Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete, amefanya uhamisho na uteuzi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri katika
baadhi ya wizara kwenye mabadiliko ya baraza lake la Mawaziri.
Akitangaza mabadiliko hayo mbele ya waandishi wa habari jana, Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema mabadiliko hayo yamefanywa baada ya
Mawaziri wanne kujiuzulu kutokana na kashfa ya operesheni tokomeza ujangili na
kufariki kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.
Mabadiliko hayo yamefanywa katika Ofisi ya Makamu wa Rais, na katika
baadhi ya wizara, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiendelea kushikilia nafasi
yake.
Katika mabadiliko hayo, Rais
Kikwete amemteua Saada Mkuya Salum, kuwa Waziri wa Fedha, kuziba pengo la Dk.
Mgimwa aliyefariki nchini Afrika Kusini.
Mkuya anakuwa Waziri wa pili kutoka Zanzibar kuiongoza wizara hiyo
akitanguliwa na Zakia Hamdan Meghji.
Pia amemteua Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Lameck Nchemba na
Adam Kigoma Malima kuwa Manibu Waziri wa wizara hiyo.
Katika Wizara ya Katiba, alieteuliwa kuwa Waziri ni Dk. Asha Rose
Migiro kuchukua nafasi ya Mathias Meinrad Chikawe alieteuliwa kuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani, kuchukua nafasi iliyoachwa na Dk. Emmanuel Nchimbi aliejiuzulu.
Katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Waziri anaendelea kuwa
Samia Suluhu Hassan ambapo wasaidizi wake sasa ni Eng. Dk. Binilith Satano
Mahenge (Mazingira) na Ummy Ali Mwalimu.
Wizara ya Viwanda na Biashara Waziri anaendelea kubakia kuwa Abdalla
Kigoda na naibu wake sasa anakuwa Janet Zebedayo Mmbene, aliyekuwa Naibu Waziri
wizara ya Fedha.
Hussein Ali Mwinyi, amerejea tena katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, kuchukua nafasi ya Shamsi Vuai Nahodha, aliejiuzulu.
Katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliyekuwa Naibu Waziri, Dk.
Seif Seleman Rashid amepandishwa kuwa waziri kamili kujaza nafasi ya Dk.
Hussein Mwinyi ambapo sasa msaidizi wake atakuwa, Dk. Kebwe Stephen Kebwe.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Joakim Mhagama ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi huku Dk. Pindi Hazara Chana akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kwa upande wa Wizara ya Mifugo, Waziri mpya anakuwa Dk. Titus Mlengeya
Dismas Kamani kuchukua nafasi ya David Mathayo aliyejiuzulu na msaidizi wake
anakuwa Kaika Saning’o Telele.
Katika wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Waziri
anaendelea kubakia Prof. Anna Tibaijuka na naibu wake sasa anakuwa George
Boniface Taguluvala Simbachawene wakati aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Amos Gabriel Makala anakuwa
Naibu Waziri wa Maji huku Godfrey Weston Zambi akiwa Naibu Waziri Kilimo,
Chakula na Ushirika.
Aliyekuwa mtangazaji wa TBC1, Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Selemani
Nkamia anakuwa Naibu Waziri mpya wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kuchukua nafasi ya Makala.
Katika Wizara ya Utalii na Maliasili, aliyekuwa Naibu Waziri Lazaro Samuel Nyalandu sasa anakuwa Waziri
kamili baada ya aliyekuwa Waziri, Balozi Hamis Kagasheki kujiuzulu na Naibu
wake anakuwa Mahmoud Hassan Mgimwa huku Naibu Waziri Nishati na Madini
akiteuliwa, Charles Muhangwa Kitwanga.
Hafla ya kuwaapisha Mawaziri hao itafanyika leo saa 10:00 jioni katika
viwanja vya Ikulu.
Mabadiliko hayo ni ya tatu tokea Rais Kikwete aingie madarakani 2005.
Kuhusu mchakato wa Baraza la katiba, alisema uchambuzi wa majina ya
yaliyopendekezwa kuwa wajumbe wa baraza hilo umekamilika na utangazwa wakati
wowote.
Wajumbe hao ni kutoka asasi za kiraia (NGO’s), Taasisi za kidini,
vyama vya siasa, Taasisi za Elimu,Kundi la Watu wenye ulemavu,Jumuiya za
wafugaji, Jumuiya za Wakulima, Jumuiya za Wavuvi na makundi yenye malengo
yanayofanana.
Kuhusu Mawaziri mzigo, alisema haamini kwamba mawaziri hao wamekuwa
mizigo kwa sababu zao isipokuwa kuna watendaji wanaosababisha waonekani
hawafanyi kazi na kwamba rais anaangalia utendaji kazi wa mtu.
Wacha kupotosha habari. Nahodha hajajiudhulu kafukuzwa nafasi ya uwaziri.
ReplyDeletekabisa kabisaa.......
ReplyDelete