Habari za Punde

Na Raya Hamad OMKR.
Imeelezwa kuwa jukumu kubwa la Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ni kuratibu mapambano dhidi ya biashara , matumizi , uingizwaji na usafirishaji wa dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kutoa taaluma kwa jamii pamoja na kutoa huduma za tiba na ushauri nasaha kwa watumiaji wa dawa za kulevya .

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dr Omar Dadi Shajak wakati akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa robo ya tatu  kuanzia Januari hadi Machi kwa kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa Serikali  kwenye ukumbi wa mikutano  Ofisini Makamu wa Kwanza wa Rais migombani .

Dr  Shajak amesema katika kupunguza  uingizwaji na usafirishaji wa dawa za kulevya Tume imetowa mafunzo ya sheria ya dawa za kulevya kwa taasisi mbali mbali zilizomo kwenye mapambano hayo kama vile Polisi , waendesha mashtaka , mahakimu , watumishi wa viwanja wa ndege , bandari, TRA, ZRB.

Lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa wa wa sheria ya dawa za kulevya na kuimarisha mashirikiano kisekta katika mapambano ya Dawa za Kulevya aidha kwa upande wa taaluma kuhusu athari ya Dawa za Kulevya imetolewa kwenye Shehia na baadhi ya Skuli na sehemu za kazi .

Jumla ya skuli 16 zimepatiwa taaluma wanawake 1,280 na wanaume 826 sawa na wanafunzi 2,126 katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo  Shehia 21na Kamati za Ulinzi zilizofaidika 7 Unguja na 14 Pemba .

Kwa upande wa Idara ya Mazingira yenye jukumu la kukusanya na kuhifadhi taarifa za kimazingira , kutoa taarifa za kimazingira ili kusaidia katika kutayarisha na kutekeleza mipango na miradi ya maendeleo, kufatilia mwenendo wa hali ya kimazingira , kukabiliana na matatizoya kimazingira , kuhamasisha wadau kuchukuwa hatua za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii na kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Dr Shajak amesema Idara imeifanyia tathmini ya athari za kimazingira na kijamii na tayari ripoti za tathmini hizo zimefanyiwa mapitio na wadau kwa utaratibu wa Idara ya Mazingira na kupatiwa vyeti kufuatia mapitio hayo miradi yote imepatiwa vyeti vya kimazingira na imetakiwa kuendelea na utekelezaji kwa kufuata masharti yaliyotolewa .
Miradi iliyopatiwa vyeti ni pamoja na Hoteli ya Zas Villa Luxury na Resort Kiwengwa , Tulia Resort Pongwe, na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo Jozani hadi Charawe kupitia Ukongoroni kuelekea Bwejuu yenye urefu wa kilomita 23, Fuoni hadi hadi Kombeni kilomita 8, Kichwele hadi Pangeni kilomita 4, Mkwajuni hadi Kijini kilomita 9, na Matemwe hadi Muyuni kilomita 7.

Aidha Idara ya Mazingira imeweza kukusanya taarifa za idadi ya Jumuiya za kimazingira zilizopo Unguja na Pemba ili kuona namna zinavyoshiriki katika kusaidia kulindana kuhifadhi mazingira ambapo hadi kufikia Machi jumla ya jumuiya 60 zimeorodheshwa .

Kwa upande wao wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa Serikali ikiongozwa na Mhe Hamza Hassan wameridhishwa na mashirikiano yaliopo na utekelezaji wa bajeti kwa 2014/2015

Aidha wameiomba  Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kuendelea kusimamia vyema majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuanzisha program maalum ya kuyahami maeneo yanayoingia maji ya chumvi, kuliangalia kwa makini eneo la madagaa Bububu na uchafuzi wa mazingira .

Hata hivyo kamati hio imesema itaendelea kufatilia kwa makini suala la makaazi ya viongozi wakuu wakiserikali kwa upande wa Zanzibar na pale wanapokwenda Tanzania Bara kwa vile bado haijaridhishwa na sehemu waanazofikia mbali na kuomba kwa  wahusika  kuwatafutia makaazi ya kudumu viongozi hao wa Kitaifa .


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.