Habari za Punde

Jamii yaaswa kushirikiana katika harakati zao za kila siku

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja na baadhi ya Viongozi na watendaji wa Ofisi yake kwenye chakula alichokiandaa  nyumbani kwake  hapo Mtaa wa Kama kwa ajili ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka Mpya wa  2017.
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akijichagulia mlo kwenye tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.

 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mahsriki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Muombwa naye hakuwa nyuma kushiriki kwenye tafrija hiyo.

 Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakitunisha misuli katika tafrija hiyo ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ na SMT Nd. Khalid Bakari Amrani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Nd. Ali Juma Hamad na Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe  na maadhimisho ya Kitaifa Bibi Riziki Daniel Yussuf.
 Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo wakifurahia chakula kitamu kilichotayarishwa kwenye Tafrija hiyo ya usiku.

 Familia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ikionekana kupozi kwenye tafrija hiyo wakifuatilia muziki laini uliokuwa ukitumbuiza katika Tafrija hiyo.
 Balozi Seif  Ali Iddi, Mkewe pamoja na Familia yao wakisakata rumba kwenye tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017 nyumbani kwao Mtaa wa Kama.
 Olaaaaaaaa. Ndii. Ni wakati wa kuingia saa 6 na dakika moja ya usiku wa kuingia mwaka mpya wa 2017 washiriki wa tafrija  hiyo wakijimwaga uwanjani kuukaribisha mwaka huo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga  akitoa shukrani kwa  niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi kwa washiriki wa Tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Othman Khamis , OMPR

Jamii imeaswa kuendelea kushirikiana katika harakati zao za kila siku za kimaisha na Kifamilia ili kukifanya kizazi chao kukua katika maadili na utamaduni unaokubalika kidini na kidunia  jambo ambalo litatoa faraja kwa wazazi, walezi pamoja na Viongozi wa Kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mh. Mihayo Juma Nhunga wakati wa hafla maalum ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka Mpya wa 2017.

Mh. Mihayo alisema hayo kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyeandaa hafla hiyo Nyumbani kwake Mtaa wa Kama nje kidogo ya Kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar akiwashukuru  baadhi ya Viongozi na Wafanyakazi wa Ofisi hiyo pamoja na Familia zao walioshiriki katika kuukaribisha mwaka mpya.

Katika kuuaga  mwaka 2016 uliobeba matukio mbali mbali yakiwemo mengi ya udhalilishaji wa Kijinsia ya yale yaliyopoteza maisha ya Wananchi wengi kutokana na ajali za bara barani,  Naibu Waziri Mihayo alisema suala la kupendana miongoni mwa Jamii ndani ya mwaka mpya wa 2017 linafaa kufanywa kuwa jambo la msingi.

Kupitia hafla  hiyo ya chakula cha usiku Mhe. Mihayo Juma Nhunga kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwatakia kheir ya mwaka Mpya Wananchi wote wa Zanzibar  na kuwataka wale waliokoseana ndani ya mwaka uliopita wasameheane.

Alisema Mwaka mpya unahitaji zaidi mambo mapya na ya msingi ili kulifanya Taifa na wananchi wake waelekee kwenye maendeleo yatakayoleta faida na kustawisha maisha yao ya kila siku.

Hafla hiyo ya chakula cha usiku uliyowakutanisha baadhi ya Viongozi  na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Familia zao iliambatana na muziki laini uliotoa burdani safi kwa washiriki hao walioshindwa kukaa kwenye viti vyao na kuonekana wakianza kuserebuka

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.