Habari za Punde

CCM Zanzibar iache kujigeuza popo


Na Salim Said Salim
KAULI za baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanaotoka CCM zinanishangaza kwa vile huwa zinabadilika kama lilivyo umbile la popo, leo ndege (anaruka) na kesho mnyama (anazaa).
Kwa lugha ya Waswahili, kiumbe wa aina hii huitwa kigeugeu. Mwenendo kama huu kwa watu wa Mombasa unajulikana kama “huku hayuko, huku hayuko unkula huu.”
Kiumbe mwingine ambaye hubadilika ni kinyonga, mara huwa na rangi ya manjano, mara kijani na wakati mwingine huwa na rangi nyekundu au hudhurungi. Ni mdudu ambaye yupo katika mahangaiko tu, lakini umbile lake linabaki lilelile.
Lakini na binadamu naye huwa pia na tabia kama hizo za popo na kinyonga. Hivi karibuni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, waliotoka CCM, wamekuwa wakisema katika mfumo wa serikali mbili wa Muungano uliopo hivi sasa, Zanzibar ina mamlaka kamili. Shabbash!
Kutokana na hali hii, ndiyo maana wanang’ang’ania, ijapokuwa Watanzania wengi, Bara na Visiwani, wameshasema serikali mbili “bai bai” na karibu kwa salama, amani na utulivu serikali tatu.
Hili limebainishwa wazi na mapendekezo ya Tume ya Katiba katika mapendekezo yake yaliyotokana na maoni ya wananchi kutoka kila pembe ya Jamhuri ya Muungano. Tume imetoa takwimu juu ya hali hii kuonyesha kuwa sio dhana, bali ni uamuzi wa wengi.
Tuchukulie hawa viongozi wa CCM wanaamini hicho wanachokisema kwamba Zanzibar inayo mamlaka kamili. Sasa kama ndiyo hivyo, mbona tunawasikia wakitaka mamlaka juu ya masuala mbalimbali na kueleza kwamba kutokuwa na madaraka hayo ni miongoni mwa kero za Muungano?
Vile vile hivi vikao vinavyotumia mamilioni ya shilingi vya mawaziri wa pande mbili za Muungano vya nini kama mambo ni shwari?
Sasa tuamini lipi, hili la popo kama mnyama kwamba Zanzibar inayo mamlaka kamili au hili la popo kama ndege la Zanzibar kubanwa katika baadhi ya mambo ndani ya Muungano, kama suala la mafuta?
Kauli hizi tunazisikia katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembe Samaki, Unguja, lililokuwa wazi kufuatia kufukuzwa uwanachama, Mansour Yusuf Himidi, mtoto wa mmoja wa viongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964, marehemu Yusuf Himidi.
Kosa (madhambi kwa mtazamo wa CCM) la Mansour ni kutoa maoni yake hadharani ya kusema mfumo wa serikali tatu ndio wenye maslahi kwa Zanzibar na ndio unaoweza kuhakikisha kuimarika kwa Muungano.
Kinachoshangaza sio Mansour peke yake katika viongozi wa juu wa CCM waliosema wazi kwamba mfumo wa serikali tatu ndio unaofaa.
Lakini hatua ya kufukuzwa chama imechukuliwa kwa Mansour tu kwa sababu amekuwa na msimamo mmoja na habadiliki kama popo au kinyonga au kishada kilichokwenda arijojo.
Lakini inawezekana huo ndio utaratibu ambao wenyewe CCM wamejiwekea wa hili likifanywa na huyu ni kosa na likifanywa na yule sio kosa.
Hata ndani ya Baraza la Wawakilishi imesikika kauli hii kutoka kwa wawakilishi wa CCM na CUF wa kutaka Zanzibar iwe na mamlaka kamili ya mafuta. Hii ina maana walikuwa wanaamini Zanzibar haina mamlaka kamili ndani ya Muungano.
Sasa hizi kauli zinazosikika katika jimbo la Kiembe Samaki zitiwe katika kikapu kipi…. Kile cha kero za Muungano au kile kilichojaa mamlaka kamili kwa Zanzibar? Jamani mbona tunaubabaisha umma? …Huku twataka, huku twataka mwisho tutankula huu!
Ni lazima Wazanzibari waamue, sio leo wanasema hili kesho lile na jipya kabisa wiki ijayo. Lakini ukichunguza utaona chote hiki ni kiwewe kama cha mfa maji kilichotokana na mapendekezo ya rasimu ya katiba ambayo baadhi ya viongozi wa CCM wameyapolea kwa huzuni na kama vile ni msiba.
Hii sio tu imesababisha kulishana viapo, bali pia kuanza kuandamwa watu kadhaa, mbali ya Jaji Warioba. Hivi sasa tayari jungu lipo jikoni la kumsakama Mwakilishi wa Uzini, Mohamed Raza kwa vile naye bila ya kutafuna maneno anapigia debe serikali tatu.
Hatujui hatima ya Raza itakuwaje, lakini naye kama Mansour, amekuwa akisisitiza kwamba Katiba ya Zanzibar na ya Muungano inampa uhuru wa kutoa maoni yake na anaona hiyo ni haki yake.
Heko Raza na natumai viongozi wengine, iwe ndani ya CCM, CUF, CHADEMA, NCR-Mageuzi au chama kingine hawatakubali kuburuzwa na chama chao pale wanapoamua kutumia haki yao ya katiba ya nchi.
Katiba ya nchi lazima ije kwanza na baadaye ndiyo za vyama vya siasa, klabu za soka, vikundi vya taarab au lelema.
Nchi, kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, lazima ije kwanza na baadaye ndiyo maslahi mengine. Uraia wetu ni wa Tanzania na sio wa chama cha siasa.
Unaposikiliza hotuba za viongozi wa CCM katika kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kiembe Samaki utakaofanyika Jumapili ijayo (Februari 2) unaona wanaopanda kwenye viriri wanazungumzia rasimu ya katiba na sio kumpigia debe mgombea wao.
Suala la serikali tatu ni uamuzi wa umma na kilichobakia ni kuangalia vipi hili linaweza kutekelezwa kwa maelewano. Kuzungumzia serikali mbili ni kuurudisha nyuma mchakato wa katiba.
Au ndio Kamati Kuu inataka kuliambia taifa kwamba imeamua wananchi hawana haki ya uamuzi na wao ndio manahodha wa nchi hii na wengine wabaki kuwa abiria waliofungwa minyororo na wapelekwe safari wasiyoitaka?
Nimesema mara nyingi sio vyema, sio vizuri na sio uungwana kujidai ni mwana wa demokrasia, lakini unakataa maamuzi ya wengi.
Kama ndani ya CCM ni sahihi kama tulivyoona mara nyingi katika kuchagua wagombea wao wa uchaguzi kuwa apataye kura chache ndie mshindi, hilo haliwezi kukubalika kwa wanademokrasia wengine.
Kwa maana hiyo ni vizuri CCM kubakia na demokrasia yao ya wachache kuwa na haki ndani ya chama chao, lakini wasiambukize wasiotaka mwenendo huo.
Hivi sasa zipo dalili za baadhi ya vingozi wa CCM Zanzibar kutaka kukwamisha mchakato wa katiba mpya. Ninachelea watakuja kula na chuya.
Ni vizuri kwa vongozi wa CCM, licha ya kulishana kiapo wakafikiria tena msimamo wao kwa maslahi ya nchi. Vitisho na kulazimisha mambo hakusaidii. Wimbi la demokrasia ya kweli linavuma kwa nguvu na halizuiliki.
Haya tumeyaona katika nchi nyingi na ni vizuri tukajifunza ili mchakato wa katiba mpya usiwe chanzo cha kuleta mfarakano ambao hautakuwa na faida kwa CCM wala wapinzani.
Kila tunapoamua kufanya jambo lazima tuheshimu mawazo ya wengi. Kama hatukufaya hivyo, badala ya kusonga mbele tutarudi nyuma na tutakapoelewa kuwa tumefanya makosa tutakuwa tumeshapotea njia.
Utashi wa kisiasa usiwe sababu ya kuizuia demokrasia kustawi na watu kusonga mbele. Kama CCM wameamua kubaki nyuma sio vibaya kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba, lakini haina haki kwa sheria za nchi na za kimataifa kuwazuia Watanzania wengine kusonga mbele na hatimaye kuwa na utawala bora wa kweli na sio wa popo au kinyonga.
Chanzo - Tanzania Daima

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.