Habari za Punde

Kwa kujitoa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Yanga yaomba radhi

 Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Yanga ya Jijini Dar es salaam Clement Andrew  Sanga  akiomba radhi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Kamati ya Mashindano ya Mapinduzi Cup kwa kutoshiriki kwa timu yake katika mashindano hayo kulikosababishwa na matatizo yaliyoshindwa kuepukika.


Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Yanga ya Jijini Dar es salaam Clement Andrew  Sanga  akikabidhi mchango wa Shilingi Milioni Kumi uliotolewa na Klabu ya Yanga kusaidia mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Uongozi wa Klabu ya Yanga ya Jijini Dar es salaam imeiomba Radhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kutoshiriki kwenye mashindano hayo licha ya kuthibitisha ushiriki wake katika hatua za awali.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo Clement  Andrew  Sanga alitoa kauli hiyo wakati akiomba radhi mbele la Kamati ya Mashindano hayo wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Clement  Andrew alisema Klabu ya Yanga tayari ilikuwa imeshajindaa vyema na mashindo hayo ya Kombe la Mapinduzi lakini katika dakika za mwisho ilikumbwa na  matatizo yaliyopelekea uongozi wa Kamatgi ya Ufundi ya Klabu hiyo ujiuzulu.     

Makamu Mwenyekiti huyo wa Dar Young African alifahamisha kwamba kutokana na mtihani huo uliyoikumba Klab yake  haikuwa rahisi kwa wakati huo kuendelea kushiriki kwenye mashindano hayo.



Hata hivyo Clement  Andrew aliithibitishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi  kwamba Klabu yake iko tayari wakati wowote kushiriki mashindao yoyoye itakayoalikwa ndani ya Visiwa vya Zanzibar.

Alisema Klabu ya Yanga ina Historia ndefu na Zanzibar na katika kuthibitisha hilo Uongozi huo wa Timu yake umeamua kutoa mchango wa shingi Milioni Kumi { 10,000,000/- }  kusaidia Mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi.

Alifahamisha kwamba hatua hiyo imelenga kuonyesha mshikamano uliopo kati ya pande hizo mbili.

Akipokea mchango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliinasihi Klabu ya hiyo ya Yanga ya Dar es salaam kuwepuka  migogoro isiyo ya lazima ambayo ikiachiwa kuendelea inachangia kuviza maendeleo ya michezo Nchini.

Balozi Seif alisema ni vyema kwa Uongozi pamoja na wanachama wa klabu hiyo kuendelea kujipangia utaratibu utakayotoa nafasi na fursa ya kujadiliwa matatizo yanayojichomoza ili kupanda ufumbuzi wa kistaarabu.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Uongozi wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi imefarajika na mchango wa klabu hiyo maarufu ya yanga ambao utasaidia kuziba mapungufu yaliyopo katika uendeshaji wa mashindano hayo.






No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.