Na. Maida Hamza - MCC
Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar imeishukuru Taasisi ya kujitolea ya kutoa huduma (VSO) kwa kuwapatia ufadhili wa mradi wa kilimo cha matunda na mbogamboga .
Mwenyekiti wa Jmumuiya hiyo Nd.Ali Omari Makame amesema Taasisi hiyo pia imewapatia mabwanashamba kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wanaojishughulisha na kilimlo hicho kwa lengo la kujiongezea kipato.
Ndugu Makame ameeleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari Makao makuu ya Umoja huo Wireles Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Amesema Umoja huo pia unaendesha programu ya kutoa taaluma na mikopo ya fedha kwa wakulima wa mbogamboga na matunda pamoja na wafanya biashara wadogowadogo wa maduka, mitumba, tungule, mkaa ili kupata pesa ambazo zinaweza kuendeleza maisha yao ya kila siku
Mwenyekiti wa Umoja wa watu wenye ulemavu ameongeza kuwa katika kuwasaidia vijana walemavu ambao hawana uwezo wa kujiendeleza katika elimu ya juu wanawasidi vifaa na fedha ili kuhakikisha nao wanapata fursa hiyo kama wanayopata vijana wengine.
Ndugu Makame ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwapatia madaktari wa kushirikiana na maafisa wa walemavu vijijini kuwatambua watoto wenye ulemavu na kuwapatia visaidizi.
Ameongeza kuwa katika kuimarisha Jumuia yao, wameanzisha darasa la lugha za alama na watu wote wanaopenda kushiriki wanakaribishwa kujiunga katika darasa hilo ili kuimarisha mawasiliano kati yao na watu wa kawaida.
Amelalamikia watu wenye ulemavu kukosa nafasi ya kushirikishwa katika kamati za sheha na udiwani hali inayopelekea kukosa utetezi wa maslahi ya walemavu katika ngazi za shehia na wadi.
Aidha amesema jumuia yao imekuwa ikichukua hatua ya kusimamia kesi za udhalilishaji wa kijinsai kwa walemavu kwa kuandaa taratibu katika kutoa ushahihidi inapohitajika.
Ametoa wito kwa jamii kuliona suala la walemavu ni suala la wananchi na sio lao peke yao ama taasis zinazowasaidia ili kujenga jamii iliyobora na kupunguza tofauti baina ya walemavu na wasio walemavu.
No comments:
Post a Comment