STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 8.08.2016
VIKAO vya
kujadili mipango ya Utelekezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020
viliendelea tena jana Ikulu mjini Zanzibar chini ya Uenyekiti wa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika vikao
hivyo vya jana Rais alikutana, kwa nyakati tofauti, na viongozi wa Wizara ya
Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji.
Akivifunga
vikao hivyo kwa nyakati tofauti, Mheshimiwa Rais alisisitiza umuhimu wa
viongozi wa Wizara hizo kusimamia kwa karibu Wizara zao na kuweka uwiano
halisia wa majukumu ya ofisi zao Unguja na Pemba kwa kufanya ziara za kikazi
mara kwa mara kisiwani Pemba wakiwa na malengo maalum yanayoeleweka.
Alibanisha
kuwa kwa kufanya hivyo wizara zitaweza kupata picha kamili ya utekelezaji wa
majukumu ya wizara zao na kurasihisha majadiliano ya ripoti za tathmini ya
utekelezaji wa kazi za wizara maarufu ‘Bangokitita’ vinavyofanyika kila baada
ya robo mwaka.
Akizungumza
katika kikao cha wizara yake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji
Balozi Ali Karume alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa namna anavyofuatilia utendaji
wa wizara jambo ambalo linazidi kuwapa viongozi ari na kuweza kufanya kazi kwa
kujiamini zaidi na kufanya maamuzi stahiki
na kutenda kazi zao kwa ufanisi.
Kwa upande
wake Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohamed
alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa jukumu alilomkabidhi kuongoza Wizara hiyo
atalitekeleza kwa umakini lakini ameishauri serikali kuongeza bajeti ya kilimo
hadi kufikia asilimia kumi ya bajeti ya serikali ili kwenda sambamba na
utekelezaji wa Azimio la Maputo.
Kuhusu
kujitosheleza kwa chakula ambapo serikali imeweka lengo la kuzalisha asilimia
80 ya mahitaji ifikapo mwaka 2020, Waziri huyo alisema utekelezaji wa lengo
hilo unaweza kufikia mapema zaidi endapo kuwatakuwa na ushiriki wa kweli wa
sekta binafsi katika sekta ya kilimo.
Mapema Dk.
Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana,
Wanawake na Watoto na kusisitiza haja kwa Wizara hiyo kuendelea kuzisaidia
familia zinazoishi katika mazingira magumu.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisisitiza kuwa Wizara hiyo ina kila sababu ya kuendelea
kuzisaidia familia hizo sambamba na kutoa taarifa kwa Serikali ili taratibu
zaidi ziendelee kuchukuliwa.
Aidha, Dk.
Shein alisisitiza haja kwa viongozi wa Wizara hiyo kufanya ziara za mara kwa
mara Unguja na Pemba ili kujua shughuli na harakati za kiutendaji katika Wizara
hiyo.
Sambamba na
hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Wizara hiyo kutokana na
juhudi inazozichukua katika kuhakikisha inatekeleza vyema majukumu yake huku
akiwasisitiza viongozi wa Wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu
zaidi.
Nao uongozi wa
Wizara hiyo ulieleza jinsi unavyoendelea na juhudi za kuhakikisha inasimamia
miongozo ya kazi, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, kuwawezesha wananchi
kiuchumi sambamba na kuimarisha maendeleo ya Wanawake, Wazee, Vijana na Watoto.
Vikao hivyo
vinatarajiwa kuendelelea hapo kesho.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment