Habari za Punde

Dk Shein amtaka Msajili wa vyama vya siasa kuhakikisha vyama vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa katiba na sheria

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                    04 Disemba, 2013


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesisitiza nafasi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ni kuvisaidia vyama nchini kufanya shughuli zake kwa mujibu wa Katiba ya nchi na Sheria iliyoanzisha vyama hivyo.
 

Akizungumza na Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi Dk. Shein amesema ingawa vyama vya siasa vimeanzishwa kwa sheria maalum na kufanya shughuli zake kwa mujibu wa Katiba mara nyingine viongozi wa vyama hivyo husahau sheria hiyo na kufanya vinginevyo.
 

“Vyama vya siasa vimetajwa katika Katiba na vimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria,ni vyema waanzilishi na waendeshaji wa vyama hivyo wakazingatia hayo katika kufanya shughuli zao” alisema Dk. Shein.
 

Kwa hiyo alimueleza msajili huyo kuwa ni wajibu wa Ofisi yake kuhakikisha kuwa viongozi wa vyama wanafuata Katiba na Sheria kwa kuwakumbusha mara kwa mara viongozi hao wajibu wao wa kuendesha shughuli za vyama vya siasa kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizopo.
 

“Sisi viongozi wa vyama vya siasa wakati mwingine husahau sheria hii na kufanya shughuli zetu bila ya kuizingatia hivyo ni wajibu wa Ofisi ya Msajili kutukumbusha kutii Sheria zilizopo na kufanya shughuli zetu bila ya kuzikiuka” Dk. Shein alimueleza Msajili.



Dk. Shein alibainisha kuwa ushabiki na ushindani wa kisiasa wakati mwingine huchukua nafasi zaidi na kuisaihau sheria hiyo na katika hali kama hiyo Ofisi ya Msajili inapaswa kuchukua nafasi yake kwa kuvikumbusha vyama vya siasa na viongozi wao.
 

“Maneno ya wanasiasa wakati mwingine yanakuwa makali sana na wafuasi wa vyama huyachukua hivyo hivyo ama kuyazidisha hivyo wanaweza kuhatarisha utulivu wa nchi” Dk. Shein alisema.
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama kuimarisha Ofisi yake Zanzibar ili iweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa vyama vya siasa nchini.
 

“Natarajia kuwa Ofisi ya Msajili Zanzibar ni Ofisi Kuu ya Ofisi ya Msajili hivyo ni muhimu iimarishwe kwa kuongezewa uwezo ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ipasavyo” alieleza Dk. Shein.
 

Aliongeza kuwa kuimarishwa kwa Ofisi hiyo humu nchini ni muhimu ili vyama vione kuwa vina Ofisi inayowahudumia wakati wote na kwa huduma wanazozihitaji kwa wakati na kwa ufanisi.
 

Dk. Shein alimhakikishia Msajili wa Vyama kuwa Serikali itaendelea kuipa ushirikiano Ofisi hiyo ili iweze kutekeleza wajibu wake nchini.
 

Kwa upande wake Msajili wa Vyama Jaji Francis Mutungi alimhakikishia Rais kuwa Ofisi yake itaimarisha Ofisi ya Msajili Zanzibar ili vyama vya Siasa viendelee kupata huduma nzuri na kwa ufanisi kulingana na hadhi yake.
 

Halikadhalika alieleza kuwa Ofisi ya Msajili ikiwa ndio mlezi wa vyama vya siasa nchini imekuwa iikishiriana bega kwa bega na vyama vya siasa kuhakikisha vyama hivyo vinatimiza wajibu kwa wananchi.
 

Alisema Ofisi ya Msajili kwa ujumla inakabiliwa na changamoto moja kubwa wakati wananchi wanaamini baadhi ya masuala yanapaswa kushughulikiwa na Msajili, kwa bahati mbaya Ofisi yake haina mamlaka ya kisheria kushughulikia masuala hayo.
 

Kwa hivyo alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa  hatua kwa hatua na kushirikiana na wadau wengine Ofisi yake inaangalia namna bora ya kushughulikia changamoto hizo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.