NA HAJI NASSOR, PEMBA
MADEREVA wa gari na wale wanaoendesha vyombo vya magurudumu mawili Mkoa wa kusini Pemba, wamelalamikia, tabia ya wajasiriamali na wafanyabiashara ndogo ndogo, kupanga bidhaa pembezoni mwa barabara, jambo linalowapa usumbufu wakati wanapochukua au kushusha abiria.
Walisema katika miaka ya hivi karibuni, kumeibuka kundi kubwa la wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuuza matunda au bidhaa kavu kama kwa kuweka meza au masunduku yao pembezoni wa barabra.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa nyakati tofauti, madereva hao walisema, yapo maeneo wananchi hao kwa makusudi wamepanga biashara zao karibu mno na barabra, hali inayosabaisha wanaposimama hulazimika kuzidi barabarani.
Mmoja kati ya madereva hao, Ali Mtumweni Kombo anaefanya kazi zake Mkoani- Chakechake, alisema hali hiyo imekuwa ikiwapa usumbufu, maana hulazimika kuwapitisha abiria wao eneo wanalotaka kushuka.
“Abiria atasema nishushe hapo, lakini ukimpitisha atakulalamikia, kumbe lile eneo alilotaka pana meza za maembe au muhogo wa wafanyabiashara, sasa inakuwa vigumu”,alisema.
Nae Mbaraka Juma Bakar alisema, maeneo kama ya Mtambile njia ya Kengeja, Mgagadu, Kenya, Ngwachani, Kipapo, Chanjamjawiri na hata ndani ya mji wa Chakechake, wafanyabiashara hao wameitumia vibaya barabara.
Kwa upande wake dereva Haji Kassim ‘Nuhu’ alisema wafanyabiashara yale maeneo yaliotengwa kwa ajili ya wao kusimama, ndio yaliotumiwa kuwekewa vibanda au miemvuli ya bidhaa zao.
“Hata ndani ya mji wa Chakechake, waliokodi milango ya biashara kisha wameweka na vibanda vya nyongeza au miemvuli, sasa unapopita na mzigo juu ya gari huwa unasita sita’’,alisema.
Akzungumza na mwandishi wa habari hizi, mfanyabiashara Haji Khatib wa Mtambile, alisema wamelazimika kukaa pembezoni ili kufuata wateja hasa wanaosafiri kutoka eneo moja kwenda jengine.
Nae Mtumwa Khalfan Said wa Chanjamjawiri, alisema sio sahihi kwamba wanavamia maeneo ya barabara, maana wapo waliojenga nyumba lakini hawajalalamikiwa.
Muhandisi wa ujenzi wa barabara kisiwani Pemba Khamis Massoud alisema kutoka ilipoishia barabara (road shoulder) hutakiwa mita 15 kusiweko kitu chochote, kwani kufanya hivyo ni kuondoa matunzo ya barabara.
“Ingawa inategemea na aina ya barabara, lakini kwa barabara kuu zinaounganisha miji ya Pemba, basi mita 15 kusiwe na hata shinda la mgomba, sembuse watu kuweka meza za biashara, hilo ni kosa’’,alieleza.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara, kujiondoa pembezoni mwa barabara, kwani inapotokezea gari kupata hitilafu, waathirika wa kwanza huwa ni wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Shehan Mohamed Shehan aliwataka wafanyabiashara hao, kutii sheria bila ya shuruti kwa kujiondoa pembezoni mwa barabara, na kurudi nyuma, ili kupisha harakati nyengine.
Juzi katika eneo la Chanjamjawiri wilaya ya Chakechake, gari moja aina ya Noha, ilianguka na karibu na meza za wafanyabiashara wa matunda waliopembezoni mwa barabara.
No comments:
Post a Comment