Habari za Punde

Shamba-Shamba-Shamba


ASALAM ALAYKUM!
Shamba, naenda shamba, leo shamba na mji hakujakuwa na tafauti baina yao. Huko nyuma ukenda shamba ilifika kuwaaga majirani nakuomba radhi pamoja na kutoa buriani na kutaka kusameheyana kutokana na shamba kuwa ni mahali pambali kabisa.


Leo mashamba yamefinywa na umamboleo wa teknolojia mpaka kuwa hakuna popote pale paitwapo shamba pakawa ni mbali, hadi ikafikia mtu akafikiria mara khamsini akitaka kwenda shamba.

Makunduchi ni shamba na unaambiwa ni maili 45 huko nyuma gari la shamba au wengine wakiliita Matwana, kwa gari ya Makunduchi ilikuwa ni nambari 10, likitoka Makunduchi saa 12 za asubuhi na wengine wakiwa wameweka nafasi tangu kumi ya usiku na kwenda Msiktini ili nafasi yake isichukuliwe.

Gari likitoka huko Makunduchi hata likifika mjini basi aliyopakiwa huwa chichi Kituo cha mwisho wa gari hilo ni markiti Darajani, basi siku hizo safari ya gari hilo nikuja mara moja na kurudi mara moja, wapi leo Makunduchi hata saa 8 za usiku utaweza kupata usafiri wakurudi mjini. Umamboleo wa Teknolojia umeyafinya masafa na kuwa sio lolote lile.


Taib! Shamba na iwe shamba lakini asiwe Mshamba, lakini wewe Mshamba nini? Ushamba na Mshamba ulikuwa unaleta maana mbalimbali, hata wewe wa mjini ukifanya mambo shaghala baghala basi siku hizo ukiitwa mshamba.

Kinachonijia juu ya shamba ni Insha za Bwana MSA, hadi leo najiuliza ilikuwaje sisi vijana wa mtaani Kikwajuni tusiokua tunajua kitu na ndio kwanza tupo Secondary school, Bwana MSA akawa anatupa maandiko yake eti tuyafanyie uhakiki na kumpukutishia makosa ya kiuandishi.


Nafikiri Bwana MSA akiona siku zitapita na hatokuweko duniani na wachache watazikumbuka kazi zake basi kina sisi tupendao kubwabwaja tutamzungumza labada huko ndipo alipokuwa anapo papiga.

Bwana MSA alikuwa na Insha zifwatazo, Roho nenda na zako, Mchuchu sio mke wa kumuoa, Bwawani na wageni bila ya kuisahau Shamba, Insha hizo zilikuwa zimejaa falsafa na tasnifa ndani yake, leo nitaifasili Insha yake ya shamba.

Akilieleza shamba na mjini na akafika hadi kusema shamba lipo Unguja tu halipo popote pale duniani. Akaendelea mbele na kusema ili uwe na shamba lazima kuwe na pahali penye mkusanyiko mkubwa wa watu na biashara na kuwe na markiti, kisha ukitoka hapo mjini utakuja ng’ambo na ukishatoka ng’ambo utakuja katika viunga ambapo hupo mjini wala hujaingia shamba, sasa kwenye viunga ukivimaliza utaanza kuona mikarafuu hapo ndipo panapoanzia shamba na kwa hali hiyo, hata Pemba shamba halipo, kwani ukiteremka bandarini iwe Mkoani au Wete utakutana na mikarafuu.

Hapo utaona falsafa na utaona nini alichokuwa anakizungumzia na mie nimegubikwa na nadharia hii ya shamba sijui wewe mwenzangu unasemaje?

Hawa magwiji wa riwaya na maandishi mbalimbali hapa kwetu Tanzania akiwa Bwana MSA na Shaaban Robert nani anawazungumza? Leo huzungumzwa watu hata hujui kile walichochangia, lakini utakuta watu hao wameenziwa hii kweli inakuwa ni haki?


Nakuachia hapo.
Ngaridjo Onana
Hamza Z. Rijal

Via Facebook

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.