STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 15.08.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewaahidi wananchi
wa vijiji vya Ukongoroni na Charawe kuwa ndani ya miezi 12 barabara yao
itajengwa kwa kiwango cha lami na kuwataka wawe na subira kwani hatua hiyo ni
kutekeleza ahadi yake kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Dk. Shein alitoa ahadi hiyo leo katika ziara yake
ya kutembelea miradi ya maendeleo sambamba na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 inavyotekelezwa katika Mikoa yote ya Unguja
na Pemba, ziara inayoendelea Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo vijiji
hivyo vimo ndani ya Wilaya hiyo.
Akiwa katika kijiji cha Ukongoroni mara baada ya
kukagua shamba la kilimo cha midimu alipata fursa ya kuwaeleza wananchi
waliofika katika banda wanalohifadhia ndimu zao kuwa kutiwa lami kwa barabara
zao hizo za Ukongoroni na Charawe ni utekelezaji wa ahadi ya chama chake ambayo
aliahidi yeye mwenyewe.
Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuwepo kwa
changamoto ya upungufu wa vifaa kwa Idara husika ya ujenzi wa barabara (UUB), juhudi
za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwani
tayari ndani ya uongozi wa Serikali anayoiongoza imeweza kuijenga kwa kiwango
cha kifusi.
Aliwaleleza wananchi hao kuwa Serikali yao ya
Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi na kuwahaidi kuwa atahakikisha
vijiji hivyo vinazidi kupata maendeleo endelevu na kamwe vijiji havitokuwa kama
vilivyokuwa hapo siku za nyuma huku akiponmgeza kilimo cha ndimu
kinavyoendeshwa hapo Ukongoroni.
Akiwa kijiji hapo, Dk. Shein aliwataka Mawaziri
husika ambao wananchi walizitaja changamoto walizonazo kupitia Wizara zao
wawahakikishie ni kwa namna gani Serikali kupitia Wizara zao itazitatua
changamoto hizo zikiwemo barabara, afya, elimu, kilimo na sekta nyenginezo.
Ambapo kwa upande wa kilimo Waziri husika wa
Wizara hiyo Hamad Rashid Mohammed alieleza hatua zinazochukuliwa kupitia mradi
wa MIVARF kuwapatia mashine wakulima wa ndimu kwa ajili ya kuzisarifu ili hatimae
wapate soko la uhakika.
Nao wananchi wa kijiji cha Ukongoroni kupitia
Sheha wao Haji Vuaa Khamis walieleza changamoto zinazowakabili ikiwemo barabara
yao yenye urefu wa kilomita 13.7 kutaka kuweka lami pamoja na ile ya Charawe
yenye urefu wa kilomita 12.8, pamoja na uhaba wa madaktari.
Nao Mawaziri wasio na Wizara Maalum kutoka vyama
vya upinzani walipongeza juhudi za Dk. Shein za kuwapelekea wananchi maendeleo
na kuahidi kuwa wataendelea kumuunga mkono kwani maendeleo hayana chama huku
wakiwataka vijana kuiheshimu Serikali na kuyathamini Mapinduzi matukufu ya
Januari 12, 1964.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa huo huko
katika Ofisi za Mkoa wa Kusini Unguja zilizopo Tunguu, Wilaya ya Kati ambapo
taarifa hiyo ilieleza mafanikio, changamoto na utekelezaji wa miradi ya
maendeleo katika Mkoa huo.
Taarifa hiyo ilitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa
kuendelea kuongoza kwa busara, hekima na uadili huku wakipongeza hatua zake kwa
kufanya ziara hizo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar.
Wakati huo
huo, Dk.
Shein aliweka jiwe la msingi katika jengo la CCM Tawi la Kaebona na kueleza kufarajika na ujenzi huo ambapo
wanaCCM hao watapata fursa ya kujadili mambo ya chama chao na kuahidi kuliezeka,
kuliweka milango, madirisha pamoja na kutoa mtaji kwa mradi wa duka lao
wanalolijenga tawini hapo.
Aidha, Dk. Shein aliweka jiwe la Msingi ghala la
kuhifadhia mazao ya JKU huko Cheju na kupongeza juhudi zizochukuliwa na kikosi
hicho chini la kuahidi kuzitekeleza changamoto zilizoelezwa zikiwemo kuwapatia
matreka pamoja na mashine ya kupandia mbegu.
Dk. Shein pia, alikihakikishia kikosi hicho kuwa
Serikali anayoiongoza itaendelea kutekeleza azma ya vikosi vya Serikali vilivyoasisi
na Rais wa Awamu ya kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Katika taarifa iliyosoma na uongozi wa JKU katika
kambi hiyo ya Cheju iliyoanzishwa mwaka 1976, ilioanzishwa kwa lengo la
kuendesha kilimo cha Mpunga wa kutegemea mvua yenye ukubwa wa ekari 85 ambazo
70 zinalimwa mpunga na kunde, 10 kilimo mchanganyiko na 5 kwa ajili ya majengo.
Uongozi huo ulieleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa
ghala hilo umetokana na vianzio vya mapato ya miradi ya Kambi na sio ruzuku
kutoka Serikalini.
Akiwa Mitakawani, Dk. Shein alipata maelezo juu ya
mradi wa maji safi na salama pamoja na kukagua mradi wa kisima cha maji na
kuitaka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kisima
hicho kiwe kimekamilika ili wananchi wa kijiji hicho wapate huduma hiyo ya
maji.
Dk. Shein pia, alizindua Mradi wa kisasa wa
ufugaji wa nyuki huko Dunga na kupata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kati
Mashavu Sukwa juu ya mradi huo ambao Wizara ya Kilimo ulipeleka wataalamu na kuanza
kwa mitego mipya 13.
Alioongeza kuwa kwa kila mtego hupelekea kupatikana
kwa lita kumi za asali ambapo kila lita moja huuzwa kwa TZS elfu 20 hivyo kwa
mara moja mfugaji anapata laki 2 shughuli ambayo anaweza kuifanya mara moja
kila baada ya miezi miwili.
Pia, Dk. Shein alipata fursa ya kukagua kazi za
ujasiriamali za Baraza la Vijana wa Wilaya ya Kati na kupongeza juhudi zao
wanazozichukua katika kuendeleza miradi yao na baadae aliweka jiwe la msingi la
jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja.
Akitoa salamu zake mara baada ya kuweka jiwe hilo
la Msingi, Dk. Shein alipongeza hatua za ujenzi huo zilizofikiwa na Wilaya hiyo
na kueleza kuwa jengo hilo la ghorofa moja litamalizwa ili liwe la mfano wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment