Habari za Punde

CCM waaswa kuimarisha Muungano

Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa iliyopo hivi sasa kwa wana CCM na wapenda amani Nchini ni kuendelea kuimarisha muungano wa Tanzania ulioleta umoja na mshikamano na maelewano ya pande zote mbili.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2014 hapo katika uwanja wa kwamabata Mgogoni Wilaya ya Magharibi alisema nje ya Muungano hakutakuwa na Zanzibar kama wasia wa Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere alivyokuwa akisisitiza wakati wa uhai wake.
 
Balozi Seif Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wana ccm hao kwamba Muungano wa Tanzania utaendelea kudumu .  “ Wana chama wa Chama cha Mapinduzi msiwe na wasi wasi.
 
Muungano utaendelea kudumu na Aprili 26 mwaka 2014 unatimiza miaka 50 tokea kuasisiwa kwake “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Alisema Taifa limepata maendeleo makubwa tokea Zanzibar na Tanganyika zilipopata uhuru wake chini ya vyama vya TANU na ASP na baadaye Chama cha Mapinduzi yaliyoelekezwa kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.
 
Alieleza kwamba upo ushahidi ulio wazi wa maendeleo hayo yaliyofanywa na Serikali zote mbili Nchini kwa kuwapelekea maendeleo wananachi wote ikiwa ni pamoja na  huduma za maji, umeme, bara bara, mawasiliano na afya.

Akizungumzia suala la mfumo wa muundo wa serikali Tatu ulioainishwa ndani ya rasimu ya katiba ya Pili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif alisema Tume ya katiba imependekeza mfumo huo baada ya kuzingatia  malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na pande zote mbili za Muungano.
 
Alifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi bado kinaendelea kuwamini kwamba mfumo wa Serikali mbili Nchini Tanzania umesaidia kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wake.
 
Hata hivyo Balozi Seif alisema waamuzi wa mwisho wa mfumo huo uko mikononi mwa wananchi wenyewe baada ya kujadiliwa na wabunge wa bunge la katiba wanaotarajiwa kukamilisha kazi yao mwezi Febuari mwakani.
 
Alisema nguvu za chama chama cha Mapinduzi kupitia wanachama wake hivi sasa zielekezwe katika kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
 
“ Mshikamano ni jambo la lazima kwa wana CCM ili kujizatiti katika kupigania kupatikana kwa ushindi huo “. Alifafanua Balozi Seif.
 
Kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar kutimia nusu karne Balozi Seif aliwaomba Wananchi wote kuendelea kushiriki vyema kwenye shsrehe hizo.
 
Akiwa Kwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Taifa Zanzibar Balozi Seif aliwapongeza wananchi kwa ushiriki wao kwenye harakati mbali mbali za sherehe hizo mjini na Vijijini Unguja na Pemba.
 
Akitoa salamu zake katika Mkutano huo Mlezi wa Mkoa wa Mjini Kichama ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mh. Shamsi Vuai Nahodha alitahadharisha wana CCM na Wananchi kupiga vita vikundi vya kihuni vinavyoashiria kurudisha maendeleo ya Taifa na Jamii kwa ujumla.
 
Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM  Taifa Mh. Sadifa Juma Khamis  aliwaasa  Vijana kutokubali kutumiwa  na wanasiasa wachache  kwa maslahi yao binafsi.
 
Mh. Sadifa alisema  tabia ya baadhi ya wanasiasa hao kuendeleza ubaguzi ikiachiwa kupandikizwa ndani ya makundi ya Vijana hao inaweza kuleta athari kubwa ndani ya Jamii hapo baadaye.
 
Akimkaribisha mgeri rasmi kwenye Mkutano huo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Mohd Yussfu aliwaambia wana ccm hao kwamba Zanzibar kamwe haitarejea katyika utawala wa kidhalimu na kibaguzi kama ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
 
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Magharibi aliwataka wana ccm na Wananchi wote kuendelea kutembea kifua mbele bila ya kujali kauli za baadhi ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka kurejesha utawala wa kitwana Nchini.
 
 

5 comments:

 1. Kwanini kusiwe na Zanzibar nje ya Mungano. Wakati ambapo Zanzibar ilikuwepo kabla ya Mungano????!!

  ReplyDelete
 2. Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa chini ya Utawala wa Kikoloni. Lakini tukirudi nyuma kidogo utagundua Kama Zanzibar ni pamoja na Tanganyika na mwambao wote wa Afrika Mashariki. Kama tulikuwa wamoja wakati huo kwanini tusiwe wamoja Leo.

  ReplyDelete
 3. Si kweli ndugu iddi

  1.Maji gani mliyowafikishia wananchi, hapa mjini tu mmeshindwa itakuwa huko vijijini? kila siku tunaamka usiku wa manane kuchota maji au mchana kununua kwa madum , kweli unaweza kujisifu ? kitu kimoja tu cha msingi ktk maisha ya binadamu kimekushindeni ,

  2.Hizo barabara zote za msaada hakuna pesa hata moja ya serikali.

  3.Umeme tumeletewa na Tanganyika ili wazidi kututawala na kutufanya tuwe tegemezi wao siku wakizima umeme wao basi tuhakikishe uchumi wote umeangamia na kuongezea umeme wao ni ghali kuliko umeme tuliokuwa nao zamani wa generator

  4. Afya aaaha hahaahaa haa haaaa , eee hehhee heeeee oohohooo hoooo ,,ihiii ihiiiiiii hiiii mbavu zinauma kwa kunichekesha ndugu Iddi , kama kweli unajivunia afya mliotuletea mbona nyinyi mnaenda nje kufanyiwa 'check up' Viongozi hutumia mamilioni ya fedha za raia wakati hata hawajaumwa wanaendea nje , jee wakiumwa si watahamia huko Marekani , Ujerumani na Uingereza afrika kusini , uchache uchache mtaenda india.
  5. Mawasiliano yamekuja kutokana na wakati sio kwamba mlikusudia yaje , na mngekuwa na uwezo basi mngezuia hata hayo tusiyapate ,
  1+2+3+4+5= muungano , kwa hio nini kifanywe ili tuondokane na matatizo , jawabu Shekhe Iddi ni kuwa muungano huu uliopo usiwepo kila mtu achukuwe nchi yake tufanye shirikisho ktk mambo tutayokubaliana. Sekta hizi kabisa zisiwemo kwenye muungano ; mambo ya ndani, fedha na benki , ushuru , ulinzi, polisi, jeshi , mambo ya nje , mawasiliano , uhamiaji , bahari na uvuvi na mafuta. Kwenye shirikisho tunaweza kushirikiana ktk kilimo , viwanda , afya , utalii na elimu nk

  ReplyDelete
 4. UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UZAIFU HAWA WANAO UPINGA HUU MUUNGANO WANALAO JAMBO, MUNGU YUPO, KAMA WANAMA MALENGO MABAYA DUAZAO ZA MNAZI MMJA NA KIDONGO CHEKUNDU ZITAWARUDIWENYEWE

  ReplyDelete
 5. ndugu chai kumbuka kila chenye mwanzo huwa na mwisho , katika kitu bora alichokiumba Mungu ni binadamu lakini hata yeye ana mwisho. Muungano utakwisha kuna siku subiri tu , nani alifkiria umoja wa urusi utasambaratika leo uko wapi? mbona sudani kusini wamejitenga kama umoja ni nguvu?

  ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.