Habari za Punde

Dk Shein Aipongeza China kwa Juhudi Zanazochukulia na China na India.katika Kuiunga Mkono Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                         
                                                                        26.08.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Serikali ya India katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kukuza uchumi wake.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati  alipokuwa na mazungumzo na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliyepo Zanzibar  Xie Xiaowu na Balozi Mdogo wa India Mhe. Tek Chand Barupal kwa nyakati tofauti walipofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.

Katika mazungumzo yake na Balozi Mdogo mpya wa China  Xie Xiaowu Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China umeleta mafanikio makubwa ya maendeleo ya kiuchumi pamoja na kuimarisha huduma za jamii hapa nchini.

Dk. Shein alieleza kuwa China na Zanzibar zinauhusiano wa muda mrefu ambao unaendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa muda wa miaka 52 hivi sasa jambo ambalo pande zote mbili zinajivunia.

Alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano huo na ushirikiano kati yake na China ambao umeasisiw na viongozi wakuu wa nchi hizo ambao ni Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na kiongozi muasisi wa China Marehemu Mao tse tung.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo elimu, kilimo, afya, viwanda, miundombinu na nyenginezo huku akiipongeza nchi hiyo kwa  kuimarisha uchumi wake.

Aidha, Dk. Shein aliipongeza China kwa kuiunga mkono Zanzibar katika ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee huko kiswani Pemba ambapo ujenzi wake  unatarajiwa kukamilika hivi karibuni, ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri ambapo ujenzi wake nao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Nae Balozi huyo Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China aliyeko Zanzibar Xie  Xiaowu alimuhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar kwa lengo la kuzidisha uhusiano na ushirikiano uliopo ambao una historia kubwa.

Balozi Xie aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuimarisha na kuendeleza sekta za maendeleo  sambamba na kukuza uchumi Zanzibar.

Pamoja na hayo, Balozi Xie alisema kuwa nchi yake itahakikisha inaendeleza ujenzi wa miradi yote iliyoanzishwa hapa Zanzibar pamoja na kuendeleeza mengine mipya ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa nafasi za masomo na ufadhili kwa Zanzibar pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uvuvi wa bahari kuu.

Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa India Tek Chad Barupal, ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walikubaliana kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa asili kati ya pande mbili hizo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar na India zina historia kubwa ambayo imeweza kuwafanya watu wa pande mbili hizo kukuza udugu wao hadi hivi leo huku akisisitiza kuwa Zanzibar na watu wake wataendelea kuthamini udugu huo.

Akielezea juu ya ushirikiano na uhusiano kati ya India na Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana ushirikiano uliopo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ushirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, biashara, miundombinu, huduma za kijamii na nyenginezo.

Kwa upande wa sekta ya biashara, Dk.Shein alisema kuwa Zanzibar na India zimekuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara ikiwemo biashara ya karafuu na biashara nyenginezo ambapo sekta hiyo nayo imeweza kukuza udugu huo kati ya watu wa pande mbili hizo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa India kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kadhaa za masomo kwa Zanzibar nchini India katika kada mbali mbali.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa lengo na madhuminu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha sekta ya viwanda vidogo vidogo sambamba na kuvifufua vile vya asili vikiwemo viwanda vidogo vidogo vilivyopo Amani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, hivyo matarajiao makubwa ni kwa nchi hiyo kuweza kuiunga mkono Zanzibar katika kufanikisha hilo.

Nae Balozi  Barupal alimuhakikishia Dk. Shein kuwa India itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo kwani inatambua na inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.