Habari za Punde

Kuelekea Siku ya Mazingira Duniani. Usafi wa kila mwisho wa mwezi waimarisha mazingira nchini


KILA ifikapo Juni 5 kila mwaka, zaidi ya nchi 100 zinaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.Jovina Bujulu wa Idara ya Habari (MAELEZO) anaelezea umuhimu wa siku hii ambayo hapa nchini  itaadhimishwa tarehe 3 na 4  mkoani Mara katika kijiji cha Butiama. 

Muelekea adhumuni makubwa ya maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii duniani kote kuelewa masuala yanayohusu mazingira na pia kuhamasisha watu kulinda na kuhifadhi mazingira. Aidha, ni siku ambayo jamii inatakiwa kutambua umuhimu wa kulinda na kuhifaddhi mazingira kwa ustawi na maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Muungano na  Mazingira, maadhimisho hayo mwaka huu yatafanyika kijijini Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na  kukumbuka mchango wake mkubwa katika masuala ya mazingira.

Wakati wa maadhimsho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika zikiwemo kupanda miti, kuendesha mijadala mbalimbali na kongamano la viongozi kuhusu mazingira na pia kufanya maonyesho ya shughuli za mazingira.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambayo Kauli Mbiu ya mwaka huu ni Hifadhi ya Mazingira: Muhimili kwa Tanzania ya Viwanda atakuwa Makamu wa Rais, Mh. Samia Suluhu Hassan.  Kaulimbiu hii inahamasisha Utunzaji wa mazingira wakati tukielekea uchumi wa viwanda.

Tarehe 9 Desemba mwaka jana, Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli aliamuru kusitisha maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Uhuru wa Tanganyika na badala yake siku hiyo iadhimishwe kwa kufanya usafi wa mazingira nchini kote. 

Katika kutekeleza agizo hilo, Dkt. Magufuli aliwaongoza Watanzania kufanya usafi siku hiyo ambapo yeye pamoja na mke wake Janeth Magufulu walifanya usafi nje ya Ikulu, ufukweni mwa Bahari karibu na Soko la Samaki la Ferry.

Akiongea na Wafanyabiashara waliofika katika eneo hilo kushiriki katika kufanya usafi Dkt. Magufuli alisema “Ni aibu kwa nchi yetu ya Tanzania kuendelea kuwa na ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo mbalimbali wakati ungeweza kuepukwa kwa kujituma kufanya usafi katika maeneo yetu.”

Amesema, suala la usafi ni muhimu katika mazingira anayoishi binadamu kwani bila kufanya hivyo atakuwa amejijengea mazingira hatarishi na hivyo kuweza kupata magonjwa kirahisi. Amesema, Serikali inatumia fedha nyingi kutibu maradhi ambayo yanaweza kuepukika kwa njia mbalimbali ikiwwemo suala la kufanya usafi.

Hivyo, aliitaka jamii kujijengea utamaduni wa kufanya usafi majumbani na mahali pa kazi ili kuepuka magonjwa kama vile kipindupindu.

Akitangaza hatua ya kuifanya  siku ya Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa siku rasmi ya usafi wa mazingira kwa nchi nzima, Naibu Waziri wa Nchi Muungano na Mazingira Luhaga Mpina alisema  uamuzi huo ulifikiwa ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa na utamaduni wa kudumu wa kufanya usafi wa mazingira ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na kupendezesha mazingira.

“Zoezi hili ni la lazima kwa kila Mtanzania bila kujali nafasi yake, cheo chake  au ushawishi wake katika jamii,  watu wote wanawajibika” alisisitiza Waziri Mpina.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene amesema kuwa Watanzania wote wa mijini na vijijini ni budi wajenge desturi ya kuweka mazingira katika hali ya usafi wakati wote na kila mmoja awe mlinzi wa kukemea watu wenye tabia ya kutupa takataka ovyo ili maeneo yote yawe katika hali ya usafi na yenye kuvutia.

Akiongelea tathmini ya siku ya kufanya usafi nchini,  Mkurugenzi Msaidizi, Ofisi ya Rais - Idara ya Mazingira anayesimamia masuala ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira Magdalena Mtenga amesema, mwitikio ni mzuri katika maeneo mengi na Wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kufanya usafi katika siku iliyopangwa.

“Kumekuwa na hali ya kuridhisha ya usafi wa mazingira katika maeneo mengi hapa nchini, hii ni kutokana na usimamizi mzuri wa Halmashauri katika Majiji, miji na Halmashari ambapo wameweka sheria ndogondogo za kuwaadhibu wanaokataa kufanya usafi na wanaochafua mazingira” amesema Mtenga.

Aidha, Mtenga ameeleza kuwa kumekuwepo na mpango nzuri wa kurejerezwa kwa taka ngumu zitokanazo na plastiki ambapo zinarudishwa viwandani na kutengeneza bidhaa nyingine.

Amesema, shughuli za usafi wa mazingira nchini zimekasimiwa kwa  Halmashauri za miji ambapo zinasimamia ujenzi wa vizimba, ukusanyaji, usafirishaji na uteketezaji  katika madampo.

Hata hivyo alitaja baadhi ya changamoto wanazokutana nazo kuwa ni pamoja na ujenzi wa makazi holela, miundombinu kama barabara ambazo hazifiki katika baadhi ya makazi na tabia ya baadhi ya watu kutupa takataka katika maeneo yasiyo rasmi.

Ili kuhakikisha kuwa agizo la usafi linazingatiwa, kumekuwepo na mashindano ya usafi katika ngazi za Majiji, Miji, na Halmashauri ambapo mwaka jana, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilikuwa mshindi wa jumla wa usafi wa mazingira kwa kupata alama 97.

Kutokana na ushindi huo Halmashauri hivyo ilipata tuzo ya gari, kombe, cheti pamoja na pikipiki katika vijiji vitatu ambavyo vilifanya vizuri katika usafi wa mazingira.

Aidha Jiji la Mbeya lilibuka na ushindi wa kwanza kwa upande wa majiji manne hapa nchini na lilizawadiwa kikombe, cheti pamoja na pikipiki. Mji mdogo wa Tunduma uliibuka mshindi kwa upande wa Miji.

Agizo la kusafisha mazingira pia linatekelezwa na makampuni, taasisi binafsi na mashirika mbalimbali ambapo  nao hushikiri kufanya usafi katika maeneo mbali mbali kama vile katika fukwe za bahari, sehemu ya mikusanyiko kama sokoni, na mitaa mbalimbali.

Ili kufanya agizo la usafi wa mazingira kuwa na tija ni budi kila mwananchi ashiriki na kuhakikisha kuwa analinda mazingira kwa gharama yoyote. 

Mazingira yanaweza kulindwa kwa kuhakikisha kwamba vitendo vyote vya uchafuzi kuanzia katika makazi yetu na mitaani vinaepukwa na kila mmoja anakuwa askari wa mwenzie katika suala la usafi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.