Habari za Punde

Wananchi wameshauriwa kuacha tabia ya kula katika mazingira si salama

Na Magreth Kinabo –MAELEZO
Wananchi wameshauriwa kuacha tabia ya kununua matunda yaliyomenywa barabarani au kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira ambayo si safi na salama ili kuweza kuepuka ugonjwa kipindupindu na kulinda afya zao.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto,Michael John wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dares Salaam kuhusu taarifa za ugonjwa huo kwa nchi nzima.

“Suala la kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu linahitaji ushirikiano wa watu wote.Usiponunua matunda yaliyomenywa na watu wanaouza barabarabani, hata wale wanaouza wataacha kuuza. Pia Serikali itatumia nguvu kidogo kwa ajili ya  kuwadhibiti,” alisema John.

Akizungumzia kuhusu juhudi zinazofanyika za kukabialiana na ugonjwa huo, alisema hivi sasa kuna timu ya wataalamu ambayo imekwenda Morogoro ikiongozwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Mpoki Ulisubisya na nyingine mkoani Dodoma ambayo itakuwa na Waziri wa wizara hiyo,Ummy Mwalimu  ili kuweza kushirikiana  na mamlaka, watendaji na baadhi ya wadau kuudhibiti ugonjwa huo.

Aliongeza kuwa ripoti ya ugonjwa huo kwa kipindi cha wiki jumla ya wagonjwa 459 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo katika mikoa 15 na vifo vitano.
Alisema mkoa wa Simiyu ndio unaongoza kuwa na idadi ya wagonjwa wengi, ukifuatiwa na Mwanza, Mara na Morogoro. Pia mikoa ya Njombe , Ruvuma na Mtwara haijawahi kuripotiwa na ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.