Habari za Punde

Acheni kukumbatia wakandarasi kutoka nje: Balozi Seif


Na Haji Nassor, Pemba
MAKAMU wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Iddi, amezitaka taasisi za serikali nchini, kuacha tabia ya kuwakumbatia wakandarasi wa nje ya nchi, wakidhani kuwa ndio wanauwezo wa kipekee wa kujenga ofisi za umma na sasa wawatumie wakandarasi wazalendo.
Alisema wakandarasi wazalendo, wameibuka kuwa na uwezo mkubwa wa kujenga majengo yenye kuvutia na ya kudumu, ambayo yapo nchini na yanaendelea kutumiwa na serikali.
Balozi Seif, alitoa tamko hilo mara baada ya kufungua jengo la ghorofa mbili la nyumba ya mkaazi kwa askari wa Uhamiaji na maofisa wake, eneo la Ndugu kitu Chakechake Pemba, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za kutumia miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar yalioasisiwa mwaka 1964.
Alisema yapo majengo ambayo yametumia gharama kubwa yaliojengwa na wakandarasi na wasimamizi kutoka nje ya nchi na hatime mengine kabla ya kuhamiwa au kukabidhiwa kwa serikali, yaliporomoko na kuitia hasara serikali.
Alisema jengo la ZSSF lililopo Chakechake Pemba, limejengwa na mkandarasi mzalendo, ingawa jengo la jirani yake lililojengwa na mkandarasi kutoka nje ya nchi, lilianguka kabla ya ujenzi kukamilika.
Alieleza wakandarasi kutoka nje ya nchi, watalazimika kutumika tu pale ambapo, kuna miradi mikubwa ambayo imeambatana na ufadhili wake, na pengine wakandarasi wazalendo hawana uwezo wa kuyajenga.
“Sisi serikalini sasa tunasema kuwatumia wakandarasi wa nje bila ya sababu maalumu, na iwe basi mbona hawa wazalendo wanajenga majengo madhubuti, si mnaona hili la Uhamiaji hapa Ndugu kitu liko safi’’,alisema.
Katika hatua nyengine Makamu huyo wa Pili wa Rais Zanzibar alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zitaendelea kuwajengea wapiganaji wake makaazi bora kila hali ya fedha itakaporuhusu.
Aidha aliwataka wapiganaji hao wa Uhamiaji watakabahatika kukaa kwenye nyumba hiyo mpya na ya kisasa, kuhakikisha wanaitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Hata hivyo ameitaka Idara hiyo ya Uhamiaji, kuhakikisha wanaifanyia matengenezo nyumba hiyo, kila wakati utakapofika na sio kuiacha hadi kuharibika.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya ndani ya nchi, Meja Generali:  Projestus Rwegasira aliomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuendelea kuwapatia maeneo mengine kwa ajili ya kujenga nyumba za kuishi watendaji wa Uhamiaji.
Mapema Kamishina wa Uhamiaji Zanzibar, Johari Massoud Sururu, alisema Uhamiaji iliamua kujenga nyumba hiyo ya ghorofa mbili, kwa ajili ya kupunguza tatizo la makaazi kwa watendaji wake.
Nae Waziri katika afisi ya Makamu wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, alisema Idara ya Uhamiaji imefikia lengo la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yenye azma ya kuwa na makaazi bora na ya kisasa.
“Lengo la Mapinduzi ambayo leo tumo kwenye shamra shamra za kutimiza miaka 53, yalikuwa ni kutukomboa na kisha kuhakikisha tunakuwa na makaazi bora na imara”,alisema.
Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba Mhe: Mwanajuma Majid Abdalla, alisema neema ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, imeshasambaa kila kona ya mkoa wake, ikiwa ni pamoja na huduma za afya, maji safia na salama na mawasiliano ya barabara.

Jengo hilo la ghorofa mbili, ambalo lilianza ujenzi wake mwezi Juni mwaka 2015, na kukamilika Novemba mwaka jana, litakuwa na uwezo wa kukaliwa na familia sita, na limetumia zaidi ya shilingi milioni 989, ambazo zimetolewa na Idara ya Uhamiaji Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.