STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22.1.2016
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed
Shein leo ameongoza mazishi ya marehemu Bi
Asha Bakari Makame aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT).
Mazishi ya Marehemu Bi Asha Bakari Makame yalifanyika huko Kianga, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Mkoa wa Mjini
Magharibi kwa heshima zote za Chama Cha Mapinduzi, ambapo viongozi mbali mbali
wa vyama na serikali walihudhuria akiwemo
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais
Balozi Seif Ali Idd.
Wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Dk. Mohammed Gharib Bilal pamoja na
Rais wa Zanzibar mstaafu Dk. Amani Abeid Karume na wananchi.
Mapema asubuhi, Alhaj Dk. Shein alifika
nyumbani kwao marehemu huko Jangombe, mjini Unguja kwa ajili ya kutoa mkono wa
pole kwa wana familia pamoja na kumuombea dua marehemu.
Baada ya hapo Alhaj Dk. Shein alishiriki katika
dua maalum (hitma) pamoja na sala ya
kumsalia Marehemu Bi Asha Bakari Makame iliyofanyika huko Masjid Noor Mohammad,
Mombasa kwa Mchina mjini Unguja.
Akisoma wasifu wa Marehemu, Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa Marehemu Bi Asha Bakari Makame
alizaliwa Disemba 12 mwaka 1949 huko Mtambwe, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Kwa mujibu wa maelezo ya Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar, Marehemu Bi Asha alipata elimu ya msingi huko huko
kijijini kwao Mtambwe na baadae alijiunga na Skuli ya Sekondari ya Fidelcastro huko
Kisiwani Pemba hadi Kidato cha nne ambapo baada ya hapo alienda nchini Bulgaria
kwa ajili ya kujiendeleza kwa elimu ya Diploma ya Siasa na Utawala.
Vuai alieleza kuwa tokea uhai wake,
Marehemu Bi Asha Bakari Makame, akiwa skuli na baada ya kumaliza skuli alikuwa
akijishughulisha na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Afro Shirazi Party (ASP) na
baadae alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pale kilipoanzishwa mnamo mwaka
1977.
Katika uhai wake Marehemu Bi Asha Bakari
Makame, aliwahi kushika nyadhifa mbali
mbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na Serikali ikiwemo Naibu Waziri,
Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo ambapo pia, aliwahi kuwa Waziri wa
Wanawake na Watoto.
Marehemu Bi Asha Bakari, alichaguliwa
kuwa Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wanawake (UWT) Taifa mnamo mwaka 1983 na
baadae alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo nafasi aliyoendelea
nayo hadi kufa kwake.
Naibu Vuai katika akisoma wasfu huo wa
Marehemu alisema kuwa marehemu Bi Asha
katika maisha yake alikuwa muumini wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar ya
Januari 12, 1964 pamoja na kuwa muumini wa kweli wa Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar uliofanyika mwaka 1964.
Marehemu Bi Asha Bakari Makame, katika
kipindi chake chote alichotumikia chama cha CCM pamoja na serikali alikuwa
kiongozi muaminifu, muadilifu, mchapakazi na asiyeyumba katika masuala ya
msingi.
Naibu Vuai alisema kuwa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kinatoa mkono wa pole kwa ndugu na jamaa wote wa marehemu. Nao
wanafamilia walitoa shukurani Kwa wale wote waliohudhuria mazishi hayo.
Marehemu ameacha watoto watatu, wakiwemo
wawili wa kike na mmoja wa kiume Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala
pema peponi. Amin.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment