Habari za Punde

DC Wete ataka ukaguzi ufanyike kuwadhibiti wasafirishaji karafuu bila kibali

Na Salmin Juma, Pemba

MKUU wa Wilaya ya Wete  Rashid Hadid Rashid , amevitaka vikosi vya ulinzi na usalama kufanya upekuzi kwenye madumu na rumbesa za majani ya ng'ombe ambazo zinadaiwa kutumika kusafirishia karafuu kutoka shehia moja kwenda nyengine.

Amesema njia hizo vinatumiwa kwa lengo la kukwepa kukata kibali cha kusafirishia karafuu jambo ambalo ni kosa kisheria.     
                           
Akizungumza na  wananchi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ununuzi wa karafuu, Mkuu wa Wilaya ya Wete Rashid Hadid Rashid ameviagiza vikosi kuhakikisha mizigo yote inafanyiwa upekuzi ili kudhibiti ujanja unaofanywa na baadhi ya wananchi.

Mkuu huyo wa Wilaya  amewataka wananchi kushirikiana  katika kudhibiti hali hiyo ili kuiwezesha Serikali kufanikisha azma yake ya kulinda karafuu dhidi ya wahujumu wa uchumi wanaojali zaidi maslahi yao .

Naye mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Wete, Hamad Omar Suleiman amesema ni vyema wananchi kufuata sheria bila ya kushurtishwa, ambapo jeshi la Polisi halitakuwa na huruma na atakayekamatwa akifanya udanganyifu huo .

Wananchi hao wameahidi kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitafanikisha kukamatwa wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria lengo ni kukomesha tabia hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.