STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 5.11.2016
![---](file:///C:/Users/User/AppData/Local/Temp/msohtmlclip1/01/clip_image002.gif)
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mama Mwanamwema Shein amewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
kuendelea kuwaelimisha vijana wasikubali kutumika katika vitendo vinavyoweza
kuvuruga amani huku akiwataka kuieleza jamii kuwa uchaguzi umekwisha hadi mwaka
2020 ndipo utafanyika uchaguzi mwengine.
Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo leo
huko Ikulu ndogo Chake Chake Pemba katika Mkutano kati yake na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wa Majimbo ya Pemba pamoja na wale wa Viti
Maalum.
Katika maelezo yake Mama Shein, aliwataka
viongozi hao kutambua kuwa nyazifa zao ni za ulezi na usimamizi wa jamii
wanayoizunguka ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza vijana kukimbilia katika kazi za
halali zitakazowapatia kipato kwani Serikali haina ajira za kutosha kwa wote
wanaohitaji.
Aidha, aliwataka viongozi hao
kuwaelimisha vijana juu ya madhara ya utumiaji wa dawa za kulevya na kuwataka
vijana walioko skuli kuongeza bidii katika masomo yao kwani nchi hii itajengwa
na wananchi wenyewe hasa vijana wenye maarifa na ujuzi.
“Kwa kuwa mimi ni mzazi, naguswa sana na
hatma ya vijana wetu kuendelea kudanganywa na kudanganyika hivyo tuendelee
kuwaelimisha katika majimbo yetu kuwa wakatae kutumika katika vitendo
vinavyoweza kuvuruga amani, wajue kuwa uchaguzi umekwisha”,alisema Mama Shein.
Mama Shein alieleza kuhuzunishwa kwake na
vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto na kuwataka viongozi hao
kuelekeza juhudi zao katika kuwaelimisha vijana na wazazi juu ya mbinu za hadaa
na mazingira yanayotumiwa na wabakaji na wadhalilishaji wote kwa jumla.
Hivyo, Mama Shein alieleza haja ya kutoa
elimu kwa mtu mmoja mmoja, vikundi pamoja na ngazi za familia na kueleza kuwa
Serikali kwa upande wake imeanza kuchukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na
kuanzisha kampeni maalum ya kutokomeza vitendo hivyo kupitia Wizara ya Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi mbali
mbali.
Pamoja na hayo, Mama Shein alisema kuwa ushindi
mkubwa kilichoupata Chama Cha Mapinduzi kwa
wagombea wake wa nafasi mbali mbali za uongozi wa kisiasa katika Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
kielelezo thabiti cha imani ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa chama
hicho.
Mama Shein alitumia fursa hiyo
kuwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kukipatia ushindi mkubwa chama
cha CCM kutokana na wananchi wa Pemba kuzikubali Sera za CCM pamoja na
kuwakubali wagombea kupitia chama hicho.
Aidha, Mama Shein alisema kuwa miongoni
mwa majukumu ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba chini ya
uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein imedhamiria ni kushirikiana na wananchi
katika kupambana na umasikini.
Mama Shein alisema kuwa Serikali imeandaa
fursa mbali mbali kupitia Wizara zake lakini na viongozi nao wanawajibu wa
kuwaunganisha wananchi na kuwahamasisha kuzifuatilia na kuzitumia fursa hizo
hasa kwa ajili ya kina mama na vijana.
Alisema kuwa kwa upande wao wakiwa wake
wa viongozi wa Serikali wamejiwekea utaratibu wa kuhamasisha na kuongeza nguvu
kwa wale ambao tayari wamehamasika katika suala zima la kupambana na umasikini.
Nae Mke wa Makamo wa Pili wa Rais, Mama
Asha Balozi aliwaeleza viongozi hao umuhimu wa Umoja wa wake wa viongozi kwa
maendeleo ya wananchi wote huku akisisitiza juu ya suala zima la kuendeleza
amani na utulivu.
Aidha, alieleza kuwa suala la udhalilishaji
ni kubwa sana litakuwa ni kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu ya umoja
huo pamoja na kueleza haja ya kuunda Kamati Maalum katika Majimbo ili iwe
kimbilio kwa wananchi pale linapotokea tatizo la udhalilishaji wa wanawake na
watoto ili wapate msaada.
Mjane wa Marehemu Mzee Abeid Amani Abeid
Karume, Mama Fatma Karume, alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Zanzibar pamoja
na kutoa pongezi na shukurani kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiongoza Zanzibar
kwa nguvu zake zote na kuendelea kusisitiza kuwa hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka
2020 wala Serikali ya Mpito na kilichokuwepo hivi sasa ni kuijenga nchi na
wananchi wake ili kuweza kupata maendeleo.
Nao Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa
Majimbo ya Pemba walitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Mama Shein
kwa nasaha zake pamoja na kuahidi kuyafanyia kazi maazimio ya mkutano huo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment