Habari za Punde

‘Anzeni kwenye vikundi vyenu utawala bora, demokrasia’



Na Haji  Nassor, Pemba

VIKUNDI vya ushirika vya wanawake kisiwani Pemba, vimetakiwa kujidhatiti kuhakikisha suala la demokrasia, utawala bona na wa sheria unaanzia kwenye vikundi vyao, badala ya kulalamikia kutokuwepo kwa hali hiyo, kwenye serikali kuu.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya wanawake na watoto Pemba, Dina Juma Makota, alipokuwa akifungua mafunzo ya haki za binadamu kwa vikundi hivyo vya mkoa wa kaskazini Pemba, yaliofanyika Kituo cha Huduma za Sheria ZLSC mjini Chakechake.

Alisema ya utawala bora na demokrasia, kamwe haihusiki kutekelezwa na serikali pekee, ambapo hasa hutakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia, vikundi vya uhsirika, shehiani na kisha serikali kuu.

Alisema kama viongozi wa asasi hizo watajipanga kuhakikisha wanakuwa na demokrasia kwa mamlaka ya uamuzi kuwakabidhi wanachama wao,  bada ya wachache kuwa ndio waamuzi dhana hiyo itakuwa endelevu.

“Jamani wanawake wenzangu, lazima suala la utawala bora, demokrasia na utawlaa wa sheria lianzie kwenye familia zetu, na kisha hata ndani ya vikundu vyetu’’,alifafanua.

Hata hivyo aliwashauri wanawake hao kuhakikisha elimu ya haki za binadamu watakayoipata kuwaelimisha wenzao kwa vile wao ni sehemu ya wawakilishi wa wengine.


Kwa upande wake Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Fatma Khamis Hemed, alisema ujasiri wa wanawake uonekane pia kwenye suala la kuzilinda na kuziheshimu haki za binadamu.

“Hata kwenye vikundi vyetu vya ushirika huko, lazima tuhakikishe sisi wanawake tusiwe mstari wa mbele kuvunjiana haki za binadamu, na badala yake tuwe walinzi’’,alifafanua.

Mapema Afisa Mfawidhi wa oifisi ya haki za binadamu na utawala bora Pemba, Suleiman Salim akiwasilisha mada juu ya haki za binadamu, alisema haki hizo ni za asili kutoka kwa Muumba mwenyewe.

“Unajua haki hizi zipo tokea asili, na sheria, katiba na mikataba mbali mbali yamekuja kwa ajili ya kuzilinda na kuona kuna kuwa na njia za kisheria pale zinapovunjwa’’,alifafanua.

Washiriki wa mafunzo hayo, walisema bado haki za bindamu zimekuwa zikivunjwa pasi na sheria kuchukua mkondo wake ipasavyo, licha ya elimu inayoendelea kutolewa.

Katika mafunzo ambayo yamewashirikisha wanawake 40 wa vikundi vya ushirika vya mkoa wa kaskazini Pemba, mada kadhaa ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na haki za binadamu

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.