Habari za Punde

GEWE: Udugu wa damu kikwazo kumaliza udhalilishaji Pemba


Na Haji Nassor, Pemba
UJOMBA, ushangazi, uami na ujirani mwema ni mambo yaliotajwa kuwa yanachangia kwa kiasi kikubwa kutomalizika kwa matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto yaliyoota mizizi ndani ya jamii.
Kauli hiyo imetolewa na wajumbe wa kamati ya GEWE wa shehia sita za wilaya ya Wete, wakati wakizungumza kwenye mkutano wa kumalizika kwa mradi huo, uliofanyika Kiuyu Kigongoni wilayani humo.
Wajumbe hao walisema, mradi huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuibua na kuyafuatilia matendo hayo, ingawa wamebaini kuwa ukaribu wa wafanyaji na wafanyiwa huzorotesha kuyamaliza.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Khamis Shaaban alisema, kwa vile wanaofanya matendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, ni wanafamilia moja, hivyo huwa vigumu kutoa ushirikiano hasa wanapoanza kutaja Polisi na mahakama.
“Mtoto akianza bakwa, wazazi huwa wakali na hushirikiana na waratibu wa wanawake na watoto kwa ukaribu, lakini kadri kesi inavyokaribia kufikishwa mahakamani, hufanya sulhu’’,alifafanua.
Nae sheha wa shehia ya Mchangamdogo Asaa Makame Said, alisema mradi wa GEWE, umesaidia jamii kupata hofu ya kufuatilia matendo hayo yanapojitokeza.
“Tatizo sugu ambalo tumekumbana nalo wakati wa kuyafuatilia matendo hayo, ni wale wafanyaji kuwa na uhusiano wa kidamu na wafanywaji, sasa hapo kinachopita ni sulhu’’,alifafanua.
Kwa upande wake Mratibu wa shehia ya Kangagani Awena Salim Kombo, alisema jamii kutokubali kutoa ushahidi hata kwa matukio walioyashuhudia nalo ni tatizo jengine walilolibaini.
Hata hivyo Mratibu wa shehia ya Mjini Ole Khadija Henock Maziku, alisema pamoja na mradi huo kuasaidi, lakini haja ya kuzaliwa mradi mwengine ipo.
“Mradi huu wa GEWE wa mwaka mmoja, umesaidia hasa katika shehia yangu, lakini TAMWA haina budi kuja na mradi ambao utawaonyesha jamii athari za kukalia ushahidi na kuzifanyia sulhu kesi za udhalilishaji’’,alifafanua.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa Jamii wilaya ya Wete, Haroub Suleiman Hemed, aliwataka masheha na waratibu hao kujenga ujasiri na uaminifu wakati wanapozifuatilia kesi hizo.
Afisa mradi huo kutoka Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA ofisi ya Zanzibar Grace Ngonyani alisema kumalizika kwa mradi huo sio mwisho wa mapambano.
“Ijapokuwa mradi unatia nanga mwezi Disemba mwaka huu, lakini nyinyi waratibu na masheha kazi ya kuzifuatilia kesi iendelee, maana ni sehemu ya majukumu yenu’’,alifafanua.
Asha Abdi Makame kutoka TAMWA, aliwataka waratibu hao kufanya kazi zaidi kwa karibu mno na masheha hao, ili wanapoifuatilia kesi wapate nguvu.

Mradi wa GEWE ambao ulikuwa wa mwaka mmoja, kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka huu ulikuwa ukifanya kazi katika shehia sita za Kinyikani, Kiungoni, Shengejuu, Mchanga mdogo, Kangagani na Mjini Ole wilaya ya Wete.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.