Habari za Punde

UN kudumisha mashirikiano na Zanzibar

 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania Alberic Kacou wakiangalia chapisho la umoja huo, huko ofisini kwa Makamu wa Kwanza Migombani mjini Zanzibar.
 Maalim Seif akifanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi huko ofisini kwake.
Maalim Seif akifanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa UN nchini, Alberic Kacou, mwengine ni Afisa kutoka ofisini za UN Zanzibar, Ana Sanga.     
 (Picha na Salmin Said, OMKR).
Na Khamis Haji , OMKR
Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Alberic Kacou ameahidi umoja huo utadumisha mashirikiano na Zanzibar, ikiwemo kuendelea na mradi wa kusaidia uchaguzi kufanyika katika hali ya uhuru na haki, ili kudumisha amani na utulivu uliopo.
Ametoa ahadi hiyo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, wakati alipofika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar, kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.
Kacou amesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini inazifahamu changamoto nyingi zilizopo Zanzibar, ikiwemo suala la vitambulisho vya Ukaazi na Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuahidi atakaye shika nafasi hiyo ataendeleza juhudi hizo chini ya mradi wa uchaguzi unaoendelea kuufadhili.
Amesema malalamiko kuwa wananchi kuwa wananyimwa haki ya vitambulisho vya Ukaazi pamoja na kutopitiwa daftari la wapiga kura yanaweza kuchangia hali ya kutoweka kwa imani na hivyo kuvuruga utulivu uliopo, iwapo hayatashughulikiwa kwa haraka.
Ameahidi umoja huo utasaidia juhudi za kudumisha amani na utulivu chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na utaendelea kusaidia shughuli za maendeleo ya wananchi, ikiwemo mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi, Uharibifu wa Mazngira pamoja na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemsifu Mwakilishi Mkaazi huyo kutokana na kipaumbele kikubwa kinachotolewa na ofisi yake kwa Zanzibar, katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo na kukuza Utawala Bora.
Maalim Seif amesema mafanikio makubwa yameweza kupatikana chini ya Serikali yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa na kwamba juhudi zaidi zinahitajika kuielimisha jamii hasa katika ngazi za chini, ambako bado changamoto za uelewa mdogo juu ya mfumo huo zinajitokeza.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema madai ya baadhi ya wananchi hasa vijana waliotimiza umri kunyimwa vitambulisho vya Ukaazi yanahitaji kupatiwa ufumbuzi, kwa sababu vitambulisho hivyo ni haki ya kila Mzanzibari kwa mujibu wa sheria.
Amesema ili Zanzibar iendelee kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano viongozi Mikoa, Wilaya na Shehia hawana budi kusimamia haki kwa kila mwananchi
Makamu wa Kwanza wa Rais pia ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa kuacha tabia ya kutoa kauli zinazochochea chuki na uhasama miongoni mwa jamii.
Aidha, Maalim Seif ameupongeza Umoja wa Mataifa kutokana na kusaidia vita dhidi ya Ukimwi, na uharibifu wa mazingira Zanzibar na na kuhimiza mkazo mkubwa kuelekezwa katika kuepusha athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika mazungumzo hayo, Maalim Seif pia alimwelezea Mwakilishi Mkaazi huyo maendeleo ya zoezi la kutafuta Katiba Mpya, ambapo alisema katika hatua iliyofikiwa hivi sasa ipo haja wadau wakuu kukutana, ili kupata maelewano kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, baadaye mwezi huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.