Habari za Punde

Balozi Mdogo wa Misri Zanzibar Afika Ofisi ya Makamu wa Pili kumuaga Baada ya Kumaliza muda wake Zanzibar.

 Balozi Mdogo wa Misri aliyepo Zanzibar Bwana Walid Mohamad akimuaga rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi wa kidiplomasia hapa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Balozi Mdogo wa Misri Bwana Walid Mohamad aliyemaliza muda wake wa ubalozi hapa Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi ya kasha Balozi Mdogo wa Misri hapa Zanzibar aliyemaliza muda wake kama ishara ya utumishi mzuri aliyoitumikia vyema Zanzibar.(Picha na Hassan Issa OMPR)Na.Othman Khamis Ame
Serikali ya Misri itaongeza jitihada zake katika kuhakikisha wanafunzi wa Zanzibar wanaendelea kupata fursa za Taaluma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Nchi hiyo cha Al - Akhzal.

Balozi Mdogo wa Misri aliyepo Zanzibar Bwana Walid Muhamad alieleza hayo akijiandaa kuaga rasmi baada ya kumaliza muda wake wa miaka minne hapa Zanzibar wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Walid Mohamad alisema  Wanafunzi wa Zanzibar wamekuwa wakipata fursa za masomo kila mwaka katika Chuo cha Kimataifa cha Al – Akhal ambacho hutoa elimu ya Dini, Ufundi, Madawa pamoja na kuanzisha mitaala ya somo la ITC ambalo Mwanafunzi wa Zanzibar amekuwa akiongoza katika mafunzo hayo.

“Misri imeweka utaratibu wa kuwasajili wanafunzi watatu wa Zanzibar kila mwaka kuingia katika chuo hicho na tayari imefikia hatua ya kuongezwa fursa zaidi na kufikia watano ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Zanzibar na Misri “ Alisema Balozi Walid.

Akizungumzia sekta ya Afya Bwana Walid Mohamad alisema Misri tayari imeshatoa mashine maalum ya uchunguzi wa maradhi ya Figo itakayosaidia wagonjwa wa Zanzibar kupata huduma hiyo muhimu kwa afya zao.


Alisema taratibu zinafanywa ili kutoa nafasi kwa wataalamu wa afya wa Misri kuja kutoa mafunzo kwa madaktari wazalendo hapa Zanzibar watakaochaguliwa kutumia mashine hiyo.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Serikali ya Misri kwa juhudi zake zilizosaidia kumalizika  kwa uchaguzi Mkuu wa n nchi hiyo kwa njia ya amani na utulivu.

Balozi Seif alisema zipo dalili zinazoonyesha kutulia kwa Taifa hilo lilioko kaskazini kwa Bara la Afrika ambalo lilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa karibu miaka minne sasa.

“Bila ya amani hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana iwe ndani ya jamii au taifa lolote  kwa jumla “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza Balozi Mdogo wa Misri hapa Zanzibar Bwana Walid Mohamad kwa kazi yake nzuri iliyofanikisha kudumika kwa uhusiano mzuri uliopo kati ya Misri na Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla.

Balozi Seif alifahamisha kwamba misaada mbali mbali inayoendelea kutolewa na Misri kwa Zanzibar imechangia kustawisha maendeleo ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa Zanzibar.

Alieleza kwamba  msaada wa mashine ya uchunguzi wa maradhi ya Figo iliyotolewa na Misri kwa kiasi kikubwa itasaidia sana kundi kubwa la wananchi hasa wale wenye kipato cha chini kupata huduma hiyo muhimu.

Alisema watu wengi wamekuwa wakifuata huduma hizo katika Hospitali za Tanzania bara au zile za nje ya nchi kutegemea uwezo wa mwananchi au mgonjwa husika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alimfahamisha Balozi Mdogo huyo wa Misri hapa Zanzibar kwamba Sekta ya elimu bado itaendelea kuwa muhimili wa maendeleo kwa  Taifa lolote Duniani.

Alimuomba Balozi huyo licha ya kumaliza muda wake wa utumishi wa Kidiplomasia lakini bado ana fursa ya kuishawishi Serikali yake kuongeza misaada yake ya maendeleo hasa sekta ya elimu kwa Wananchi wa Zanzibar.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.