Habari za Punde

Waongeza makalio, nguvu za kiume kutofidiwa

Na Mwantanga Ame
NAIBU Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Steven Kabwe, amesema serikali haina mpango wa kuwalipa fidia watu walioathirika kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu sehemu za siri na kuongeza makalio.

Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa wanawake, Mhe.Rukia Kassim, aliyetaka kujua kama serikali ina mpango wa kuwafidia waathirika wanaotumia dawa za kuongeza nguvu na kuongeza  makalio maarufu Mchina.

Akijibu swali  hilo, Naibu Waziri huyo, alisema ni kweli hivi sasa zipo taarifa kwamba  baadhi ya watu wanatumia dawa hizo, lakini bado serikali haijathibitisha  lakini hata kama ni kweli haina mpango wa kuwafidia.

Alisema taarifa ambazo serikali inazo ni kwamba  watumiaji wa dawa hizo, wamekuwa wakifanya mambo hayo kwa siri, ikiwemo kwenye mahoteli.

Alisema kwa mujibu wa sheria namba 1 ya Mamlaka ya Uingizaji na  Udhibiti Dawa ya 2003, imekuwa ikizuia uingizaji wa vitu vyenye madhara kwa binadamu na kazi hiyo inafanywa mara kwa mara.

Alisema kutokana na  hali hiyo, serikali ya Tanzania bado haijabariki dawa hizo na wanaotumia wako hatarini kupata madhara.


Wakati huo huo serikali imesema imeandaa mpango wa  kutowapatia viza wanafunzi ambao wamepewa mikopo ya elimu ya juu ambao wana dhamira ya kuondoka nchini baada ya kumaliza masomo yao.

Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi, Mhe.Jenister Mhagama, alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge, Everin Edwad Sokoine, aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kupunguza tatizo la wanafunzi wa Tanzania wanaopatiwa mikopo, lakini baada ya kumaliza masomo yao huenda kufanya kazi nje ya nchi na kukimbia kulipa mikopo yao.

Alisema serikali inakusudia kuchukua hatua hizo, baada ya kuandaa mpango huo kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji .


Alisema serikali itautekeleza mpango huo kwa vile hivi sasa tayari imeshafanya usajili wa Watanzania wote, ili waweze kupatiwa vitambulisho vya taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.