uwezo wa kukamilisha ndoto yao hiyo ya kukabiliana na matukio ya mitandao.

Mapema Kaimu Mwenyekiti wa Mkoa wa Vyuo Vikuu vya CCM Zanzibar Ndugu Machano Haji Machano ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi iliyochukuwa katika kusaidia vijana wa vyuo vikuu waliopata ajali ya gari Mkoani Dodoma hivi karibuni.

Ndugu Machano alisema  wanachama wa Mkoa huo wa Vyuo Vikuu CCM Zanzibar wamefarajika na hatua hiyo ambayo inapaswa kupongezwa na kuungwa mkono na wananchi wote.

Kaimu Mwenyekiti huyo wa Mkoa wa Vyuo vikuu CCM Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi kwamba watakuwa tayari kutumia Hekima, Elimu na ujuzi wao katika kutetea maslahi ya Chama chao na Serikali kwa ujumla.

Alishauri kwamba katika kuwajengea uwezo wa Kitaaluma Vijana hao wa vyuo vikuu ni busara kwa Chama cha Mapinduzi wakati huu kuanzisha utaratibu wa kuwadhamini wanafunzi wote wasomi wa chama hicho katika kuwapatia elimu ya juuzaidi kwenye vyuo tofauti ndani na nje ya Nchi.
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.