Habari za Punde

CCM waondoshe hofu, wasikilize maoni ya wengi


Na Muona Mbali

Wakati ule wa kutafuta maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa siasa tuufate nchini Tanzania, nakumbuka kuna kigogo kimoja kwa wakati ule mzee John Malecela alisimama katika kiriri pale Kijangwani na kusema kuwa CCM ni "JABALI".

Aliendelea kusema kwa ilivyokuwa ni jabali , basi ni vugumu kulivunja au kuliteterusha.Na aliwataka wana-ccm bila ya woga kuukubali mfumo wa vyama vingi.

Hadi leo CCM yabakia hivyo sasa kwanini leo hii CCM iugopee mfumo wa wananchi wautakao katika katiba yao kwa maslahi ya vizazi vijavyo?

Ikumbukwe kuwa kuna kitabu kimoja cha Muumba wa dunia hii kimetaja kama ni mfano tu jinsi Dola kubwa na lenye nguvu lilivyoporomoka na kusambaratika (Surati Rum katika Koraani -Roman Empire).Huu ni mfano tu.

Lakini katika miaka ya karne ya 20, kama ni ushahidi tu ulimwengu umeshuhudia mataifa kadhaa kusambaratika na nguvu zao za himaya ima kupungua au kutoweka kabisa. 

Tumeshuhudia kupungua himaya ya dola la Uingereza baada ya mataifa kama 50 yaliokuwa chini ya himaya yake kuwa huru,miongoni mwao ni (Tanganyika1961 na Zanzibar 1963) na mengineyo

Pia dunia imeshuhudia kuporomoka kwa dola kubwa la wasovieti na kila nchi kuchukuwa chake. Tumeshuhudia pia dola la Yugoslavia kuporomoka na Waserbia kuchukua chao,Montenegro na chao, Kosovo na kadhalika. Pia tumeona Czechoslovakia, waCheck wakachukuwa chao na Waslovak wakabaki na chao. 

Pia majuzi tu tumeona jinsi himaya ya nchi kubwa Barani Afrika yaani Sudan kila upande ukabakia na chake. Pia kuna ushahidi mkubwa karibuni tu Uingereza, wananchi wa Scotland watajiamulia yao kwa maslahi yao badala ya kuamuliwa kutoka London.  Jee leo pana hofiwa nini katika Tanzania?

Kinachodaiwa na Rasimu ya katiba si kuuvunja Muungano lakini  katika Rasimu inapendekeza Serikali tatu, maana yake Serikali ya Tanzania itakuwepo, Muungano wa Tanzania utakuwepo. 

Kinacholiliwa na Watanganyika wawe na uhondo wa kuwa na Serikali yao kama uhondo uliopo kwa wananchi wa Zanzibar kuwa na serikali yao.

Lakini pia panatakiwa upeo zaidi wa kujiamulia mambo yao ya ndani yasiokuwa ya muungano, ukusanyaji wa mapato, haki sawa kwa pande zote mbili na kuondoa makero ya muungano yaliyopo katika taratibu za kimuungano uliopo sasa.

Kama kwa wenzetu yamefanyika ya madola kuporomoka na kusambaratika , sisi hatutaki hilo. Tunachokitaka uwe na nguvu zaidi, haki zaidi bila ya malalamiko na makero kwa pande zote mbili.

Kwa hivyo wale vigogo vya ccm wenye  woga wasiwe na woga na wenye hofu waondoshe  hofu . Tuwajengee mustakabali ya mazingira mema vizazi vijavyo!!

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.