Habari za Punde

Maalim Seif Atembelea Wananchi wa Maafa ya Mvua.

Na: Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameiagiza Idara ya maafa Zanzibar kushirikiana na Wakuu wa Wilaya kufanya utafiti juu ya watu walioathiriwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, ili waweze kupatiwa misaada ya haraka.

Amesema mvua hiyo imeleta athari kubwa kwa baadhi ya wananchi hasa katika maeneo ya Mjini na Magharibi, na kwamba misaada ya haraka inahitajika kwa waathirika hao.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akifanya ziara ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo yakiwemo Mwanakwerekwe, Kwahani na Jang’ombe, ambapo baadhi ya nyumba zimeathiriwa kabisa na kupekelea baadhi ya wananchi kukosa makaazi.

Sambamba na hilo Maalim Seif ameeleza haja kwa Baraza la Manispaa na Idara ya Ujenzi kufanya utafiti wa kina juu ya hali ya mitaro katika manispaa ya Zanzibar, ikiwa ni njia moja wapo ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la kupita na kutuama kwa maji katika maeneo hayo.

Ametoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyoathirika na mvua hasa yale yaliyo karibu na maziwa, kuchukua tahadhari hasa kwa watoto ambao hupenda kucheza kwenye maeneo hayo bila ya kujua athari zinazoweza kujitokeza.

Akiwa katika eneo la bwawa la Mwanakwerekwe ambapo kijana mmoja Hamad Juma Suleiman (26) mkaazi wa Mwanakwerekwe alizama na bado hajaonekana, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekitaka kikosi cha zimamoto na uokozi kuendelea kumtafuta mtu huyo ili aweze kustiriwa.

Naibu Kamishna wa kikosi cha zimamoto na uokozi Zanzibar Bw.  Gora Haji Gora, amesema wanaendelea kumtafuta kijana huyo, licha ya kukabiliwa na changamoto zikiwemo mavumbi mengi yatokanayo na takataka katika eneo hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 

Mhe. Mohd Aboud Mohd, amesema Serikali iko pamoja na waathirika hao na inaendelea na taratibu zake ili iweze kuwapatia misaada inayohitajika.
Mhe. Aboud ambaye Ofisi yake ndiyo inayohusika na maafa, amesema tayari wameshawasiliana na Wakuu wa Wilaya ili kufanya tathmini na kuweza kuwahudumia waathirika hao ambapo kipaumbele kitatolewa kwa wale waliokosa makaazi kabisa.

Mapema Mkuu wa Idara ya kazi, ujenzi na mazingira kutoka Baraza la Manispaa la Zanzibar Bw. Mzee Khamis pamoja na Mkurugenzi Idara ya Ujenzi Bw. Ramadhan Mussa Bakar, wamekiri kuwa athari za mvua hizo zimetokana na matatizo ya mitaro katika maeneo hayo.

Wameeleza kuwa tayari upo mpango wa kuyafanyia utafiti maeneo na mitaro katika manispaa ya Zanzibar ili waweze kuirekebisha na kupunguza athari hizo.
Wamesema athari hizo zinaweza kuondoka iwapo mitaro ya uhakika inayopeleka maji baharini itajengwa na kutunzwa.

Hata hivyo wataalamu hao wa ujenzi, wamewashauri wananchi kujenga utamaduni wa kutupa taka katika maeneo yaliyotengwa kwa kazi hiyo, na kuacha kutupa taka hizo kwenye mitaro, jambo ambalo hupelekea mitaro hiyo kuziba mara kwa mara na kusababisha mafuriko.

Sheha wa shehia ya Jang’ombe Bw. Khamis Ahmada Salum na Sheha wa Kwahani Bw. Nassir Ali Kombo wamesema maeneo hayo yamekuwa yakiathirika kila ifikapo msimu wa mvua kubwa, na kuiomba serikali kuweka utaratibu wa kuyadhibiti maji hayo.

Kutokana na mvua hizo zinazoendelea kunyesha, inasadikiwa kuwa zaidi ya familia mia moja zimeathirika zikiwemo zile zilizokosa makaazi kabisa, huku mtu mmoja akithibitishwa kufariki katika bwawa la Mwanakwerekwe na mwengine ambaye alizama kwenye bwawa hilo hadi tunatuma taarifa hizi bado hajaonekana.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.