Habari za Punde

Manispaa kuzawadia Shehiya zitakazojipanga vizuri katika uhifadhi na utunzaji mazingira

Na Maryam Kidiko – Maelezo 

Baraza la Manispaa Wilaya ya Mjini linakusudia kutowa zawadi kwa shehiya za Wilaya hiyo ziakazofanya vizuri zaidi katika uhifadhi na utunzaji  Mazingira.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Kituo cha afya Chumbuni Mkurugenzi wa Baraza hilo Aboud Hassan Serenge alisema lengo la kutoa zawadi hizo ni kuwashajiisha wanachi kujenga tabia ya kutunza mazingira ikiwa ni moja ya njia ya kupambana na maradhi ya mripuko.

 Alisema Baraza la Manispaa litaendelea kushirikiana  na viongozi wa Majimbo ya Wilaya hiyo kwa  kutoa Vifaa vya kufanyia usafi ili kuhakikisha Mazingira ya mji yanakuwa salama kwa maisha ya wananchi .

“Sisi kama Baraza la Manispaa nijukumu letu kuhakikisha Mazingira yanakuwa masafi hivyo tutashirikiana kwa karibu  na Majimbo kutowa Vifaa vya usafi ili kuhakikisha Mji wetu unakuwa katika hali ya usalama “Alisema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo alisema kuwa kwa wale ambao watajikusanya pamoja na kufanya usajili unaokubalika watawatengenezea mazingira mazuri ya kuhakikisha wanapata ada ya kazi wanayoifanya sambamba na ada ya Vifaa.

Vile vile alieleza kuwa miongoni mwa vitu wanavyo zingatia katika Bajeti yao ni kutoa vifaa kwa ajili ya usafi wa mazingira ili kuepusha kutokea kwa maradhi ya Miripuko .

Sheha wa Shehia ya Kwamtumwajeni, Jimbo la Magomeni, Rajab Ali Ngauchwa alisema  suala la usafi wa  mazingira amelipokea vizuri na kwa kushirikiana na wananchi ameahidi watalisimamia  kwa ukamilifu licha ya chaangamoto ziliopo.

Alizitaja Changamoto hizo kuwa ni pamoja na muitiko mdogo wa baadhi ya wananchi juu ya suala hilo, ukosefu wa vifaa na kukosekana  Sehemu ya kuwekea taka (Madampo).

Sheha Ngauchwa amewataka Wananchi wa Shehia yake  kurejesha utamaduni wa zamani  wa kusafisha mazingira yaliyowazunguka kwa hiari bila ya kushurutishwa jambo ambalo litasaidia kufanikisha kuweka Mazingira Safi.

“Ningependa kuwasisitiza tushirikiane pamoja kuweza kuweka mazingira yetu kuwa safi bila ya kutegemeana na kubaguwana kwa Siasa zetu kwani suala la usafi halitaki siasa,”Alisema Ngauchwa.

Nao Wananchi kutoka Shehia mbali mbali Jimbo la Magomeni Walisema kuwa suala la kuweka Mazingira safi sio suala la kuwaachia Manispaa kufanya usafi peke yao bali  suala hilo linamuhusu kila mmoja wetu.

Sambamba na hayo wamesema suala la kutunza  mazingira ni suala  muhimu na kila mmoja anajukumu  la kuhakikisha mazingira  yaliyomzunguka yanakuwa salama wakati wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.