STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Djibouti 8.05.2017
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea Kampuni ya
simu ya ‘Djibouti Telecom Haramuos’ na kupongeza jinsi kampuni hiyo inavyofanya
kazi zake ndani na nje ya nchi hiyo.
Katika
ziara yake hiyo mjini Djibouti, Dk. Shein alipata maelezo juu ya uendeshaji wa
Kampuni hiyo inayojumuisha mkonga wa mawasiliano kupitia katika bahari pamoja
na maeneo ya nchi kavu kwa nchi mbali mbali zikiwemo za Afrika ya Mashariki.
Akipata
maelezo kutoka kwa uongozi wa Kampuni hiyo, alielezwa kuwa zaidi ya nchi 90
zimekuwa zikifaidika na mkonga wa mawasiliano kutoka kampuni hiyo zikiwemo
Ausralia, nchi za Asia, Ulaya na Afrika.
Huduma
za mtandao huo kwa mujibu wa maelezo ya uongozi wa Kampjni hiyo ,zina mchango
mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi na wa kijamii kutokana na kurahisika kwa
mawasiliano ya kimtandao katika shughuli mbali mbali zikiwemo za biashara,
elimu, na afya.
Hata hivyo, uongozi huo
wa ‘Djibouti Telecom Haromous’ ulimueleza Dk. Shein kuwa Kampuni yao bado
inaendelea kupanua soko lake na tayari imeshaanza hatua za mashirikiano na nchi
mbali mbali zikiwemo nchi zilizokuwa hazipitiwa na bahari kama Rwanda na nchi
nyenginezo.
Mapema katika Ofisi za
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Djiboti mkutano maalum wa
kubadilishana mawazo kati ya viongozi waliokuwemo katika ziara hiyo ya Dk.
Shein,kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
walipata fursa ya kubadilishana mawazo juu ya kuimarisha uhusiano na
ushirikiano katika sekta za maendeleo na viongozi wenzao wa Djibouti.
Kwa upande wa viongozi
wa Tanzania, walieleza haja ya kukuza ushirikiano na uhusiano kati ya Tanzania
na Djiboti hasa katika miradi ya maendeleo na kueleza kuwa ziara hiyo
itawezesha kujua mikakati na kujifunza mbinu mbali mbali na baadae kufanyiwa
kazi.
Aidha, viongozi hao
walitumia fursa hiyo kueleza hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi mpya wa miundombinu ya mawasiliano,
bandari.
Pamoja na hayo viongozi
hao kwa pamoja walitoa rai kwa vuiongozi hao wa Djiboti kwa kuwaalika
wawekezaji na wafanyabiashara wa Djiboti kuja kuitembelea Tanzania ikiwemo
Zanzibar sambamba na kuekeza miradi yao.
Pia, viongozi hao
walieleza juhudi zinazochukuliwa katika kuimarisha sekta ya utalii hasa
ikizingatiwa kwamba sekta hiyo ina mchango mkubwa kwa Zanzibar na Tanzania kwa
jumla kutokana na mchango wake katika uchumi.
Nao viongozi wa Djibouti
walieleza kufarajika kwao kwa ziara ya Dk. Shen nchini humo, na kueleza kuwa
ziara hiyo itakuwa mwanga mkubwa katika kuazisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii sambamba na kuimarisha
uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Djibouti na Tanzania.
Viongozi hao walieleza
kuwa nchi yao iko katika usalama mkubwa hivi sasa na ndio imekuwa chachu ya
maendeleo wanayoyapata ikiwa ni pamoja na kuwa kivutio cha wawekezaji kutoka
ndani na nje ya bara la Afrika.
Viongozi hao wajibuti
wakiwemo Mawaziri wan chi hiyo walieleza kuwa Djibouti na Tanzania ina maeneo
mengi ya kushirikiana hasa kwa kuzingatia kufanana kwa mazingira ya nchi mbili
hizo.
Pamoja na hayo, viongozi
hao walieleza mikakati yao ya kuimarisha uchumi wa nchi yao ikiwa ni pamoja na
hatua za kupanua soko nje ya nchi yao pamoja na mashirikiano na nchi nyengine
ambayo yamepelekea kushirikiana katika kuekeza miradi kadhaa ambapo nchi kama
Ethiopia imekuwa ni miongoni mwa nchi hizo.
Viongozi hao kwa pamoja
walieleza haja ya kuwepo kwa ziara za mara kwa mara kwa pande zote mbili ili
kuweza kukaa pamoja na kujadili namna ya kuendeleza na kukuza ushirikiano
katika sekta za maendeleo na uchumi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment