Habari za Punde

Naibu Waziri wa Afya Awataka Wanaotoa Tiba Asili Kufuata Sheria.

Na Maryam Kidiko -Maelezo Zanzibar.
NAIBU Waziri ,Wizara ya Afya Harusi Said Suleiman amelitaka Baraza la Tiba asili kuwachukulia hatuwa wale wote ambao hawafuati sheria katika kutoa huduma za tiba asili.

Hayo ameyasema huko Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja katika sherehe za  maadhimisho ya 15 ya Waganga wa asili Barani Afrika yaliyoambatana na vipimo mbali mbali vilivyopimwa bure kama vile Macho, Sukari,Presha, Ukimwi, Viungo vya Mwili na Kifua Kikuu.

Alisema kuwa Wizara ya Afya haina tatizo kwa wanaotaka kuuza dawa hizo kwa kutowa huduma kwa Jamii ila wafuate sheria zinazotakiwa na sio kuwenda kinyume na sheria hizo.

Aidha amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamvumilia mtu yoyote Yule ataeuza madawa hayo kinyume na taratibu zilizowekwa na Baraza hilo

“Kuna Watu ambao wanauza Madawa ya asili ambayo hayana viwango vinavotakiwa na kusababisha madhara makubwa kwa Jamii na kupelekea vifo visivyotarajiwa’’Alisema Naibu huyo.

Hata hivyo alisema kuwa Serikali itazidi kuwa karibu na Waganga asili ili kuhakikisha kuleta maendeleo mazuri kwa wanaotibiwa kupitia Madawa hayo.

Vile vile alisema zinapotoka nafasi za mafunzo juu ya fani zao wataweza kupatiwa nafasi hizo ili kwenda kujifunza zaidi kwa lengo la kupata taaluma hiyo .

Sambamba na hayo amewaomba Waganga hao kuchukuwa hatua na juhudi kubwa kuweza kuelimisha Jamii juu ya uwepo wa uuzaji wa madawa ya asili yasio na viwango ili kuepukana na matatizo ya Kiafya.

Akiwasisitiza Waganga hao kuwa na mashirikiano na kuhakikisha wanaendelea kutowa huduma nzuri ili kufikia lengo lililokusudiwa.

“Jambo lolote likiwa na mashirikiano litaleta faida kubwa hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja ili lengo lipatikanwe kwa juhudi mtazofanya 
”Aliongezea Naibu Waziri Harusi.

Nae Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Waganga Zanzibar Haji Juma Msanif alisema Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kushirikiana na Jumuiya ya Waganga Zanzibar (JUTIJAZA) kila mwaka wanaendelea kuazimisha sherehe za tiba asili Afrika.

Alisema kwa kuendeleza maadhimisho hayo wameweza kuunda Umoja wa Waganga asili Afrika Mashariki lengo kujua mambo mbali mbali yanayowakabili .

Katibu huyo alisema kuna mashirikiano mazuri kati yao na Madaktari wa Hospitali yanayopelekea hali nzuri ya matibabu kwa wagojwa wanaofika katika vituo hivyo.

“Kutokana na mashirikiano mazuri kati yetu imepelekea kupeana Rufaa kwani Magojwa yanayohusu hospitali tunawapelekea wao na yanayotuhusu sisi wanatuletea’Alisema Haji Msanif.

Akifafanuwa zaidi alisema Jamii imekuwa ikiziamini Dawa za asili kwa kuamini kwao kumeweza kufunguliwa kliniki mbali mbali za Madawa hayo ambazo zinaendeshwa na watu wenye asili ya Eshia kama vile Wachina na Wakorea.

Aidha amezielezea Kliniki hizo kuwa zinauwezo mkubwa wa kutumia vifaa vya Kimagharibi katika kuendesha matibabu yake jambo ambalo linavutia kwani kliniki hizo zimeweza kufata sheria.

Maazimisho hayo huazimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Agosti , ambapo 

kauli mbiu ya mwaka huu ni UJUMUISHAJI WA TIBA ASILI KATIKA MIFUMO YA AFYA TULIPOFIKA HAPA,
                                             
                      IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.