Habari za Punde

Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO Yatoa Msaada wa Fedha,Shilingi Milioni Tano na Vifaa vya Michezo kwa Watoto wa Kituo cha Amani Center cha Mjini Moshi

Meneja wa Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo kanda ya Kaskazini,Henry Kinabo (kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 5 afisa uhusiano wa kituo cha kulea watoto waishio kwenye mazingira magumu cha Amani Center ,Kampuni ya Tigo imetoa kiasi hicho cha fedha pamoja na vifaa vya michezo kwa ajili ya maandalizi ya mbio za Kilimanjaro Marathoni.
Meneja wa kampuni ya Tigo Kanda ya Kaskazini,Henry Kinabo akikabidhi fulana kwa watoto waishio katika mazingira magumu ya Kituo cha Aman Center cha mjini Moshi.
Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini ,Henry Kinabo akifurahia jambo na afisa uhusiano wa kituo cha kulelea watoto waishio katika mazingira magumu cha Amani Center ,Salma Khatibu,wengine ni watoto waishio katika kituo hicho.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

Moshi, Februari 25 2016: Tigo Tanzania leo imetoa mchango wa vifaa vya michezo na pesa taslimu 5m/- kwa kituo kinacholelea watoto wa mitaani cha Amani kilichopo mjini Moshi kukisaidia kushiriki katika mashindano ya mwaka huu ya mbio za Kili Marathon.
Akiongea katika makabidhiano ya msaada huo kituoni hapo, Mkurugenzi wa Tigo wa Kanda ya Kaskazini George Lugata amesema, “msaada huu ni sehemu ya jitihada mbalimbali za kampuni ya Tigo katika kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto za kimaisha na kuinua hali ya maisha ya watanzania kama ilivyoainishwa katika sera yetu ya kuisadia jamii.”
Aidha aliendelea kusema: “Tunaamini msaada huu utaleta tabasamu katika nyuso za watoto na walimu wa Amani Centre na kuwasaidia kufanya vizuri katika mshindano ya Kili Marathon.”
Mashindano ya Kili Marathon ambayo mwaka huu yanadhaminiwa na Tigo pamoja na kampuni zinginezo, yanafanyika mjini Moshi jumapili ijayo.
Akipokea msaada huo kutoka Tigo, Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Centre,Meindert Schaap  ameishukuru Tigo kwa moyo wa upendo na kuahidi ushindi kwa washiriki kutoka Amani Centre katika mashindano ya Kili Marathon.

“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Tigo kwa msaada huu na tunaamini hii ni motisha tosha kwa washiriki wetu katika mbio za Kili Marathon kufanya vizuri na kukipa ushindi na sifa kituo chetu,”alisema Schaap.

Kituo cha Amani centre kilianziswa mwaka 2008 kwa lengo la kuwapa hifadhi na elimu watoto waishio katika mazingira magumu. Mpaka sasa kituo kina jumla ya watoto 71 wakiwemo wavulana 58 na wasichana 13.
Mwisho.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.