Habari za Punde

ZEC kupitia upya mipaka ya majimbo

Na Khamis Salum
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inakusudia kufanya kazi  ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar, katika kipindi cha miezi sita ijao.

Hayo yalibanishwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, katika mkutano na wadau wa uchaguzi uliofanyika jana hoteli ya Grand Palace, Malindi mjini Unguja.

Alisema, kazi hiyo itaendeshwa kwa matakwa ya  katiba  na inaelekezwa  kufanyika katika kipindi  cha kila baada ya miaka minane hadi 10.
Mara ya mwisho kazi hiyo ilifanywa na ZEC mwaka 2005.

Jecha, alisema historia  ya Zanzibar  inaonesha  kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi  visiwani hapa  inafanywa  kila baada ya kipindi maalum kama inavyoelekezwa  katika sheria.

"Jambo  hili limeshatokea  tangu miaka ya 1957, 1961 na 1963 wakati visiwa vyetu vilipoanzisha utaratibu wa kuchagua viongozi wake kwa njia ya uchaguzi," alisema.

Aidha, alisema,  kazi kama hizo zimeshaendeshwa mara mbili  na ZEC mwaka 2000 na 2005.


Alisema,  hivi sasa ni miaka tisa  tangu Tume ya Uchaguzi  ya Zanzibar ilipofanya uchunguzi  wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar na sheria hiyo inaelekeza  kuwa kazi hiyo  inaweza kufanyika  katika kipindi cha miaka minane hadi miaka 10.

Alieleza, kwa maelekezo hayo, hesabu zinaonesha kuwa hivi sasa  tayari Tume imeshachelewa kuifanya kazi hiyo kwa mwaka mmoja, hivyo upo mwaka mmoja wa kuifanya kazi hiyo, vyenginevyo itakuwa imekiukwa maelekezo ya katiba.

Alisema, uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar kupanga kuifanya kazi hiyo katika kipindi hichi, unatokana na matakwa ya katiba.

Aliseka kazi hiyo  tayari imepangiwa utaratibu wake na ZEC na utekelezaji wake utaanza rasmi mwezi huu na kuendelea  mpaka mwanzoni mwa 2015.

Mwenyekiti huyo, alisema, pamoja na kazi hiyo kusimamiwa  na kutekelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kisheria, utendaji wake  mpaka kufikia maamuzi umepangwa kuwashirikisha watu wote katika jamii ya Wazanzibari.

"ZEC inategemea  kwa kiasi kikubwa  kupata maoni yenu juu ya  hali halisi ya majimbo ya uchaguzi ilivyo hivi sasa  katika wilaya  mbali mbali Unguja na Pemba,” alisema.

Alisema, ili kupata maoni hayo, ZEC imeandaa utaratibu wa kukusanya maoni  juu ya majimbo kwa utaratibu mzuri ambao utatoa fursa kwa wadau wote kuchangia.

Hata hivyo, alisema, kwa taasisi au watu ambao hawatapata  kutoa maoni ana kwa ana mbele ya Tume ya Uchaguzi juu ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi, wanaweza kutoa maoni hayo kwa maandishi.

Mkurugenzi wa ZEC,Salum Kassim Ali, alisema, kumekuwepo na changamoto mbali mbali juu ya hilo, ikiwemo kutojulikana mipaka, ukubwa wa majimbo na idadi ya watu.

Alisema, kazi hiyo itafanyika kwa uweledi mkubwa kwa kushirikiana na taasisi nyengine ikiwemo Wizara ya Tawala za Mikoa, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali na Idara ya Upimaji na Ramani.

Hivyo, aliwataka wananchi kutoa kila aina ya ushirikiano kwa ZEC katika kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Mapema wakichangia mkutano huo, baadhi ya wajumbe waliishauri ZEC kujipanga vyema kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kwa amani na utulivu kwa wananchi.


Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliitahadharisha ZEC kuwa makini na namna wananchi watakavyoshirikishwa katika zoezi hilo ili kuepuka vurugu zinazoweza kujitokeza na kuharibu dhamira njema ya zoezi hilo.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.