STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.10.2016
WIZARA ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na
Watoto imeeleza haja ya kutambua vyema
taarifa na kumbukumbu za wageni wanaokuja kufanya kazi ama kuekeza hapa
Zanzibar ambao hutoka nje ya Tanzania ili kuepuka changamoto za kiusalama,
ajira na masuala mengineyo ya kijamii.
Hayo yameelezwa leo na
uongozi wa Wizara hiyo, huko Ikulu mjini
Zanzibar katika kikao maalum kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na uongozi wa Wizara hiyo ilipokuwa
ikiwasilisha Taarifa yake ya Utekelezaji
wa Mpango Kazi wa Wizara kwa kipindi cha
Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Katika maelezo yake, Waziri
wa Wizara hiyo Maudline Cyrus Castico alieleza kuwa kuna umuhimu wa kuchukuliwa
juhudi za makusudi katika kujua taarifa na kumbukumbu kwa wawekezaji na
wafanyakazi wanaotoka nje ya nchi kwa ajili kuepuka changamoto kadhaa ambazo
zingeweza kupatiwa uvumbuzi mapema iwapo hatua zitachukuliwa.
Waziri Castico pia,
alieleza haja kwa Serikali kuweka mkakati maalum kwa baadhi ya watoto ambao
hutembea nyakati za usiku mkubwa ili kuwakinga na matukio mabaya ambayo yanaweza
kuwatokezea nyakati hizo.
Aidha, alizieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara
yake katika kuielimisha jamii kupitia vyombo vya habari, juu ya kuepukana na mambo mbali mbali yenye athari kwa jamii
likiwemo suala zima la udhalilishaji hapa nchini.
Waziri Castico alitumia
fursa hiyo kwa niaba ya viongozi na wafanyakazi wa Wizara yake kutoa pongezi
kwa Dk. Shein kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuliongoza Taifa na kusisitiza kuwa
uongozi wake umeleta maendeleo endelevu katika nyanja zote za siasa, uchumi,
ustawi wa jamii, elimu, miundombinu, utamaduni na maendeleo mengine kwa ujumla.
Sambamba na hayo,
Waziri Castico alieleza kuwa Zanzibar imeendelea kuwa na amani na utulivu jambo
ambalo linatoa faraja na ni nyenzo kubwa ya kujiletea maendeleo endelevu kwa
wananchi.
Uongozi huo, ulieleza
jinsi Zanzibar inavyopata sifa kubwa Kimataifa kutokana na kuanzisha Pencheni
Jamii kwa wazee kuanzia miaka 70, ikiwa ni miongoni mwa juhudi kubwa za uongozi
wa Dk. Shein katika kuhakikisha wazee wanaenziwa, wanatunzwa na wanaendelea
kuyafaidi matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar
ya Januari 12, 1964.
Nae Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa upande wake
alitoa pongezi kwa Wizara hiyo huku akieleza juhudi mbali mbali zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la ajira,
uwezeshaji, wazee, vijana, wanawake na watoto.
Dk. Shein alieleza
kuwa ni jukumu la kila mwananchi kupiga vita suala zima la udhalilishaji kwa
watoto na hata watu wazima wakiwemo wanawake huku akieleza mikakati
inayoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza haja ya kutolewa elimu kwa wananchi juu ya usalama katika maeneo
yao ya kazi pamoja na nyumba zao wanazoishi
ili kuepuka majanga na athari zinazoweza kutokezea huku akieleza umuhimu wa
mashirikiano kati ya Wizara hiyo na Mawakala wanaowapeleka vijana kufanya kazi
nje ya nchi.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alitilia mkazo suala zima la kupata
taarifa na kumbukumbu sahihi za wageni wanaokuja hapa nchini kwa ajili ya
kufanya kazi au kuekeza na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na
uongozi pamoja na watendaji wa Wizara hiyo.
Balozi Seif alieleza
kuwa Serikali italiangalia kwa mtazamo maalum suala zima la udhalilishaji
pamoja na matembezi ya watoto wadogo nyakati za usiku mkubwa huku akieleza haja ya kuendeleza mashirikiano
kati ya Wizara hiyo na Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Katibu Mkuu wa
Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza
uwasilishwaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo na kusisitiza suala zima la taarifa
kwa wageni huku akigusia suala zima la viongozi kuwasimamia vyema wafanyakazi
wao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment